Virusi vya Corona: Wanasayansi nchini Australia waanza kufanya majaribio ya chanjo mbili

Wanasayansi nchini Australia wameanza kufanya majaribio ya dawa mbili zinazoweza kuwa chanjo dhidi ya virusi vya corona.

Hiyo inatajwa kuwa ni "hatua muhimu " ya majaribio ya maabara.

Chanjo hizo zilizotengenezwa na Chuo Kikuu cha Oxford na kampuni ya Marekani ya madawa - Inovio Pharmaceutical, zimeidhinishwa kufanyiwa majaribio kwa wanyama na Shrika la Afya Duniani (WHO).

Shirika la taifa la sayansi nchini Australia litatathmini kama chanjo hizo zinafanya kazi, na iwapo zitakuwa salama kwa binadamu.

Majaribio ya kwanza kwa binadamu yalifanyika nchini Marekani mwezi uliopita, lakini hata hivyo yaliruka hatua ya majaribio kwa wanyama.

Kuna chanjo nyingine kadhaa zinazofanyiwa uchunguzi katika maeneo mbali mbali duniani kwa sasa kwa kasi isiyo ya kawaida.

Lakini wanasayansi wa Jumuiya ya Madola wa Australia na Shirika la Utafiti wa kisayansi (CSIRO) wanasema vipimo vyao vitakuwa ni vya kwanza vilivyokamilika vya kutumia mnyama kabla ya kufanyika kwa vipimo halisi vya kliniki.

Watafiti wanasema kasi na kiwango cha ushirikiano uliowawezesha kufikia hatua hii havikutarajiwa.

"Kwa kawaida inaweza kuchukua takriban mwaka mmoja hadi miwili kufikia hapa tulipo, na kusema ukweli tumefupisha kipindi hicho hadi miezi," Dkt Rob Grenfell kutoka CSIRO amewaambia waandishi wa habari Alhamisi.

Itafanya kazi vipi?

Katika kipindi cha siku chche zilizopita timu ya CSIRO iliingiza sampuli za chanjo katika mwili wa pandaporiambaye alithibitishwa kuwa na maambukizi ya coronavirus sawa na anavyoambukizwa binadamu.

Sars-CoV-2 ni virusi ambavyo husababisha ugonjwa wa Covid-19. Kuna walau chanjo 20 zinazotengenezwa kote duniani.

CSIRO inafanyia vipimo aina mbili zilizochaguliwa na taasisi inayosimamia nyingi kati ya tafiti hizi duniani ya Umoja wa Ugunduzi dhidi ya Maradhi ya Kuambukiza.

Aina moja, iliyotengenezwa na Chuo Kikuu cha Oxford, ni chanjo ya wadudu. Hutumia virusi vyenye "kasoro" kuweka protini za virusi vya corona kwenye mfumo wa kinga ya mwili na kupata jibu.

"Lakini haviwezi kuzaliana … kwa hiyo hakuna uwezekano wa kuugua kupitia chanjo hii," anasema Profesa Trevor Drew, mkurugenzi wa Maabara ya Afya ya Wanyama ya Austarlia katika mji wa Victoria, ambako kipimo hicho kinafanyika.

Ameielezea chanjo nyengine pia -kutoka Inovio - kuwa "ni ya tofauti kabisa lakini pia inaleta matumaini".

Imebuniwa kuweka aina fulani ya protini katika virusi vya corona katika mfumo wa kinga ya mwili, na kuamsha seli za mwili kuzalisha protini hizo kabla ya mfumo wa kinga ya mwili kuanza kujilinda."

"Ni jambo la muhimu sana kuwa na njia mbadala katika kuliendea hili," ameeleza Profesa Drew. "Inatupatia uwezekano mkubwa wa kufaulu."

Majibu yanaweza kupatikana lini?

Majibu ya awali kutoka kwa wanyama yatatolewa mapema mwezi Juni, wanasayansi hao wameeleza.

Kama zitafaulu, basi chanjo hizo zitapandishwa katika ngazi ya majaribio kwa binadamu na yatafanyika katika maabara za sehemu nyengine pia.

Katika hatua hiyo, kasi ya kupata dawa katika soko la jumla inaweza kuongezeka, lakini wataalamu wanaonya kuwa bado itachukua muda wa walau miezi 18 kutimiza muda wa usimamizi na viwango.

Chanjo ya Chuo Kikuu cha Oxford, kwa mfano, inajaribiwa na maabara nyingine kwa kutumia myama mwingine kando na wasimamizi wa viwango wa Marekani.

"Chanjo zote zinazofanyiwa majaribio zinachunguzwa pia na kampuni na mashirika mengine kwa sababu hakuna shirika moja linaloweza kutengeneza chanjo peke yake," anasema Dkt Grenfell.

Lakini anasema ana ''matumaini'' juu ya kazi inayofanyika, kutokana na kiwango cha ushirikiano wa dunia katika kutekeleza hilo.

"Huu ni ushirikiano wa dhati baina ya wasomi, umma, na pia sekta binafsi ambao umewezesha kusema ukweli kupata mafanikio kwa wakati huu," alisema