Coronavirus: Habari za kupotosha zilizosambazwa Afrika kuhusu virusi vya corona?

zaidi ya mataifa 40 ya Afrika yameripoti visa vya coronavirus

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, zaidi ya mataifa 40 ya Afrika yameripoti visa vya coronavirus

Nchi za Afrika zimekuwa na ongezeko la idadi ya visa vipya vya ugonjwa wa corona na serikali nyingi kwa sasa zimeweka sheria kali za watu kutosongeleana.

Wakati zinaendelea kujitayarisha kwa ongezeko zaidi la visa hivi, kumekuwa na taarifa nyingi za kupotosha kote barani Afrika.

1. Chanjo haifanyiwi majaribio barani Afrika

Kuna taarifa nyingi zinazosambazwa katika mitandao ya kijamii zinazodai kwamba watu wa Afrika watatumiwa katika majaribio ya chanjo dhidi ya virusi vya corona kama ilivyokawaida kwa panyabuku.

Hatahivyo, madai kama hayo si ya kweli - hakuna chanjo ya Covid 19 na ni majaribio kidogo tu ya chanjo hiyo yanayoendelea kwasasa na hakuna yanayofanyika katika bara la Afrika.

Hatujui madai haya yalianzia wapi lakini zaidi yanazungumzia vile watu wa Afrika watapewa chanjo katika majaribio ya ikiwa ni salama kwa matumizi ya mataifa ya Magharibi.

Moja wapo ni video katika mtandao wa Youtube inayomuonesha mwanamke anayezungumza Kifaransa akisema: "Kwa sasa kuna chanjo kwa ajili ya raia wote wa Afrika lakini hakuna hata chanjo moja ambayo imepatikana kwasababu ya nchi za Magharibi.

Kwahiyo, ninasihi ndugu zangu wa Afrika musikubali kutumia chanjo yoyote." Video hiyo imetazamwa na zaidi ya watu 20,000 huku watumiaji wengi wa mitandao ya kijamii wakionesha kumuunga mkono.

Video nyengine katika mtandao wa Youtube inaendeleza madai sawia na hayo kwamba chanjo ya majaribio itatumiwa kwa raia wa Afrika ili kuthibitisha ikiwa ni salama kwa matumizi kabla ya kuanza kutumika katika nchi tajiri.

Hofu kuhusu chanjo si jambo geni katika baadhi ya maeneo ambayo watu hawaamini dawa za hospitalini.

Katika nchi zinazozungumza Kifaransa barani Afrika, kuna uvumi kuwa chanjo ya Covid 19 imesambaa, na pia kulikuwa na madai sawia na hayo na taarifa za kupotosha kuhusu chanjo ya Ebola, tiba ambayo imechangia katika kukabiliana na ugonjwa huu.

Vipimo vya coronavirus Afrika Kusini
Maelezo ya picha, Vipimo vya coronavirus Afrika Kusini

2. Kuwa mweusi siyo kinga ya kutopata Covid-19

Kumekuwa na mijadala kadha katika mitandao ya kijami kuhusu rangi ya ngozi ya mtu na kinga ya mwili dhidi ya ugonjwa wa corona.

Machi 13 Waziri wa Afya nchini Kenya alifutilia mbali uvumi kuwa ''wale wenye ngozi nyeusi hawawezi kushikwa na coronavirus".

Tulizungumza na Professor Thumbi Ndung'u kutoka Chuo cha mafunzo ya Tiba cha Nelson R Mandela, Durban ambaye alisema "hakuna ushahidi wowote wa kuthibitisha hilo - na hakika, tunachofahamu ni kwamba watu weusi pia wanapata ugonjwa huu."

3. Chai ya rangi haitibu coronavirus

Kuhakikisha unakunywa maji mengi ni vizuri lakini kunywa chai ya siturungi sio tiba ya Covid 19 kama ambavyo imekuwa ikidaiwa.

Vyombo vya habari nchini Kenya vimekuwa vikiangazia madai ya uongo kwamba kwamba unywaji wa chai unaweza kutibu coronavirus
Maelezo ya picha, Vyombo vya habari nchini Kenya vimekuwa vikiangazia madai ya uongo kwamba kwamba unywaji wa chai unaweza kutibu coronavirus

Kulingana na vyombo vya habari vya eneo nchini kenya, watu wamekuwa wakipigiana simu na kuarifiana kwamba wanywe chai ya rangi kuzuia wasishikwe na ugonjwa wa corona - na iwapo hawatafanya hivyo watakufa kwasababu ya ugonjwa huu.

Hii ni dhana tu ambayo imesambaa kila mahali na wala haijathibitishwa kwa misingi ya tiba.

Wanasayansi kote duniani wanafanya utafiti na pengine chanjo huenda ikapatikana lakini inavyotarajiwa ni kwamba hakuna chanjo itakayokuwa tayari hadi pengine katikati ya mwaka ujao.

4. Huna haja ya kunyoa kidevu chako kujilinda dhidi ya virusi

Mchoro wa zamani uliochorwa na mamlaka ya afya ya Marekani kuhusu ndevu na upumuaji umekuwa ukitumiwa vibaya na kupendekeza kwamba wanaume wanastahili kunyoa ndevu zao ili wasipate coronavirus.

Kichwa cha habari katika gazeti la The Nigerian Punch kimeandikwa: "Kujilinda dhidi ya coronavirus, nyoa ndevu zako, CDC imeonya"

Huna haja ya kunyoa kidevu chako kujilinda dhidi ya virusi
Maelezo ya picha, Huna haja ya kunyoa kidevu chako kujilinda dhidi ya virusi

Mchoro wa Kituo cha Udhibiti wa Magonjwa Marekani (CDC) unaonesha mifano kadhaa ya nywele za usoni na zile ambazo unastahili kuziepuka wakati unavaa barakoa.

Kuna aina za kunyoa videvu ambazo zimepitishwa na zingine zimekatazwa kwa misingi kwamba zinaingiliana na valvu na kuzuia mfumo wa upumuaji kufanyakazi vizuri.

Mchoro huo ni wa kweli lakini uliundwa mwaka 2017 kabla ya kutokea kwa mlipuko wa corona kwa wafanyakazi ambao wanavaa barakoa.

Tofauti na kile ambacho kimekuwa kikiripotiwa, kituo cha CDC hakijawahi kuuchapisha mchoro huo katika siku za hivi karibuni na wala hakijapendekeza kwamba watu wanastahili kunyoa videvu kwa mtindo fulani.

Vichwa vya habari sawa na hivyo vimeshuhudiwa katika nchi zingine pia na kusambazwa na maelfu ya watumiaji wa mitandao ya kijamii.

Shirika la habari la Australia la 7News liliandika ujumbe kwenye mtandao wa kijamii: "Vile kidevu chako kinaweza kuongeza hatari ya kupata coronavirus bila kujua."

Kwasasa, wizara ya afya Uingereza inashauri kwamba wakati ambapo barakoa ni muhimu kwa wahudumu wa mahospitali, kuna ushahidi kidogo wa umuhimu wake kwa umma".

5. Mhubiri wa Nigeria akabiliana na virusi vya corona

Mhubiri mmoja wa kanisa la kiinjilisti anayedai kwamba anaweza kutibu virusi pia naye amekuwa akitoa taarifa za uwongo.

Picha ya zamani

Taarifa kumhusu David Kingleo Elijah kutoka kanisa la Glorious Mount of Possibility zilianza kusambaa mitandaoni baada ya video inayomuonesha akisema kuwa ataenda China na kuharibu kirusi hicho ilipowekwa kwenye mtandao wa Youtube na kusambazwa katika mitandao mingine.

"Nitaharibu coronavirus kwa nguvu ya unabii. Ninakwenda China, ninataka kuharibu kirusi cha corona," anasema hivyo kwenye video.

Siku chache baadaye, taarifa zikasamba tena kwenye mablogi zikidai kwamba alisafiri China lakini amelazwa hospitali baada ya kupata ugonjwa wa corona. Ingawa mablogu wanamtambulisha mhubiri huyo kwa jina tofauti la Elija Emeka Chibuke.

Picha iliyokuwa inamuonesha akiwa hospitali ni ya Adeshina Adesanya, msanii wa Nigeria maarufu kama Mhubiri Ajidara, aliyeaga dunia hospitalini mwaka 2017..

6. Kunywa supu ya pilipili siyo dawa.

Nchini Nigeria, mhubiri mmoja aliweka video na tangazo akidai kwamba supu ya pilipili ni tiba ya coronavirus.

Madai hayo pia yalisambazwa katika mtandao wa WhatsApp.

Hakuna tiba kwasasa wala matibabu maalum ya coronavirus na madai hayo hayana ufafanuzi wa kina wa tiba inayopatikana katika supu ya pilipili - mlo wa kitamaduni wa Nigeria wenye pilipili.

WHO imesema kwamba mlipuko huo umesababisha taarifa za uwongo zenye kupotosha.

Katika nchi ya Cape Verde, taifa la magharibi mwa Afrika lenye kuzungumza kireno, kuna ujumbe uliosambaa katika mtandao wa kijamii ukidai kuwa daktari wa Brazil alipendekeza chai ya shamari kama tiba ya virusi vya corona. Hilo lilifanya watu kukimbilia kununua kiungo hicho katika masoko ya eneo, kwa mujibu wa shirika la habari la AFP.

Hata hivyo, wizara ya afya ya Brazil imeonya watu kutosambaza taarifa zenye kupendekeza kwamba kiungo cha shamari ni tiba ya coronavirus.

Aidha Shirika la Afya Duniani limesema kwamba uoshaji mikono kwa njia sahihi ni muhimu katika kupambana na kuzuia maabukizi.