Coronavirus: Jinsi virusi vya corona vinavyowaathiri watu kiakili

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Na Faith Sudi
- Nafasi, BBC Swahili
Maambukizi ya virusi vya corona yalipotangazwa kuwa janga la dunia mapema mwezi huu, mataifa mengi duniani yaliamua kuchukua hatua ambazo waliamini kwamba zitawakinga raia wao kutopata maambukizi ya ugonjwa huo.
Viongozi wa mataifa ya Afrika Mashariki mmoja baada ya mwingine walitoa taarifa kwa vyombo vya habari wakitoa mwelekeo wa hatua ambazo wamechukua kuhakikisha kwamba wanadhibiti maambukizi ya virusi vya Corona.
Baadhi ya hatua zilizochukuliwa na mataifa ya Afrika Mashariki ni kusitisha: safari za ndege za nje au ndani ya nchi, mikutano ya hadhara, kufungwa kwa shule zote suala ambalo limeathiri maisha ya kawaida ya jamii.
Lakini hatua ambayo imepuuzwa na ambayo ni muhimu ni ile ya afya ya kiakili.
Katiba ya WHO inasema kwamba " Afya ni hali ya kuwa na afya bora kamilifu kimwili, kiakili na kijamii na wala sio tu kutokuwa na magonjwa mwilini au akilini"
"Afya mbaya ya kiakili uhusishwa na mabadilko ya haraka ya jamii, dhiki katika mazingira ya kazini, ubaguzi wa kijinsia, magonjwa mwilini, ukiukwaji wa haki za kibinadamu na kadhalika." kulingana WHO.

Chanzo cha picha, Getty Images
Tukizingatia eneo la Afrika Mashariki tangu kuanza kwa mlipuko pamoja na kuenea kwa virusi vya Corona, baadhi ya hatua zilizochukuliwa zimesababisha mabadiliko ya haraka katika maisha ya kila mtu na ambayo ndiyo hali ilivyo hadi kufikia sasa.
Wasiwasi, hofu na suita fahamu ndiyo hali ya maisha ya sasa katika ukanda huu.
Kwanza, wazazi walipewa siku chache kuwachukua watoto kutoka shuleni. Hii ilimaanisha kwamba iwapo haukuwa umehifadhi pesa za shughli za dharura, ulijikuta katika njia panda kwa sababu kwa kawaida, katika muhula wa kwanza wanafunzi hurejea nyumbani mwanzoni mwa mwezi wa Aprili.

Chanzo cha picha, Wambui
Wambui Waiganjo ni mzazi kutoka nchini Kenya. Mmoja wa watoto wake alikuwa katika shule ya mabweni na wakati rais alipotangaza kwamba shule zote zinafungwa, alikuwa na wasiwasi kuhusu jinsi mtoto wake atakavyofika nyumbani.
" Siku hiyo sikuweza kufanya kazi. Kila wakati nilimpigia mwalimu simu kumuuliza iwapo watoto wameshaondoka shuleni. Aliponiambia wameondoka, hofu yangu kuu ilikuwa ni iwapo atafika nyumbani, kwa sababu hakuna jinsi tungeweza kuwasiliana naye... Kuna wakati hata nilihisi amechukua muda mrefu ningeenda mwenyewe shuleni nikamchukue"
Hata hivyo anasema kwamba alilazimka kufanya ununuzi wa dharura wakati aliposikia kwamba wanafunzi wanarejea nyumbani.
"Nilienda kinyume na bajeti yangu kwa sababu chakula ambacho kingenitosha mimi kwa wiki mbili, kisha kijana aje kutoka shuleni… hicho kwa hakika kingekuwa cha wiki moja tu… Kwa hivyo hilo liliwacha pengo kwenye bajeti yangu."
Wambui ambaye ni msimamizi wa kampuni ya African Fine Coffees tawi la Kenya hajaathirika na agizo la kufanyia kazi nyumbani kwani ofisi yake ipo nyumbani kwake lakini anasema kwamba wasiwasi wake kuu ni jinsi ugonjwa huo unavyosambaa. Hali hii anasema imemfanya kuwa na kiwewe.
"Kila wakati ninaketi nikiwaza kwamba natumai sijagusa kitu ambacho kitanifanya nipate maambukizi. Na wakati ninaporudi nyumbani, kitu cha kwanza ni kuingia katika bafu na kuosha nguo zangu zote. Ninaishi kwa wasiwasi... Kiwewe kimekuwa sehemu ya maisha yangu"
Kila mtu ameathirika kwa njia moja au nyingine. Sherehe za harusi na matanga, usafiri na utalii, biashara na ajira. Maisha kwa kweli yamebadilika.

Chanzo cha picha, Gladys Njeri
Kinyume na Wambui ambaye ofisi yake ni nyumbani kwake, Bi Gladys Njeri ambaye pia ni mzazi amelazimika kufanyia kazi nyumbani kufuatia agizo la rais Kenyatta kama njia moja ya kudhibiti maambukizi. Lakini kwake ni changamoto si haba.
"Nikienda kwenye chumba cha malazi kujaribu kufanya kazi watoto wananifuata… Nikiwasiliana na mteja kwenye simu, wanataka pia kuzungumza naye… Ha ha ha… Ni vigumu sana" anasema Gladys huku akicheka kwa kejeli
Gladys anasema kwamba jinsi idadi ya watu wanaoambukizwa inavyozidi kuongezeka ndivyo wasiwasi wake unazidi kuongezeka.
"Ninakosa usingizi...Ninashindwa kulala. Ninafikiria tu jinsi nitakavyopata pesa. Kwa sababu kazi ninayoifanya ni ya malipo baada ya kazi. Na hapa nyumbani siwezi kabisa kufanya kazi. Hii inanipa msongo wa mawazo."
Katika kanda ya bara Afrika Mashariki utalii, uchukuzi na mikahawa ni baadhi ya biashara zilizoathirika zaidi. Wafanyikazi wengi katika sekta hizi walilazimika kuenda nyumbani.
Siku ya Jumatano, rais Uhuru Kenyatta alitangaza amri ya kutotoka nje usiku kuanzia Ijumaa tarehe 27. Amri hii inatazamiwa kuathiri hata zaidi biashara hasa ile ya wachuuzi wadogo wadogo.

Chanzo cha picha, Mwanasaikolojia Loice Noo
Ni mabadiliko kama haya katika hali ya kawaida ya maisha ambayo Mwanasaikolojia Loice Noo wa chuo kikuu cha kikristo cha Pan Africa anasema kwamba yanasababisha mkanganyiko.
" Mabadiliko kama haya huleta hasara kubwa kama vile kubadilisha mazingira ya kazi, na pia husababisha mtu kuwa katika hali ya kushindwa kujua Kwanini? Kivipi? Lini? Wapi? Nini?... Hii humfanya mtu kuwa na wasiwasi na kiwewe."
Loice anasema kwamba mitandao ya kijamii pia inachangia kwa kiasi kikubwa katika kuathirika kwa akili wakati kama huu ambapo watu wana maswali mengi kuhusu hali ilivyo.
" Watu wengi wanatumia muda mwingi kwenye mitandao ya kijamii kusoma kila taarifa kuhusu Corona ambazo zinawaathiri kiakili kwa kuwasababisha kuwa na wasiwasi. Kwa sababu si kila taarifa inayochapishwa ni ya kuwaelimisha watu na kuwatia moyo"
"Watu wanapaswa kujipumzisha na taarifa zozote kuhusu Corona. Kama mimi nachukua wakati huu kupika na watoto wangu na kusafisha boma letu. Watu wajihusishe na mambo ambayo yanawasadia kupumzisha akili. Na muhimu zaidi kuzingatia mwelekeo waliopewa wa kuosha mikono kwa sabuni na maji kila mara, kutoslimiana kwa mikono, na kutoshika nyuso zao ili kujilinda na maambukizi ya virusi vya corona."
Hata hivyo, Bi Loice anashauri kwamba iwapo unahisi kwamba unazongwa na mawazo, 'zungumza' na mtu yeyote ambaye unahisi na unajua kwamba atakusikiliza hata kama ni kwa njia ya simu. Na kwamba tuwape sikio wale wanaotuzungumzia kwani ndiyo njia pekee ambayo tunaweza kusaidiana kwa sasa.
Waingereza husema 'kuzungumza ni kutatua'.
Magonjwa ya mwili yanasemekana kuwa na uwezo wa kumfanya mtu kupatwa na ugonjwa wa kiakili kwa sabau hali ya mtu ya afya uhusishwa na homoni nyingi ambazo zinaweza kuathiri akili ya ta mtu.
Magonjwa sugu kama vile saratani, ukimwi na ugojwa wa kisukari huathiri akili na hali ya maisha ya watu.
Kupimwa na kupatikana na ugonjwa unaeza kumsababishia mtu huzuni na mshtuko. Hisia kama hizi ni za kawaida na hisia hizi pekee haziwezi kutumiwa kikamilifu kama ishra ya ugonjwa wa akili bali pia zinaweza kuchangia msongo wa mawazo ambao huenda ukawa na athari kubwa .
Wakati mwingine si ugonjwa unaoleta msongo wa mawazo ila matibabu yanayotumika.

Magonjwa mengine husababisha ongezeko la sukari kwenye damu ambayo huathiri jinsi akili inavyofanya kazi.
Watu wanaoishi na magonjwa sugu mara kwa mara hukumbwa na msongo wa mawazo na uchungu ambao uhusishwa na wasiwasi.
Mental health is a state of well-being in which an individual realizes his or her own abilities, can cope with the normal stresses of life, can work productively and is able to make a contribution to his or her community.
Afya ya akili ni hali ya ambayo mtu anaweza kutambua uwezo wake , kukabiliana na dhiki za kawaida za maisha, kuweza kufanikiwa na na jinsi anavyoweza kuchangia pakubwa katika maendeleo ya jamii kwa jumla
Mambo kadhaa ya kijamii, kisaikolojia na baiolojia huchangia kiwango cha afya ya akili ya mtu. Kwa mfano ghasia, shinikizo za kijamii na kiuchumi zinatambulika kuwa hatari katika afya ya kiakili.
Afya mbaya ya kiakili uhusishwa na mabadilko ya haraka ya jamii, mazingira mabaya ya kazi,, ubaguzi wa kijinsia, magonjwa mwilini, ukiukwaajwa haki z a kibinadamu na kadhalika.












