Coronavirus: Je ndevu zinakuhatarisha kupata maambukizi ya ugonjwa huu?

Wafanyakazi wa afya nchini Uingereza sasa wametakiwa kunyoa ndevu zao ili kuruhusu barakoa kuzuia maambukizi.

Chanzo cha picha, CDC

Maelezo ya picha, Wafanyakazi wa afya nchini Uingereza sasa wametakiwa kunyoa ndevu zao ili kuruhusu barakoa kuzuia maambukizi.

Madai ya kushangaza kwamba wanaume wanaonywa kunyoa ndevu zao ili kujilinda dhidi ya virusi vya corona yamesambaa katika mitandao ya kijamii.

Onyo hilo linatoka katika picha iliotolewa na kituo cha Marekani cha kudhibiti magonjwa CDC, ikionyesha aina ya ndevu zinazoweza kumfanya mtu kuambukizwa virusi vya ugonjwa huo hatari.

Baadhi ya vyombo vya habari na mitandao ya kijamii vimetumia picha hiyo kama onyo jipya kwamba wanaume wenye aina fulani ya ndevu wanatakiwa kunyoa ili kuzuia kuambukizwa ugonjwa huo.

Tatizo ni kwamba picha hiyo ya CDC haikutolewa kuhusiana mlipuko wa virusi vya corona.

Ukweli ni kwamba ilichapishwa mwaka 2017 katika blogi iliowalenga wale wanaume wenye ndevu kazini.

Blogi hiyo ilielezea: Nywele zilizopo usoni kama vile masharubu, na ndevu ambazo zinakaribia eneo ambalo mwanadamu hutumia kupumua zinaweza kuzuia barakoa kufanya kazi yake kama inavyohitajika.

Mbali na blogi hiyo, barakoa nyingi ambazo zimekuwa zikitumiwa ili kujilinda dhidi ya ugonjwa huo hazifuniki vizuri pua na mdomo zinazotumika kupumua.

Wafanyakazi wa afya nchini Uingereza sasa wametakiwa kunyoa ndevu zao ili kuruhusu barakoa kuzuia maambukizi.

Mzee mwenye ndevu

Chanzo cha picha, Getty Images

Maafisa wakuu wa hospitali nchini humo katika chuo kikuu cha Southampton wametuma barua pepe kwa wafanyakazi huku picha hiyo ikiwa imeandamana na barua hiyo, ikizungumzia kuhusu tatizo hilo na barakoa zisizoweza kuziba vizuri nyuso zenye ndevu nyingi.

Barua kutoka kwa mkurugenzi wa matibabu Derek Sandeman anasema kwamba nywele za usoni zinazuia uwezo wa barakoa kuzuia maambukizi.

Anaongezea: Ninaandika kuwaarifu wale ambao hawana Imani za kidini kuhusu ufugaji wa ndevu ama utamaduni na ambao wanafanya kazi katika maeneo hatari kufikiria kunyoa.

"Natambua kwamba kwa wengine hili ni suala kubwa. lakini ninaamini kwamba hiki ndio kitu muhimu."

Kulingana na afisa wa maswala ya usalama wa kiafya ndevu huzuia barakoa kuzima maeneo ya mwanadamiu anayotumia kama vile mdomo na pua.