Coronavirus: Mwanafunzi wa Cameroon asimulia alivyopona

Chanzo cha picha, Pavel Daryl Kem Senoua
Kabla Kem Senou Pavel Daryl, mwenye umri wa miaka 21-ambaye ni mwanafunzi raia wa Cameroon anayeishi katika mji wa Jingzhou, kuambukizwa virusi vya corona, hakuwa na mpango wa kuondoka China, hata kama hilo lingewezekana.
"Chochote kitakachofanyika sitaki kupeleka ugonjwa Afrika," alisema akiwa katika chumba chake cha malazi katika Chuko Kikuu, ambako ametengwa kwa siku 14.
Alikuwa anaugua homa kali, kukohoa vibaya na kuonyesha dalili za mafua. Alipokuwa mgonjwa alikumbuka jinsi alivyopata malaria akiwa mtoto Cameroon. Alihofia sana maisha yake.
"Nilipokuwa nikienda hosipitali kwa mara ya kwanza nilikuwa nikiwaza kifo na jinsi ambavyo huenda ikanitokea," alisema.
Kwa siku 13 alitengwa katika hospitali moja nchini China.
Alitibiwa kwa antibiotiki na dawa za kutibu wagonjwa walio na virusi vya Ukimwi, HIV. Baada ya wiki mbili ya uangalizi alianza kuonesha dalili ya kupona.
Uchunguzi wa kimatibabu wa CT scan haukuonesha dalili zozote za ugonjwa.
Alikuwa mtu wa kwanza mwenye asili ya kiafrika aliyepona baada ya kuambukizwa na virusi hatari vya corona.China aligharamia matibabu yake.

Chanzo cha picha, Pavel Daryl Kem Senoua

Misri ni nchi ya kwanza ya Afrika kuthibitisha kisa cha maambukiza ya virusi vya corona.
Wataalamu wa Afya wameonya kuwa nchi zlizo na mifumo hafifu za matibabu huenda zikakabiliwa na changamoto ya kukabiliana na mlipuko wa virusi hivyo, ambavyo vimesababisha vifo vya watu zaidi ya 1,600 na wengine zaidi ya 68,000 kupata maambukizi wengi wao nchini, China.
"Sitaki kurudi nyumbani kabla nikamilishe masomo yangu. Nadhani hakuna haja ya kurudi nyumbani kwasababu gharama zote za hospitali zimesimamiwa na serikali ya China," alisema Bwana Senoua.
Kuwaondoa au la?
Tangu mwezi Januari, serikali za mataifa tofauti duniani, zikiongozwa na Marekani, zilianza mpango wa kuwaondoa raia wao kutoka mji wa Wuhan na miji mingine jirani.
Lakini maelfu ya wanafunzi wa matafa ya Afrika, wafanyikazi na familia zao, wamesalia katika mkoa wa kati wa Hubei uliowekewa vikwazo vya usafiri ili kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona - Mlipuko wa virusi hivyo ulianza katika mji wa Wuhan ambao ni makao makuu ya mkoa- na wengine wanashinikiza serikali zao kuchukua hatua ya kuwasaidia.
"Sisi ni wana wa Afrika lakini Afrika haiko tayari kutuokoa wakati huu tunaohitaji msaada wa dharura," anasema Tisiliyani Salima, mwanafunzi anayesomea matibabu katika chuo kikuu cha matibabu cha Tongji na rais wa chama chwa wanafunzi wa Zambia mjini Wuhan.

Fahamu zaidi kuhusu virusi vya corona

Chanzo cha picha, Getty

Kwa karibu mwezi mmoja Bi Salima amekuwa akiishi kwa kujitenga mwenyewe.
Maisha kwa mwanafunzi huyo wa miaka 24 yameanza kupoteza maana. Anatumia muda wake mwingi kufuatilia taarifa za ugonjwa huo katika mitandao ya kijamii ya China
Amekuwa kama daraja la mawasiliano kati ya ubalozi wa Zambia na wanafunzi 186 wa Zambia wanaoishi katika mji wa Wahun uliotengwa ili kudhibiti maambukizi.
Wengi wao wanahofia usalama wa chakula, upatikanaji wa huduma muhimu na ukosefu wa taarifa katika mji huo ambao wiki hii umeshuhudia vifo vya watu 100 kwa siku.
Aliona wanafunzi wenzake wa kimatifa wakiondolewa katika eneo hilo huku yeye na wanafunzi raia wenzake wakiachwa nyuma.
"Mataifa ya kusini mwa jangwa la Sahara yamekuwa katika hali hiyo," anasema mmoja wa wanafunzi aliyekubali kuzungumza na BBC kwa masharti kwamba asitambulishwe.
"Hadharani na pembene mataifa ya Afrika yanasema China ina uwezo wa kukabiliana na janga hilo la kiafya. Lakini hali ya maambukizi haijadhibitiwa ipasavyo. Ukifuatilia tamko rasmi unapata hisia kwamba mataifa ya Afrika hayataki kukosea China. Hatuna uwezo wa kujitetea," alisema mwanafunzi huyo.

Chanzo cha picha, EPA
China kwa sasa ni mshirika mkuu wa kibiashara wa Afrika na uhusianao kati yake na mataifa ya bara hilo umeendelea kuimarika katika miaka ya hivi karibuni.
Hatua ambayo imefanya China kuwa mwenyeji wa wanafunzi takriban 80,000 wa kiafrika, wengi wao wakivutiwa kusoma huko kutokana na mpango wa msaada wa elimu uliotolewa na utawala wa nchi hiyo.
Lakini viongozi wa kijamii wanasema watoto wadogo kwa wakubwa, na familia zimeachwa Hubei huku wakipata msaada kidogo au bila mchango wowote wa serikali zao.
"Watu wanasema: 'Tusirudishwe nyumbani kwasababu Nigeria haiwezi kutuhudumia.'Nahisi vibaya kwasababu mwisho wa siku mimi pia ni mwanadamu," anasema Angela, mhitimu wa hivi karibuni wa a kutoka Nigeria, ambaye alipeana jina lake la kwanza tu.
"Ningelishukuru sana laiti wangelitambua uwepo wa Wnaigeria hapa lakini inaoneka hilo sio jambo la msingi. Hatupati jibu lolote kutoka kwa serikali yetu," anasema.

Chanzo cha picha, AFP
Wiki iliyopita kwa mara ya kwanza katika siku 22 tangu mji huo kuwekwa chini ya uangalizi, ukosefu wa chakula ulimlazimu Angela kutoka nyumbani kwake kwenda kununua bidhaa hiyo muhimu.
"Mji huo umesalia mahame. Nilipotoka katika jengo hilo nilikuwa na hofu huenda nisiruhusiwe kurudi humo. watu wanapimwa viwango vya joto nje ya lango,"alisema katika mahojiano ya simu kutoka nyumbani kwake.
'Tunahisi kutelekezwa'
Baadhi ya mataifa yamekuwa yakiwatumia wanainchi wake msaada wa kifedha .
Kwa mujibu wa mkuu wa chama cha wanafunzi wa Ivory Coast nchini Wuhan wanafunzi 77 wa nchi hiyo walipewa dola 490 kufuatia mashauriano ya wiki moja na serikali yao. Lakini wengi wao wanalalamika serikali ilichukua muda kufikia uamuzi huo.
Ghana pia imeripotiwa kuwatumia usaidizi wa kifedha raia wake nchini China.
"Kuisha hapa hakutuhakikishii usalama wetu. Tuko tu katika nchi ambayo ina mifumu mizuri ya kimatibabu," anasema Bi Salima.
"Tunahisi kutelekezwa. China ilikasirishwa na hatua ya Marekani kuondoa raia wake ikisema hatua hiyo ilizua hali ya taharuki," alisema mwanafunzi mmoja aliyekubali kuzungumza na BBC kwa masharti kwamba asitambulishwe. "Kuna hali ya kutoaminiana kutoka kwa mamlaka," aliongeza.
Baadhi ya maafisa wanatoa witu wa kubuniwa mpango wa bara la Asia kuwasaidia raia wa mataifa ya Afrika nchini China.













