Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Brexit: Uingereza yaanza safari mpya nje ya muungano wa Ulaya
Viongozi wa Ulaya wameelezea masikitiko yao baada ya Uingereza kujiondoa katika muungano wa Ulaya EU, huku rais wa Ufaransa Emmanuel Macron akisisitiza kuwa Uingereza ilikuwa "mshirika wa karibu" na Ufaransa.
Bwana Macron amesema kuwa "amesikitishwa sana" na hatua hiyo huku Guy Verhofstadt wa muungano wa EU akiahidi kuwa watafaya juhudi zote "kuhakikisha EU ni mradi ambao siku moja mtataka kujiunga nao tena".
Hatua hiyo ya kihistoria ambayo ilifanyika saa sita usiku saa za Uingereza iliadhimishwa kwa sherehe na mandamano kwa wale waliopinga hatua ya nhi hiyo kujiondoa muungano wa Ulaya maarufu kama Brexit.
Aliyekuwa waziri wa Brexit, David Davis amesema mwisho wa siku kila mtu atakuwa mshindi.
Uingereza imekuwa mwanachama wa Muungano wa Ulaya kwa miaka 47 - na hatimaye imejiondoa kutoka muungano huo baada ya miaka zaidi ya mitatu tangu ilipoamua kufanya hivyo katika kura ya maoni.
Mishumaa iliwashwa kuadhimisha siku hiyo huko Scotland, ambayo ilipiga kura ya kubaki EU, huku waliopiga kura kuondoka wakisherehekea mjini London katika bustani ya bunge.
Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson ameapa kuleta nchi pamoja na kulipeleka taifa mbele".
Katika ujumbe kwenye mtandao wa kijamii saa moja kabla ya Uingereza kujiondoa: "kwa watu wengi hii ni hatua ya matumaini, wakati ambao hawakudhania hili litawahi kufikiwa.
"Na pia kuna wale ambao wameghadhabishwa na kuingiwa na hofu kuhusu hali ya baadae"
"Na alfu kuna kundi la tatu - pengine kubwa zaidi - ambalo lilikua limeanza kuwa na wasiwasi kuhusu mgogoro wa kisiasa na kuhofia hautawahi kufika kikomo.
"Naelewa hisia zote hizo na jukumu letu kama serikali - kazi yangu - sasa ni kuleta nchi hii pamoja na kuendelea mbele."
Alisema kwamba "kutokana na uwezo wake na utendakazi wake wa kuvutia, EU imebadilika katika kipindi cha miaka 50 na kuchukua mkondo ambao hauendani na malengo ya nchi hii".
"Kitu muhimu zaidi cha kusema usiku huu ni kwamba huu sio mwisho bali ni mwanzo," alisema na kuongeza "ni wakati wa mwanzo mpya halisi wa kitaifa na mabadiliko".
Uingereza iliadhimisha vipi tukio hilo?
Sherehe za kuadhimisha Brexit zilifanyika katika kumbi tofauti za burudani huku watu wakisubiri saa iliyowekwa ya nchi hiyo kujiondoa rasmi EU.
Mamia ya watu walikusanyika katika bustani ya bunge kusherehekea Brexit, wakiimba nyimbo za kizalendo na kushangilia hutuba kutoka kwa viongozi wakuu walioshinikiza nchi kujiondoa katika muungano wa Ulaya (EU), akiwemo Nigel Farage.
Kiongozi huyo wa chama cha Brexit alisema: "Naomba tusherehekee usiku huu jinsi ambavyo hatujawahi kufanya hivyo tena.
"Hii ni hatua kubwa sana inayofanyika katika nchi yetu tukufu katika historia ya ulimwengu wa sasa."
Pia unaweza kusoma:
Awali waandamanaji wanaopinga Brexit waliandamana katika eneo la Whitehall "kuaga" muungano huo - na kufanya mkutano wa hadhara huku kesha yz kuwasha mishumaa - zikifanyika Uskochi.
Matukio mengine ya kuhistoria yaliofanyika siku hiyo yaliyoandamana na hisia mseto ilikuwa ni pamoja na:
- Bendera ya Muungano kuondolewa katika taasisi za Muungano mjini Brussels
- Mkutano wa kwanza wa mawaziri kufanyika Sunderland, mji wa kwanza kuunga mkono Brexit wakati matokeo ya kura ya mwaka 2016 yalipotangazwa.
- Makao makuu ya serikali ya Uingereza kuwashwa taa pamoja na kuondolewa kwa benderea za Muungano.
- Sarafu ya paundi 50 yaanza kutumika kuadhimisha siku hiyo.
Katoka jimbo la Ireland Kaskazini, kundi linalolijiita jamii ya mpakani inayopinga Brexit lilifanya msururu wa maandamano mjini Armagh, karibu na mpaka wa Jamhuri ya Ireland.
Ilipofika saa sita usiku sawa na 2300 GMT, Waziri kiongozi wa kwanza wa Uskochi Nicola Sturgeon aliweka kwenye twitter bendera ya EU, na kuongeza: "Uskochi itarejea Ulaya kama taifa huru. - #LeaveALightOnForScotland"
Akizungumza mjini Cardiff, Waziri kiongozi wa kwanza wa Wales, Mark Drakeford alisema Wales, ambayo ilipiga kura ya kubaki EU, itasalia "Taifa la Ulaya".
Kipi kinachoendelea kwasasa?
Raia wa Uingereza watashuhudia mabadiliko kidogo yanayoanza moja kwa moja kwasababu nchi hiyo imejiondo kwenye Muungano wa Ulaya.
Sheria nyingi za Ulaya zitaendelea kuwepo - ikiwa ni pamoja na usafiri huru wa watu - hadi Desemba 31, wakati ambapo kipindi cha mpito kitakapokuwa kinafikia ukomo wake.
Uingereza inalenga kutia saini makubaliano ya biashara huru na Umoja wa Ulaya, wenye kufanana na ule wa Muungano wa Ulaya na Canada.
Lakini viongozi wa Ulaya wameonya kwamba Uingereza inakibarua kigumu cha kufikia makubalino ndani ya siku ya ukomo iliyotengwa.
Ulaya imechukuliaje hatua hii?
Rais wa Tume ya Ulaya Ursula von der Leyen amesema Uingereza na Brussels ziapigania maslahi yao wakati wa mazungumzo ya kibiashara.
Pia alitoa shukrani kwa raia wa Uingereza waliotoa mchango wao kwa Muungano wa Ulaya na kuufanya kuwa imara zaidi na kuongeza kwamba siku ya mwisho ya Uingereza kujiondoa kwenye Muungano ilikuwa huzuni.
Nini kitakachofuata sasa?
Mhariri wa siasa wa BBC, Bi Laura Kuenssburg amekuwa akifuatilia mchakato mzima wa Brexit na huu ni uchambuzi wake:
Usiku wa kuhuzunisha haukuwa kikwazo kwa wanasherehekea katika bustani ya bunge. Tumeamka asbuh hii tukiwa hatuko tena kwenye Muungano wa ulaya. lakini bado tutafuata sheria zao hadi mwishoni mwa mwaka huu, bila kuwa na usemi wowote.
Tumeondoka katika EU baada ya miaka zaidi ya 40 lakini kumbuka tu kwamba mengi ya yaliyopo kwasasa yataendelea - Uingereza na Umoja wa Ulaya, wanadoaambao walionekana kila mmoja kuwa na mtazamo wake hatimaye wametengena - lakini badi wanaishi katika nyumba moja na kulipia gharama pamoja.
Lakini kile ambacho waziri mkuu anakisifia kama mwanzo mpya, wenye matumaini, unaanza baada ya majadiliano makali na majirani zetu.
Ombi la Uingereza: makubaliano huria ya kibiashara, ushirikiano wa usalama na mpango mpya wa uvuvi ni baadhi tu ya majadiliano muhimu yaliyoko mbele.
Vipi kuhusu Marekani?
Waziri wa mambo ya nje wa marekani Mike Pompeo amesema: "Nifuraha yangu kuona Uingereza na Marekani zimekubaliana juu ya mpango wa Brexit ambao unatilia maanani maslahi ya raia wa uingereza.
"Tutaendelea kujiimarisha na kujenga uhusiano thabiti na Uingereza wakati wanapofungua ukurasa mpya."
Balozi wa WashingtonUingereza, Woody Johnson, amesema Brexit ni mpango ambao kwa kipindi kirefu umekuwa ukiungwa mkono na Rais Donald Trump.
Uhusiano wa kipekee na Marekani na Uingereza ni jambo endelevu ambalo linaendelea kuimarika zaidi katika enzi hii mpya kwa Uingereza," amesema Johnson katika taarifa.
Uingereza imefika vipi hapa?
Uingereza ilijiunga na Muungano wa Umoja wa Ulaya 1 January, 1973, hilo lilikuwa jaribio la 3. Miaka miwili baadae nchi hiyo ilipiga kura na baada ya kupata ushindi mkubwa wa ndio ikasalia kwenye muungano huo katika kura ya kwanza ya maoni nchini humo.
Waziri Mkuu wa chama cha Conservative David Cameron alifanya kura nyengine ya maono Juni 2016, wakati kukiwa na shinikizo la juu kutoka kwa wabunge wa chama chake pamoja na Nigel Farage wa chama cha UK Independence Party.
Bwana Cameron aliongoza kampeni ya kusalia Muungano wa Ulaya lakini akashindwa kwa kura chache za asilimia 52 dhidi ya asilimia 48 na waliokuwa wanaunga mkono kuondoka EU, suala ambalo lilianzishwa na mbunge mwenzake wa Conservative Boris Johnson.
Mrithi wake kama waziri mkuu, Theresa May, alishindwa kufikia makubaliano ya kuondoka EU mara kadhaa baada ya kura kupigwa bungeni na wadhifa wake ukachukuliwa na Bwana Johnson, ambaye pia mpango wake haukufaulu.
Bwana Johnson alifanikiwa kuitisha uchaguzi wa mapema Desemba mwaka jana, na kushinda baada ya kupata wingi wa viti 80 kwa ahadi yake ya kuhakikisha kwamba Uingereza inajiondoa EU.
Mpango wa waziri huyo mkuu wa kujiondoa Muungano wa Ulaya ulipitishwa na wabunge kabla ya Krismasi na mswada huo ukawa sheria mapema mwaka huu.