Mtoto wa miaka 9 atatunukiwa shahada ya uhandisi wa umeme

Chanzo cha picha, EVN
Alikuwa na umri wa miaka minne alipoanza shule ya msingi, lakini hata kabla ya wanafunzi wenzake kuanza sekondari, Laurent Simons anahitimu shahada ya chuo kikuu akiwa na umri wa miaka tisa.
Laurent Simons kutoka Ubelgiji alitumia muda wa mwaka mmoja kumaliza darasa la kwanza katika shule ya msingi, kama wanafunzi wengine.
Baada ya hapo kasi yake iliongezeka na katika mwaka uliofuatia alimaliza miaka 2 hadi 6. Akiwa na umri wa miaka 6, alianza elimu ya sekondari na kufanya kila kitu ndani ya miezi 18 wakati kwa kawaida elimu ya msingi huchukua miaka sita kumaliza.
Baada ya hapo alipumzika kidogo. Akiwa na umri wa miaka nane, alichukua likizo ya kunoa ubongo (sabato) kwa muda wa miezi sita akichukua mapumziko hayo akiwa nyumbani. Miezi minane iliyopita, alijiandikisha katika mahafali ya chuo kikuu.
Uhandisi, Udaktari au vyote?
Laurent anapendelea jinsi gani teknolojia inaweza saidia mwili wa binadamu, utafiti wake wa mahafali ya chuo unahusu kikadi cha eletroniki kilichounganishwa kwenye ubongo.
Kikadi hiki kinapima na kufuatilia maelfu ya neva kwa wakati mmoja.

Chanzo cha picha, Laurent Simons
Baada ya miezi tisa ya kusoma, atapokea shahada ya uhandisi wa umeme mwezi Disemba, Lakini hana uhakika jinsi gani ameweza kufanya vitu vyote hivi.
Kipindi cha BBC Newsday kilipomuuliza inakuaje anatunukiwa shahada akiwa na umri wa miaka tisa, Laurent alijibu na kusema '' Hata mimi sijui.''

Chanzo cha picha, Laurent Simons
Anatokea katika familia ya madaktari na sasa anataka kusomea udaktari na kufanya shahada ya uzamivu. Lakini malengo yake yamepita sifa za kitaaluma.
''Lengo kubwa ni kutengeneza viungo bandia'' amesema mtoto huyo wa miaka 9. Viungo bandia ni viungo vinavyotetengenezwa na mwanadamu ambavyo siku moja vinaweza kutumika kama mbadala wa viungo halisi, kama vile moyo na figo na kuondoa mfumo wa kuchangia viungo.
Unaweza pia kusoma
Laurent amesema ''Lengo kubwa ni kuongeza urefu wa maisha''.
Lengo lake kwa viungo vya bandia ni kurefusha umri wa mwanadamu na kuboresha maisha.

Chanzo cha picha, EVN
''Ninataka kurefusha maisha ya watu wengine, wakiwemo babu na bibi yangu,'' anasema.
Ni Babu na Bibi yake ndio wa kwanza kugundua kipaji chake kabla ya kwenda shuleni.
''Alilelewa na wazee hao na wakagundua kuna jambo ndani yake kisha wakaanza kuzungumzia.Tulifikiri kama ilivyo kwa wazee wengine wanapojivunia mjukuu wao, na hatukuchukulia kwa umuhimu sana,'' anakumbuka Alexander Simons, baba yake.
Lakini waalimu wake wa shule ya msingi waliwaambia jambo hilo hilo, wazazi wakaanza kufuatilia namna mtoto wao alivyo na maendeleo mazuri, hata wataalamu walishangazwa na maendeleo yake

Chanzo cha picha, Laurent Simons
Mbali na kuwa ana kumbukumbu na IQ, kijana huyu mdogo pia ana uwezo katika kuchambua mambo. Tangu mwanzo alikuwa akipenda hesabu na sayansi lakini hakuonyesha mapenzi na masomo ya lugha.
Baba yake anasema alionyesha kukataa kwenda shuleni kwa siku kadhaa na akitaka kwenda ufukweni kucheza. Lakini alibadili mwelekeo baada ya kwenda Chuo Kikuu.
Na namna anavyowajibika ni ya kustaajabisha.
''Siku ya Jumatatu, anapata utambulisho wa somo, Jumanne anakuwa kwenye maabara na Jumatano huwa ni siku ya kujisomea. Hukaa nyumbani na kusoma kwa saa nane. huitumia siku ya Alhamisi kukutana na wakuu wa idara na kuwauliza maswali, Siku ya Ijumaa hufanya mitihani,'' Baba yake ameeleza.
''Wanafunzi wengine huwachukua majuma manane mpaka 12 kumaliza mzunguko huu.''
Utoto
Kuhakikisha kuwa Laurent anafurahia na anasoma kwa njia zake mwenyewe, mara nyingi hufundishwa katika chumba mbali na wanafunzi wengine, ambao maisha yao ya utoto walishayapita.

Chanzo cha picha, Laurent Simons
Lakini Baba yake anasema hajapoteza furaha yake ya utoto na hashinikizwi kufanya vitu asivyo vifurahia.
Tayari ni maarufu. Ukurasa wake wa instagram una zaidi ya watu 35,000.
Ameweka picha zake akiwa anatembea na mbwa wake, akiogelea na kufanya mahojiano na vyombo vya habari.
''Huwa anajitapa kwa marafiki zake anapoonekana kwenye runinga,'' anasema baba yake.













