Wafanyakazi wa serikali waanza kukumbatia mtindo mpya wa mavazi Kenya - je wana lengo gani?

Pauline Mburu na Margaret Njoki ni miongoni mwa wafanyakazi wa serikali waliovalia nguo zilizotengezwa nchini Kenya

Wafanyakazi wa serikali nchini Kenya wameanza kuvaa nguo rasmi zilizoundwa nchini Kenya kufuatia agizo la serikali la tarehe 17 mwezi Oktoba 2019.

Agizo hilo litakuwa likitekelezwa katika siku ya Ijumaa na siku kuu za kitaifa ikiwa miongoni mwa ajenda nne za rais Uhuru Kenyatta kuhusu utengenezaji na uvaaji wa nguo zilizotengezwa nchini.

Pauline Mburu na Margaret Njoki wakiendelea na kazi zao za kila siku

Na hii leo wafanyakazi kadhaa wa serikali walionekana katika afisi zao wakiwa wamevalia nguo hizo huku wakiendelea na kazi zao kama kawaida.

Hatahivyo baadhi ya Wakenya waliohojiwa wameomba nguo hizo zinazoundwa nchini kuuzwa kwa bei watakazoweza kumudu.

'' Ni vyema kununua nguo zilizotengezwa humu nchini lakini iwapo ziko bei ya juu haina haja ya kujilazimisha kuzinunua ilhali kuna nguo ambazo zinauzwa bei ya chini''.

Wengine wamesema kwamba ni hatua muhimu itakayoweza kuongeza ajira miongoni mwa Wakenya.

Kutoka kushoto nlkwenda kulia ni Dkt. D Opworo, Dkt, Kinyua na Dkt, Mbaluku wa kituo cha utafiti wa kilimo

Agizo hilo lilitolewa katika barua iliotoka katika ofisi ya Mwansheria mkuu iliosema kwamba hatua hiyo ni miongoni mwa harakati za kuafikia ajenda nne na hususan kupanuka kwa soko la bidhaa zilizoundwa nchini kupitia uzalishaji bidhaa bora zaidi na kubuni ajira.

Hata ijapokuwa haijulikani iwapo vazi hilo litashinikizwa kuvaliwa katika kila idara ya serikali, maafisa wakuu wa serikali pamoja na wizara zote zinadaiwa kupokea agizo hilo.

Kulingana na gazeti la Daily Nation nchini Kenya, hili lilikuwa wazi katika siku kuu ya mashujaa siku ya Jumapili iliofanyika mjini Mombasa, ambapo suti za kawaida zinazovaliwa na maafisa wakuu ziliwekwa kando na maafisa hao kuonekana kuvalia nguo zenye mitindo ya Kiafrika.

Rais Uhuru Kenyatta na makamu wake William Ruto pamoja na mawaziri walivalia nguo zilizoundwa nchini Kenya katika kile kilichotarajiwa kuwa mfano kwa Wakenya kukumbatia agizo hilo.

Mfanyakazi wa serikali Betty C Ngeno akiwa amevalia vazi aina la kitenge

Hii sio mara ya kwanza kwa serikali kushinikiza kuvaliwa kwa nguo zilizoundwa nchini ili kupiga jeki masoko ya humu nchini.

Wakati wa uzinduzi wa kiwanda cha kisasa cha Rivatex mwaka huu, rais Uhuru kenyatta alitoa wito kwa Wakenya kuvalia nguo zilizoundwa humu nchini.

Aliwataka maafisa wa serikali pamoja na Wakenya kukumbatia vitambaa kadhaa vya Kiafrika na mitindo kila wanapokuwa Afrika ama hata ughaibuni.