Iwapo Rais Kagame na Nkurunziza watakutana DR Congo - Ni yapi matarajio ya wengi?

Chanzo cha picha, Ikulu ya Rais wa Rwanda
Rais wa Rwanda Paul Kagame na mwenzake wa Burundi wanakutana kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka minne wakati wa ufunguzi rasmi wa mabaara ya utamaduni mjini Bukavu.
Wawili hao wataandamana na rais wa DR Congo Felix Tshisekedi na aliyekuwa rais wa taifa hilo Joseph kabila katika ufunguzi huo.
Hatahivyo mara ya mwisho kwa wawili hao kukutana ilikuwa mwezi Aprili 2015 katika eneo la Butare kusini mwa Rwanda, ambapo mwezi moja baadaye jaribio la mapinduzi dhidi ya rais Pierre Nkurunziza lilimkasirisha rais huyo aliyedai kwamba huenda Rwanda ilihusika.
Madai hayo yaliathiri uhusiano kati ya mataifa hayo kibiashara na kiuchumi baada ya mataifa hayo kufunga mipaka yao.
Raia wa Rwanda na wenzao wa Burundi hawakuweza tena kushirikiana kibiashara mpakani kama ilivyokuwa hapo awali hatua ambayo iliathiri uchumi wa maelfu wa raia hao kutoka pande zote mbili.
Mwaka 2018 rais wa Burundi Pierre Nkurunziza aliandika barua kwa rais wa Uganda Yoweri Museveni akiitaja Rwanda kuwa 'adui badala ya kuwa mshirika wake'.
Septemba mwaka 2019 wake wa marais wa mataifa yote mawili walikutana pembezoni mwa kongamano la Umoja wa mataifa mjini New York.
Hatua hiyo ilizua hisia kali miongoni mwa raia wa mataifa hayo mawili ambao walitoa wito kwa wake hao wa kwanza kuingilia kati na kumaliza uhusiano uliopo kati ya waume zao { Kagame na Nkurunziza}.
Na hii leo kamati za maswala ya kiusalama kutoka mataifa ya DR Congo, Rwanda na Burundi zinakutana ili kuangazia swala la usalama miongoni mwa mataifa hayo matatu.
Ni katika mkutano huo ambapo mengi yanatarajiwa kutoka kwa viongozi wa mataifa hayo mawili hatua ambayo huenda ikajenga ama kuharibu kabisa uhusiano kati ya mataifa hayo mawili.
Iwapo wawili hao watakubaliana na kuondoa uhasama wataimarisha uhusiano uliopo kati ya raia wa mataifa hayo mawili kupiga jeki uchumi wa mpakani mbali na kuimarisha usalama kati yao dhidi ya makundi ya waasi kutoka pande zote mbili.
Rwanda na Burundi zimekuwa na uhasama kwa muda sasa, Burundi ikiituhumu Rwanda kwa kuhusika katika jaribio la kupindua serikali mwaka 2015 ambalo lilifeli.
Je Burundi inasemaje kuhusu Rwanda
Burundi hudai kwamba Rwanda iliwafadhili waliohusika na kwamba inatoa hifadhi kwao. Rwanda mara kwa mara imekuwa ikikanusha tuhuma hizo.
Mwaka uliopita Rais Nkurunziza alimwandikia barua rais wa Uganda akiwa mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika mashariki mwaka huo akisema ' Rwanda sasa si mshirika tena ndani ya jumuiya bali ni kama adui'.
"Rwanda ndiyo nchi pekee katika kanda hii ambayo ndiyo moja wa wahusika wakuu katika kuvuruga uthabiti wa taifa langu na kwa hivyo siichukulii kama taifa mshirika, lakini kama adui ya nchi yangu," alinukuliwa akisema katika barua hiyo, ambayo iilitiwa saini na Bw Nkurunziza mnamo tarehe 4 Desemba.
Kiongozi huyo aliitisha kikao maalum cha EAC kufanyika ili kujadili mzozo huo kati ya Rwanda na Burundi.
Burundi inasisitiza kwamba Rwanda ndiyo chanzo kikuu cha machafuko yaliyotokea Burundi tangu Aprili 2015, na kwamba mzozo huo ulianza mapema mwaka 2010 wakati baadhi ya makundi ya upinzani yalipoanza kusema kwamba hakungekuwa na uchaguzi 2015.
Burundi inadai kwamba Rwanda imekuwa ikihusika katika visa vya utovu wa amani nchi mwake, ikishirikiana na mkoloni wa zamani Ubelgiji.
"Rwanda ilikataa kushirikiana na kundi la pamoja la kutathmini hali halisi lakini Burundi ilishirikiana kikamilifu, na huu ni ushahidi tosha kwamba taifa hilo halijawahi kutaka ukweli ufahamike kwa sababu ya uchokozi wake dhidi ya Burundi.
"Ni wazi kwamba Jumuiya ya Afrika Mashariki haifai kufumbia macho mateso haya yanayowakuta wana wa Burundi."
Vilevile Burundi imesema kamwe haitakubali pendekezo la jumuiya ya kimataifa la kuruhusu vikosi kutoka nje kudumisha amani Burundi na kutolewa kwa msamaha kwa wanaodaiwa kuhusika katika jaribio la mapinduzi ya serikali ya mwaka 2015 kama masharti kabla ya kufanyika kwa uchaguzi wa mwaka 2020.
Barua hiyo inasema kukubaliwa kwa mapendekezo hayo kutakuwa ni ukiukaji wa sheria za Burundi.
"Wahusika katika mapinduzi ya serikali kote huwajibishwa na kushtakiwa katika mahakama na majopo ya mahakama, kwa nini basi hawa wa Burundi iwe tofauti kwao?," barua hiyo inasema.
"Nasikitika, Mheshimiwa Rais (Bw Museveni) kukufahamisha kwamba kamwe sitaketi meza moja na wahusika wa mapinduzi…ninapendekeza kuandaliwa kwa kikao maalum cha viongozi wa mataifa ambacho ajenda yake itakuwa kutatua suala la mzozo wa wazi kati ya Burundi na Rwanda," alisema Bw Nkurunziza kwenye barua hiyo.
Nkurunziza kupigania muhula wa tatu

Burundi imekumbwa na mzozo wa kisiasa tangu Aprili 2015 wakati Bw Nkurunziza alipotangaza kwamba angewania urais kwa muhula wa tatu.
Mnamo 30 Novemba, Rais Magufuli, Rais Museveni na Rais Kenyatta walipokuwa wamekwenda kwa Mkutano wa 20 wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC), hawakuweza kuendelea na kikao.
Rais Museveni ambaye ni Mwenyekiti alisema mkutano huo uliahirishwa hadi tarehe 27 Desemba, 2018 kutokana na mmoja wa wanachama wa jumuiya hiyo ambaye ni nchi ya Burundi kutohudhuria, ilihali mkataba wa jumuiya hiyo unataka maamuzi yafanywe na wanachama wote kwa pamoja.
"Tuliamua kuahirisha mkutano kwa leo kwa sababu mmoja wetu ambaye ni Burundi hakuja, tumeahirisha mkutano mpaka tarehe 27 Desemba, 2018 wakati sisi wote tutakapokuwepo, kwa sababu mkataba wa Afrika Mashariki unasema mambo mawili, moja lazima tuwe na mkutano mmoja wa kawaida kila mwaka na ndio huu wa leo.
"Lakini vile vile uamuzi wowote utakaofanyika lazima wanachama wote wawepo, kwa hiyo kama mmoja hayupo sio vizuri kuendelea, inakuwa inakwenda kinyume na mkataba" alisema Rais Museveni.
Serikali ya Rwanda inasemaje?

Chanzo cha picha, Reuters
Rais wa Rwanda Paul Kagame amekana madai yaliotolewa na Umoja wa Mataifa kwamba taifa lake linaendelea kuwasaidia waasi katika nchi jirani ya Burundi.
Bw Kagame amesema kuwa tatizo la Burundi linatoka ndani ya nchi hiyo, na sio nje.
Mnamo mwezi machi 2019 serikali ya Rwanda iliwasihi wananchi wake wanaoshi karibu na karibu na mpaka kati ya nchi hiyo na nchi ya Burundi kusitisha biashara yoyote na majirani zao wa nchi ya Burundi, siku chache baada ya Rwanda kuwakataza wananchi wake kwenda nchini Uganda.
Rwanda inashutumu nchi hizo kusaidia makundi ya waasi yanayoipinga.












