Ifahamu faida ya mama kujifungua mtoto kwa mara nyingine kupitia upasuaji

Chanzo cha picha, Getty Images
Kupanga kujifungua kwa njia ya upasuaji huenda ndio njia salama kwa wanawake ambao waliwahi katika kipindi cha nyuma kujifungua watoto kupitia njia hiyo, kwa mujibu wa utafiti mpya katika PLoS Medicine.
Kujaribu kujifungua kwa njia ya kawaida baada ya kujifungua kwa upasuaji kumehusishwa na ongezeko la hatari ya kuzuka matatizo kwa mama na mwana ikilinganishwa na iwapo mama huyo angeamua kujifungua kwa upasuaji tena.
Utafiti huo umetokana na visa 74,000 vya akina mama waliojifungua huko Usktochi.
Wataalamu wanasema akina mama wanapaswa kupewa fursa ya kuchagua kati ya kujifungua kwa njia ya kawaida na kupitia upasuaji na wapaswa kuarifiwa kuhusu hatari ya mbinu zote mbili.
Nini maana ya kujifungua kupitia upasuaji?
Caesarean section kama inavyofahamika ni wakati mtoto anazaliwa kwa kulipasua tumbo la mama kuingia ndani ya kizazi chake.
Upasuaji huo unaweza kuwa:
- Wa hiari au uliopangwa - kutokana na ombi la mama au kwasababu za kimatibabu, kama mfano mtoto amekaa vibaya tumboni au ni mkubwa sana.
- Wa dharura - kawaida kutokana na matatizo wakati mama akiwa kwenye uchungu wa kujifungua.
Ni njia ipi ilio salama zaid ?
Kuzaa au kujifungua kuna hatari zake na haijalishi ni kupitia njia gani.
Utafiti uliofanywa nchini Uskotchi umelinganisha hatari za upasuaji wa kupangwa au hiari dhidi ya kujifungua kupitia njia ya kawaida ya kumsukuma mtoto (miongoni mwa wanawake waliojifungua kupitia upasuaji awali) na umegundua:
- Wanawake 45,579 walizaa kupitia upasuaji wa hiari na 28,464 walijaribu kujifungua kupitia njia ya kawaida
- 28.4% ya waliojaribu kuzaa kwa njia ya kawaida waliishia kufanyiwa upasuaji wa dharura
- Kujifungua kwa njia ya kawaida kumehusishwa na hatari inayoongezeka ya mama kuwa na matatizo makubwa wakati wa kujifungua na baada, ikilinganishwa na waliojifunguwa kupitia upasuaji.
- 1.8% ya wanaojaribu kujifungua kwa njia ya kawaida na 0.8% ya waliopanga kujifungua kupitia upasuaji walikabiliwa na matatizo makubwa ya uzazi kama kupasuka kwa uzao, kuvuja damu au maambukizi.
- Matatizo kwa mtoto yalitokea katika 8% ya mimba za akina mama waliojaribu kujifungua kwa njia ya kawaida na 6.4% ya waliochaguwa kwa hiari upasuaji.

Chanzo cha picha, Getty Images
Kwa mujibu wa kituo cha madaktari wa afya ya uzazi wa akina mama Royal College of Obstetricians and Gynaecologists, kwa mara nyingi, wanawake wanaweza kupewa fursa ya kuchagua kati ya njia hizo mbili kwasababu hatari zilizopo ni za chini.
Kwa ujumla, baada ya upasuaji mmoja au Caesarean, kati ya wanawake watatu au wanne wanaopata uchungu wa kujifungua huishia kuzaa kwa njia ya kawaida huku mmoja kati ya wanne wanaishi kufanyiwa upasuaji wa dharura.
Faida na madhara
Uponaji baada ya upasuaji wa huchukua muda mrefu na kuna hatari ya mama kupata maambukizi na kuvuja damu kutokana na upasuaji huo.
Kidonda kinasalia kwa kila upasuaji, jambo linalohatarisha kondo la nyuma kukuwa kwenye kidonda katika mimba za siku zijazo na kuzusha matatizo.
Kuna hatari ndogo pia kwa mtoto kutokana na upasuaji ikiwa ni pamoja na matatizo ya kupumua nakukatwa kwa bahati mbaya wakati wa upasuaji.
Kujifungua ka njia salama ina maana mama anakaa hospitali kwa kipindi kifupi, anapona haraka na kurudi katika shughuli zake za kawaida haraka .
Lakini mara nyingine husihia kuraruka kwa ngozi baina ya uke na sehemu ya haja kubwa.
Kadhalika haipendekezwi kwa mama kujifungua kwa njia ya kawaida iwapo aliwahi kujifungua kwa upasuaji mara mbili au tatu awali.













