Syridio Dusabumuremyi: Kiongozi wa upinzani Rwanda FDU-Inkingi 'auawa kwa kuchomwa kisu'

Syridio Dusabumuremyi was at work when he was attacked

Chanzo cha picha, ©FDU-Inking

Maelezo ya picha, Syridio Dusabumuremyi alikuwa kazini aliposhambuliwa
Muda wa kusoma: Dakika 2

Mwanasiasa maarufu wa upinzani nchini Rwanda amedunguwa kisu na kuuawa, chama chake cha FDU-Inkingi kinasema.

Syridio Dusabumuremyi, mratibu wa chama hicho cha upinzani FDU-Inkingi, alikuwa kazini wakati aliposhambuliwa na wanaume wawili, kiongozi wa chama hicho Victoire Ingabire ameieleza BBC.

Mwanamume huyo ambaye ni baba ya watoto wawili alikuwana duka la kuuza chakula katika kituo cha afya katika wilaya ya kati ya Muhanga.

Idara ya upelelezi nchini Rwanda imetuma ujumbe katika mtandao wa twitter kueleza kwamba imewakamata washukiwa wawili wanaotuhumiwa kuhusika na mauaji ya Syridio Dusabumuremyi.

Ruka X ujumbe
Ruhusu maudhui? (Mitandao ya kijamii)

Mkala hii imebeba madhui yaliyotoka kwenye mitandao ya kijamii. Tunaomba ruhusa yako kabla kitu chochote hakija pakiwa, sababu wanaweza wakawa wanatumia Cookies na tekinolojia nyingine. Unaweza ukasoma sera sera ya kutumia cookies katika mitandao ya kijamii kabla ya kukubali. Kutazama maudhui haya chagua accept and continue

Onyo: Imetoka kwingine na inaweza kuwa na matangazo

Mwisho wa X ujumbe

Katika ujumbe huo, idara hiyo imeeleza kwamba Dusabumuremyi Sylidio alichomwa kisu hadi kufa na watu wasiojulikana, aliuawa akiwa kazini katika kituo cha afya wilayani ya Muhanga.

Kwenye ujumbe uliofuata, idara hiyo ya upelelezi imeeleza kwamba katika uchunguzi wa awali, washukiwa wawili wamekamatwa kwa kuhusika na mauaji hayo.

Imeendelea kusema uchunguzi unaendelea kubaini dhamira ya mauaji hayo.

Bi Ingabire anasema mauaji ya Dusabumuremyi ni ya hivi karibuni kufuatia msururu wa mashambulio dhidi ya wafuasi wa chama chake kwa lengo la kuwatishia.

Wapinzani wengine waliouawa

Miezi miwili iliyopita, Eugène Ndereyimana, mwakilishi wa chama cha FDU-Inkingi kutoka eneo la mashariki mwa Rwanda alitoweka. Mpaka sasa hajapatikana.

Mnamo Machi, Anselme Mutuyimana, msemaji wa chama hicho alitekwa na baadaye kukutikana amefariki msituni magharibi mwa nchi hiyo.

Mnamo 2016, mwanachama wa FDU-Inkingi Jean Damascène Habarugira aliuawa.

Bi Ingabire, ambaye ni mkosoaji mkubwa wa rais Paul Kagame, amesema chama chake kinalengwa kwasababu kinapania kutetea haki za raia wa Rwanda na uhuru wao.

"Lengo letu ni zuri na hatutaacha kulipigania hata wakafanya lolote," amesema.

Victoire Ingabire
Maelezo ya picha, Kiongozi wa upinzani Rwanda Victoire Ingabire amesema chama chake kinalengwa kwasababu kinapania kutetea haki za raia wa Rwanda na uhuru wao

Victoire Ingabire ni nani?

Victoire Ingabire Umuhoza alizaliwa oktoba tarehe tatu mwaka 1968.

Ni mke na mama wa watoto wa tatu.

Amesomea Sheria na masuala ya uhasibu na hatimaye kufuzu kwa shahada ya uchumi na biashara nchini Uholanzi.

Tangu mwaka 1997, Ingabire amejihusisha na harakati za upinzani nchini Rwanda akiwa mafichoni Uholanzi.

Aliteuliwa na muungano wa kundi la viongozi wa upinzani ambao una wanachama nchini Rwanda, barani Ulaya, Marekani na Canada.

Mnamo mwezi Januari mwaka 2010 Bi Ingabire alirejea Rwanda kutoka mafichoni nchini Uholanzi baada ya kutajwa kuhusika kwenye mauaji ya kimbari ya mwaka 1994, ili kugombea uchaguzi wa urais.

Alikamatwa na kuzuiliwa kuwania urais.

Bi Ingabire, ni mwanachama wa jamii ya Wahutu na alihoji kwa nini makumbusho rasmi ya mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 nchini Rwanda hayakujumuisha Mhutu yeyote

Bi Ingabire alikamatwa na hatimae kufungwa jela mwaka 15 kwa makosa ya ugaidi pamoja na kuhatarisha usalama wa kitaifa.

Hata hivyo sasa yuko huru baada ya kupewa msamaha na Rais Kagame.