Grace Mugabe: Mfahamu mke wa aliyekuwa rais wa Zimbabwe Robert Mugabe

Grace Mugabe

Chanzo cha picha, Grace Mugabe/facebook

Aliyekuwa mke wa rais wa Zimbabwe Grace Mugabe, kwa miaka kadhaa alikuwa akijiandaa kuwa mrithi wa mumewe aliyekuwa na umri wa miaka 93 kabla ya kifo chake hivi majuzi akiwa na umri wa miaka 95.

Alikuwa mwanamke aliyenyamaza akijulikana tu kwa ununuzi wake wa vitu vya bei ghali na kazi zake za kusaidia wasiojiweza kabla ya kupanda hadhi na kuwa mtu maarufu katika chama tawala cha Zanu-PF kama kiongozi wa wanawake.

Alihusika pakubwa katika kuwakabili na kuwatimua wanachama wa chama hicho waliopigiwa upatu kumrithi mumewe.

Hatahivyo alishindwa kumkabili aliyekuwa makamu wa rais wa taifa hilo Emmerson Mnangagwa.

Bi Mugabe alimshutumu kwa kutomtii na kumfuta kazi 2017 , lakini msururu wa matukio baada ya hatua yao ilisababisha kuondolewa kwao madarakani.

Maafisa wa jeshi walikiteka chombo cha habari cha taifa na kumweka Mugabe katika kifungo cha nyumbani.

Bwana Mnangagwa alichaguliwa kiongozi wa Zanu- Pf mnamo tarehe 19 Novemba.

Grace Mugabe wakati akitoa hotuba yake mbele ya umati

Chanzo cha picha, AFP

Akiwa na umri wa miaka 52 , bwana Mugabe alikuwa amempita bi Mugabe kwa miongo minne wakati kiongozi huyo mkongwe ambaye aliitawala Zimbabwe baada ya kipindi cha ukoloni mwaka 1980 hadi alipojiuzulu Novemba 2017.

Bi Mugabe amekuwa shabiki mkubwa wa mumewe huku mapema 2017 akinukuliwa akisema kwamba mumewe anaweza kushinda kura hata akiwa maiti.

Hajakataa kutaka kumrithi mumewe na katika mkutano wa kisiasa 2014 alisema kwamba 'nataka kuwa rais, kwa nini nisiwe, kwani mimi sio Mzimbabwe?'

line

Kutoka kuwa mpiga chapa hadi kuwa mke wa rais

Grace na Robert Mugabe pamoja

Chanzo cha picha, AFP/ Getty Images

  • Alianza uhusiano na Robert Mugabe, ambaye alikuwa na miaka 41 zaidi yake akifanya kazi kama mpiga chapa katika Ikulu ya rais nchini Zimbabwe
  • Bwana Mugabe alikuwa bado amemuoa mkewe wa kwanza Sally ambaye alikua mgonjwa kupitia kiasi.
  • Alifunga ndoa na Mugabe, mumewe wa pili mwaka 1996 katika sherehe ya hali ya juu.
  • Wana watoto watatu - Bona, Robert na Chatunga
  • Ana jina la utani "Gucci Grace" ambalo alipewa na wakosoaji wake ambao walimshutumu kwa ununuzi wa vitu ghali.
  • Alichaguliwa mkuu wa wanawake katika chama tawala cha Zanu PF 2014, na alitarajiwa kuteuliwa kuwa makamu wa rais mwezi Disemba.
  • Alishutumiwa kwa kumpiga mwanamitindo mmoja nchini Afrika Kusini 2017.
line

Wapinzani wa kisiasa walikuwa wameonya kwamba kulikuwa na mpango wa familia kupokezana uongozi wa taifa hilo na bi Mugabe alikosolewa kwa kutaka kutumia kinga yake ya kidiplomasia wakati alipo tuhumiwa kwa kumpiga mwanamitindo mwernye umri wa miaka 20.

Hii haikuwa mara ya kwanza kushutumiwa kwa kuwashambulia watu.

Pamoja na mumewe Bi Mugabe amewekewa vikwazo na EU pamoja na US , ikiwemo vile vya kusafiri kufuatia hatua ya kunyakuwa ardhi mbali na tuhuma za kufanya udanganyifu katika uchaguzi na usakaji wa wapinzani wa kisiasa.

Jinsi bi Grace Mugabe alivyopanda hadhi.

Aliyekuwa rais wa Zimbabwe marehemu Robert Mugabe alianza uhusiano wake na Bi Grace Marufu wakati alipokuwa akifanya kazi kama mpiga chapa katika Ikulu ya Zimbabwe.

Wawili hao walianza uhusiano huo wa kimapenzi wakati Mugabe alipokuwa ameoana na mkewe wa kwanza. Wakati huo mke wa kwanza wa Mugabe alikuwa mgonjwa kupitia kiasi.

''Alikuja kwangu na kuniuliza kuhusu familia yangu'', alisema katika mahojiano kuhusu mkutano wao wa kwanza 1980.

''Nilimchukulia kama babangu . Sikufikiria kwamba ataniangalia na kuniambia : Nampenda huyu msichana . sikutarajia''.

Aliyekuwa Mke wa rais wa Zimbabwe Grace Mugabe - tarehe 2 Disemba

Chanzo cha picha, Reuters

Bwana Mugabe anasema kwamba Sally alimruhusu kufunga ndoa kabla ya kifo chake 1992 - ijapokuwa hakumuoa Grace hadi miaka minne baadaye.

Wawili hao wana watoto watatu: Bona, Robert and Chatunga.

Kwa jina Gucci Grace, Grace Mugabe alishutumiwa na baadhi kwa matumizi yake ya hali ya juu wakati wa ununuzi.

Familia hiyo ina mali, biashara na mashamba katika maeneo tofauti nchini humo hususan katika maeneo ya magharibi yenye matajiri wengi pamoja na mkoa wa kaskazini wa Mashonaland.

Katika miaka kadhaa , Bi Mugabe amejaribu kujikuza kama mfanyabiashara maarufu na anajichukulia kama muhisani baada ya kuanzisha kituo cha watoto mayatima eneo moja nje ya mji mkuu wa Harare kupitia usaidizi wa ufadhili wa China.

Alipokea shahada ya uzamifu kwa njia ya utata kutoka chuo kikuu cha Zimbabwe katika kipindi cha miezi miwili pekee 2014 licha ya kwamba hoja yake haikuhifadhiwa na haijawahi kuwekwa wazi.

Licha ya hayo , hadhi yake ilitumika katika vifaa vya kumfanyia kampeni alipokuwa akijiandaa kuchukua uongozi wa chama cha Zanu PF wingi ya wanawake.

Tangu alipoanza kushiriki katika siasa , alijulikana kwa ulimi wake mkali na sifa yake ya kishupavu.

Wakati alipokuwa akiwashambulia wapinzani wake bi Mugabe alikuwa akimtetea mumewe kwa hali na mali.

Ameshutumiwa kwa kuweka wazi uchafu wa chama cha Zanu PF kwa kuwataka wanachama kujiuzulu ama hata kuomba msamaha.

Grace dhidi ya manaibu wa mumewe

Bi Mugabe aliongoza kuondolewa mamlakani kwa aliyekuwa makamu wa rais bi Joice Mujuru, 2014.

Alisema kwamba makamu huyo wa rais anafaa kufutwa kazi kwa kuwa alikuwa fisadi ,mnyang'anyi , asiyeweza kujimudu, m'beya , muongo na mtu asiye na shukrani huku akimshutumu kwa kushirikiana na wapinzani na watu weupe kukandamiza faida iliopatikana baada ya uhuru.

Joice Mujuru 2004

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Joice Mujuru alikuwa mshirika mkuu wa bwana Mugabe

Miezi michache baadaye , bi Mujuru alifukuzwa katika chama cha Zanu PF , na bado ni kiongozi wa chama cha upinzani cha National Peoples Party na anaogoza muungano wa vyama ambapo amewasihi raia kujisajili kupiga.

Makamu mpya wa rais alikuwa bwana Mnangagwa , waziri wa zamani wa haki ambaye bi Mugabe alimtaja kuwa mtiifu na mwenye nidhamu.

Lakini kufikia 2017, bi Mugabe alikuwa akimtaka mumewe kumuondoa bwana Mnangangwa .

Alipopendekeza kwamba wafuasi wake walikuwa wanapanga kufanya mapinduzi.

Wakati alipokuwa mgonjwa katika mkutano wa hadhara na akasafirishwa nje ya taifa kwa matibabu , wafuasi wake walilalamika kwamba alikuwa amewekewa sumu katika ice cream kutoka kampuni ya maziwa ya bi Mugabe, madai ambayo alikana.

Baadaye alisema kwamba alikuwa amepewa sumu , lakini ilikuwa uongo kupendekeza kwamba sumu hiyo ilitoka kwa mke wa rais.