Double Dave: Nyoka mwenye vichwa viwili apatikana Marekani

Double Dave nyoka mwenye vichwa viwili

Chanzo cha picha, David Schneider, Herpetological Associates

Maelezo ya picha, Nyoka huyo alipatikana katika msitu mmoja uliopo katika jimbo la New Jersey

Nyoka asiye wa kawaida mweye vichwa viwili amepatikana katika msitu mmoja katika jimbo la New Jersy nchini Marekani.

Mnyama huyo aliyepewa jina la Double Dave alionekana mwezi ulioipita na kuchukuliwa na kundi moja la mazingira.

Akiwa na vichwa vilivyounganishwa na mwili wake , nyoka huyo mdogo mwenye sumu kali ana vichwa viwili vilivyokamilika, macho manne na limi mbili ambazo zilikuwa zikifanya kazi tofauti.

''Itakuwa vigumu kwa nyoka huyo kuishi msituni'', alisema mwanamazingira Dave Schneider.

Anasema kwamba nyoka huyo hujibadilisha na kujikamua anapotaka kutoroka hivyobasi itakuwa rahisi kwa wanyama wengine kumkamata.

Bwana Schneider kutoka Muungano wa wataalam wa wanyama wanaotambaa anayesomea wanyama hao walio katika tishio la kuangamia amesema kwamba yeye na mwenzake walimuona Double Dave mnamo tarehe 25 mwezi Agosti katika msitu.

Tukio hili lilijiri wakati walipokuwa wakimtazama nyoka mwengine aliyekuwa akijifungua.

Nyoka wenye vichwa viwili huzaliwa sawa na pacha ambapo kiini tete kinachokuwa hujigawanya mara mbili na kutoa pacha wanaofanana kabla ya kusita kujigawanya kwa ghafla.

Walimpatia jina Double Dave kwa sababu bwana Schneider na mwenzake wote wanaitwa David.

Bwana Schneider aliambia BBC kibali maalum kimepatikana kutoka kwa mamlaka ya wanyama wanaotambaa kumhifadhi na kumfanyia utafiti nyoka huyo asiye wa kawaida.