'Hakuna vinasaba vya mapenzi ya jinsia moja'

Rainbow flag at a gay pride parade

Chanzo cha picha, Getty Images

Utafiti wa vinasaba wa watu laki tano umefikia hitimisho kuwa, hakuna hata "kinasaba kimoja cha mapenzi ya jinsia moja".

Utafiti huo, uliochapishwa kwenye jarida la Science, umetumia data kutoka Uingereza kupitia mitandao ya Biobank na 23andMe, na kugundua utofauti wa vinasaba unaohusishwa na mahusiano ya wapenzi wa jinsia moja.

Hata hivyo, muundo wa jeni, kwa wastani wa 25% unachangia mahusiano ya mapenzi ya jinsia moja.

Kundi la wanaharakati wa mapenzi ya jinsia moja GLAAD limesema utafiti huo umethibitisha kwa: "hakuna hitimisho la moja kwa moja juu ya ushawishi wa maumbile ama malezi katika tabia za wapenzi wa jinsia moja."

Watafiti waliziangazia kwa ujumla wake mfumo mzima wa muundo wa vinasaba, kwa lugha ya kitaalamu genome - za watu 409,000 waliowafanyia utafiti.

Walioshiriki utafiti huo pia waliulizwa kama wanajihusisha na mapenzi ya jinsia moja tu ama kama wana mahusiano na jinsia tofauti (mahusiano ya kawaida).

Watafiti wmetoka katika vyuo mashuhuri vya Marekani vya Harvard and MIT na wamehitimisha kuwa vinasaba vinachangia 8-25% ya tabia ya wapenzi wa jinsia moja, baada ya kutafiti genome yote.

'Ni vigumu kubashiri'

Profesa Ben Neale, mtaalamu wa vinasaba kutoka hospitali ya Massachusetts, ambaye alishiriki katika utafiti huo amesema: "Vinasaba ni chini ya nusu ya hadithi nzima ya tabia za mahusiano, lakini ni moja ya michango ya kitabia.

"Hakuna hata kinasaba kimoja cha mapenzi ya jinsia moja, na kipimo cha kinasaba hakitasaidia lolote kutambua kama wewe unaweza kuwa ni mpenzi wa jinsia moja.

"Ni vigumu kweli kweli kubashiri mahusiano ya kimapenzi ya mtu kwa kuangalia vinasaba vyao."

Fah Sathirapongsasuti, mwanasayansi mwandamizi kutoka 23andMe, ameongeza; "Hili ni jambo la kiasili na la kawaida kwa utofauti wa maumbile yetu, na linaenda kusisitiza kuwa hakuna haja ya kujaribu kutengeneza dawa ya kutibu wapenzi wa jinsia moja."

David Curtis, kutoka Chuo Kikuu cha London amesema: "Utafiti huu unaonesha dhahiri kuwa hakuna hicho kitu kinachoitwa 'kinasaba cha mapenzi ya jinsia moja'.

"Hata kuwa na mapenzi ya jinsia moja hayaamuliwi kijenetiki, kama utafiti unavyoonesha, japo haimaanishi kuwa kuna mapungufu ya hapa na pale ambayo yanachangia tabia binafsi ya mtu."

Zeke Stokes, mtandao wa GLAAD, amesema: "Utafiti huu unapigia mstari kile ambacho kwa muda mrefu kinajulikana kuwa hakuna hitimisho la moja kwa moja juu ya ushawishi wa maumbile ama malezi katika tabia za wapenzi wa jinsia moja."