Namibia: Mamba watano wasadikiwa kuuwawa kwa sumu

Chanzo cha picha, Getty Images
Mamba wapatao watano wamekutwa wameuwawa kaskazini magharibi mwa mpaka wa Namibia na Angola, chanzo cha vifo hivyo hakijafahamika bado ingawa inasadikiwa kuwa waliwekewa sumu.
"Inawezakana kuwa kuna baadhi ya watu ambao walidhuliwa na mamba hao kwa namna moja au nyingine. Labda Mamba hao waliwauwa wanyama wao au wapendwa wao hivyo wakaamua kuwawekea sumu ili wafe," afisa mahusiano wa wizara ya mazingira,Romeo Muyunda aeleza.
"Lakini pia inawezekana sio sumu pekee kwa sababu baadhi ya mamba wamekutwa wakiwa na majeraha , mfano kuna mamba mmoja aliokutwa amekutwa kichwa na wengine mkia.
Vivyo hivyo hatuwezi kusema sababu moja kwa moja, Je, ni binadamu au wanyama wengine ndio wamewadhuru.
Licha ya kwamba kuna baadhi ya watu ambao wanakula mamba lakini sio upande wa Namibia labda Angola," Muyunda alifafanua katika kipindi cha redio cha BBC Focus on Africa.
Mamlaka ya Namibia imeweka sera ambazo zinawalinda Mamba na kunufaisha raia wa nchi yake hivyo inawawia vigumu kuamini kuwa ni raia wa Namibia ndio wamefanya vitendo hivyo.
Wizara ya mazingira nchini Namibia imezindua mpango maalum wakishirikiana na Angola ili kubaini chanzo cha vifo vya mamba hao waliouwawa katika mto Kunene.
"Inawezekana kuwa sumu hiyo iliwekwa upande wa Angola. Tunaamini kuwa watu hao walikuwa na njama za kulipiza kisasi kama matokeo ya migogoro ya wanyama wa porini"
Matukio kama hayo huwa yanatokea wakati watu wanapokasirishwa na kupoteza kwa wanyama wao na watu kuuwawa na mamba", alinukuliwa Muyunda.

Chanzo cha picha, Getty Images
Mpaka sasa haijajulikana idadi kamili ya mamba wameuwawa na chanzo cha vifo vyao.
"Tunatoa rai kwa raia wote wa Namibia ambao wana migogoro na wanyama wa porini wasichukue sheria mikononi mwao kwa sababu kuna sheria ambazo zinapaswa kufuatwa ili kupata suluhu".
Kwa sasa, wanakijiji wa maeneo ya karibu ya mto huo wamesisitizwa kutokula nyama ya mamba, wakati uchunguzi wa kujua ni sumu gani imewauwa mamba hao.
Mmiliki wa nyumba ya wageni katika eneo hilo ni miongoni mwa watu waliotoa taarifa kuhusu tukio hilo.

Chanzo cha picha, Getty Images
Mamba ni miongoni mwa vivutio vya utalii nchini Namibia.













