Israel inasema kwamba ilishambulia maeneo ya ndege zisizo na rubani za Iran nchini Syria

Chanzo cha picha, AFP
Israel imeshambulia kambi za kijeshi za Iran nchini Syria ili kuzuia kile ilichokitaja kuwa utumizi wa ndege zisizokuwa na rubani kuishambulia.
Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alipongeza juhudi za operesheni hiyo iliotekelezwa na jeshi lake.
Israel inaaminika kutekeleza mamia ya mashambulio nchini Syria tangu vita vya wenyewe kwa wenyewe 2011 ili kujaribu kuizuia Iran.
Msemaji wa jeshi la Israel alisema kwamba mashambulio hayo siku ya Jumamosi yalilenga wapiganaji wa Kikurdi wa Iran katika eneo la Aqraba , kusini mashariki mwa mji mkuu wa Damascus.
Duru za kjeshi za Syria zilizonukuliwa na chombo cha habari cha kitaifa cha Sanaa zilisema kwamba mifumo ya ulinzi ya angani ya Syria iligundua kwamba Israel ilikuwa inajiandaa kutekeleza mashambulizi kutoka katika milima ya Golan ikielekea katika mji wa Damascus.
''Uchokozi huo ulikabiliwa na kufikia sasa idadi kubwa ya silaha za Israel zimeharibiwa kabla ya kutimiza lengo lake'', duru hizo zilisema.
Katika ujumbe wa Twitter, Bwana Netanyahu alisema: Iran haina kinga kokote. ''Jeshi letu litatekeleza operesheni zake dhidi ya uchokozi wa Iran. Iwapo mtu anapanga kukuua muue wewe kwanza''.
'Shambulio la wazi'
Kwengineko ripoti zimesema kwamba ndege zisizo na rubani za Israel ambazo zilikuwa zikifanya uchunguzi ziliwasili katika ngome ya kundi la Hezbollah katika mji mkuu wa Lebanon wa Beirut.
Maafisa wa Hezbollah wamesema kwamba ndege zisizokuwa na rubani zilianguka katika paa ya kituo kimoja cha habari kinachomilikiwa na kundi hilo na ilifuatiwa na ndege nyengine isiokuwa na rubani ambayo ililipuka angani na kuanguka karibu na kitu hicho.

Chanzo cha picha, AFP
Wakaazi waliambia chombo cha habari cha AP kwamba walisikia mlipuko mkubwa ambao uliyumbisha eneo hilo baada ya kusikia sauti ya ndege
Jeshi la Israel lilikana kuzungumzia kuhusu ripoti hizo.
Waziri mkuu wa Lebanon Saad Hariri alitaja hatua hiyo ya Israel kama shambulio la wazi dhidi ya taifa huru la Lebanon.
''Uchokozi huu mpya ndio unaozua hofu ya usalama wa eneo hili lote na jaribio la kuzua hofu zaidi'' , alisema katika taarifa.
Israel pia ilidaiwa kutekeleza shambulio la angani mwezi uliopita katika hifadhi moja ya silaha nchini Iraq.
Gazeti la New York Times , lilinukuu maafisa wa Marekani ambao hawakutaka kujulikana wakisema kwamba ndio iliotekeleza shambulio la Julai 19 katika hifadhi ya silaha ambayo maafisa walikuwa wakisema kwamba inatumiwa na Iran kupeleka silaha Syria.
Jeshi la Israel limekataa kutoa tamko kuhusu shambulio hilo.
Lakini ni kwa nini Israel na Iran ni maadui
Tangu kufanyika kwa Mapinduzi ya Iran ya mwaka 1979, ambapo viongozi wa kidini wenye msimamo mkali walichukua mamlaka na kumaliza utawala wa Shah, Iran imekuwa ikiitisha kuangamizwa kwa Israel.
Iran husema taifa la Israel halina haki zozote za kuwepo, kwa sababu liliundwa kwenye ardhi ambayo ilitekwa kutoka kwa Waislamu.

Israel hutazama Iran kama tishio kuu dhidi ya kuwepo kwake. Taifa hilo la Kiyahudi limekuwa likisisitiza kwamba Iran haifai kuruhusiwa kuwa na silaha zozote za kinyuklia.
Viongozi wao wana wasiwasi sana kuhusu kuenea kwa ushawishi wa Iran katika Mashariki ya Kati.
Syria inaingiaje katika mzozo huu?
Israel imekuwa ikifuatilia matukio katika taifa jirani la Syria kwa wasiwasi tangu vita vilipozuka mwaka 2011.
Israel imekuwa haishiriki katika vita hivyo kati ya serikali ya Bashar al-Assad na waasi.

Chanzo cha picha, AFP
Lakini Iran imeshiriki sana katika vita hivyo ambapo imetuma maelfu ya wapiganaji na washauri wa kijeshi kusaidia wanajeshi wa Bw Assad.
Israel ina wasiwasi pia kwamba Israel inajaribu kuwatuma wapiganaji na silaha kisiri nchini Lebanon - jirani mwingine wa Israel - ambayo pia huitishia Israel.
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu mara kwa mara amesisitiza kwamba taifa lake halitairuhusu Iran ijenge kambi Syria ambazo zinaweza kutumiwa dhidi ya Israel.
Kwa hivyo, kadiri Iran ilivyoendelea kujiimarisha nchini Syria ndivyo Israel ilivyodhidisha mashambulio dhidi ya kambi na wanajeshi wa Iran huko.
Iran na Israel zishawahi kupigana?
Hapa. Iran kwa muda mrefu imekuwa ikiunga mkono makundi yanayoishambulia Israel - kwa mfano Hezbollah wa Lebanon na kundi la Hamas la Palestina.
Lakini mataifa hayo mawili hayajawahi kupigana moja kwa moja na inakadiriwa kwamba vita kama hivyo vinaweza kusababisha uharibifu mkubwa.
Iran ina shehena kubwa ya makombora ya masafa marefu na ina washirika walio na silaha kali pia wanaopakana na Israel.
Israel nayo ina jeshi lenye nguvu sana na inadaiwa kuwa na silaha za nyuklia.
Aidha, Israel huungwa mkono kikamilifu na Marekani.













