Sababu ya Iran na Israel kushambuliana Syria

Iranian protesters pour kerosene on an Israeli flag during the funeral procession of Brigadier General Mohammad Ali Allahdadi in Tehran on January 21, 2015.

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Waandamanaji wa Iran wakichoma bendera ya Israel wakati wa mazishi ya afisa wa ngazi ya juu wa Iran aliyeuawa nchini Syria mwaka 2015

Israel imeshambulia kwa mabomu na makombora vikosi vya Iran nchini Syria na kuzua wasiwasi kwamba mataifa hayo mawili hasimu huenda yakapigana.

Lakini je, uhasama wao ulianza wapi na nini kinaweza kutokea?

Kwa nini Israel na Iran ni maadui

Tangu kufanyika kwa Mapinduzi ya Iran ya mwaka 1979, ambapo viongozi wa kidini wenye msimamo mkali walichukua mamlaka na kumaliza utawala wa Shah, Iran imekuwa ikiitisha kuangamizwa kwa Israel.

Iran husema taifa la Israel halina haki zozote za kuwepo, kwa sababu liliundwa kwenye ardhi ambayo ilitekwa kutoka kwa Waislamu.

Map showing locations of Israel, Syria and Iran

Israel hutazama Iran kama tishio kuu dhidi ya kuwepo kwake. Taifa hilo la Kiyahudi limekuwa likisisitiza kwamba Iran haifai kuruhusiwa kuwa na silaha zozote za kinyuklia.

Viongozi wao wana wasiwasi sana kuhusu kuenea kwa ushawishi wa Iran katika Mashariki ya Kati.

Syria inaingiaje katika mzozo huu?

Israel imekuwa ikifuatilia matukio katika taifa jirani la Syria kwa wasiwasi tangu vita vilipozuka mwaka 2011.

Israel imekuwa haishiriki katika vita hivyo kati ya serikali ya Bashar al-Assad na waasi.

Israeli army sergeant Amit Malekin, 19, commander of a mobile rocket launcher, poses for a picture in the Israeli-occupied Golan Heights near the border between Israel and Syria on February 26, 2018.

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Jeshi la Israel hulinda eneo la Golan Heights ambalo linakaliwa na Israel katika mpaka wake na Syria

Lakini Iran imeshiriki sana katika vita hivyo ambapo imetuma maelfu ya wapiganaji na washauri wa kijeshi kusaidia wanajeshi wa Bw Assad.

Israel ina wasiwasi pia kwamba Israel inajaribu kuwatuma wapiganaji na silaha kisiri nchini Lebanon - jirani mwingine wa Israel - ambayo pia huitishia Israel.

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu mara kwa mara amesisitiza kwamba taifa lake halitairuhusu Iran ijenge kambi Syria ambazo zinaweza kutumiwa dhidi ya Israel.

Kwa hivyo, kadiri Iran ilivyoendelea kujiimarisha nchini Syria ndivyo Israel ilivyodhidisha mashambulio dhidi ya kambi na wanajeshi wa Iran huko.

Iran na Israel zishawahi kupigana?

Hapa. Iran kwa muda mrefu imekuwa ikiunga mkono makundi yanayoishambulia Israel - kwa mfano Hezbollah wa Lebanon na kundi la Hamas la Palestina.

Lakini mataifa hayo mawili hayajawahi kupigana moja kwa moja na inakadiriwa kwamba vita kama hivyo vinaweza kusababisha uharibifu mkubwa.

Iran ina shehena kubwa ya makombora ya masafa marefu na ina washirika walio na silaha kali pia wanaopakana na Israel.

Israel nayo ina jeshi lenye nguvu sana na inadaiwa kuwa na silaha za nyuklia.

Aidha, Israel huungwa mkono kikamilifu na Marekani.