Tanzania yapanga kuvuna 10% ya mamba na viboko wote wa mjini

Muda wa kusoma: Dakika 2

Serikali ya Tanzania imetangaza kuuza asilimia 10 ya mamba na viboko nchini humo hususani katika maeneo ambayo yanamuingiliano mkubwa wa wanyama hao na binaadamu.

Hatua hiyo hata hivyo imeibua maswali mengi mitandaoni na kumlazimu Waziri wa Maliasili na Utalii Hamisi Kigwangalla amelazimika kueleza mtandaoni kwa nini serikali imeamuua kufanya hivyo na kuwa suala hilo lipo kwa mujibu wa sheria.

"...Ujangili tumeudhabiti kwa mafanikio makubwa sana. Changamoto mpya imezaliwa, wanyama wakali/waharibifu wanavamia maeneo ya watu. Tumeamua kuuza asilimia 10 ya mamba wote nchini," Kigwangalla alieleza kupitia mtandao wake wa Twitter.

Licha ya kuuza kiwango hicho cha mamba, Kigwangalla akaeleza kuwa wanapanga kujenga uzio kwenye maeneo ambayo matokeo ya mashambulizi ya mara kwa mara ya mamba kwa binadamu.

Pia viboko wote waliopo kwenye mabwawa, mito na maziwa yaliyo maeneo ya mjini watauzwa kwa kupitia mnada.

Hata hivyo, suasa hilo likaibua mjadala mkali mtandaoni.

Kigwangalla amefafanua kuwa suala hilo ni la kwaida na linafanyika baada ya utafiti na linaruhusiwa kwa mujibu wa sheria za nchi na kanuni za uhifadhi.

Pia amebainisha kuwa kila mwaka kuanzia Julai Mosi Tanzania hufungua shughuli za uwindaji, na huanza na wanyama kati ya asilimia 5 - 10 kutokana na aina husika.

Wanyama watakaouzwa ni madume ambayo yana umri mkubwa: "Hili la kuvuna wanyama lina kanuni na utaratibu wake wa kisayansi. Tunauza madume tupu tena yaliyozeeka. Hata tukiyaacha yatakufa tu na hatutopata faida yoyote ile. Pesa tunazopata huingia kusaidia shughuli za uhifadhi. Tuna maeneo makubwa sana tunayohifadhi kwa gharama kubwa," ameeleza Kingwangalla.