India yalitwaa jimbo la Kashmir, Pakistan yaapa kupinga kwa nguvu zote

Kashmir

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Kashmiri ni moja ya maeneo yenye uwepo mkubwa zaidi wa wanajeshi duniani

Serikali ya India kupitia chama tawala cha kihafidhina cha kihindu cha BJP inasherehekea hatua yake ya kuliondolea mamlaka ya kujitawala jimbo la Jammu Kashmir baada ya miongo saba.

Serikali ya India inadai kuwa kupewa hadhi ya kujitawala kwa jimbo hilo ilikuwa "makosa makubwa ya kihistoria".

Serikali ya nchi jirani Pakistani hata hivyo imepinga vikali hatua hiyo ya India, ikitahadharisha kuwa ni kinyume cha sheria na makubaliano ya kimataifa na watalipinga jambo hilo mpaka ngazi za Umoja wa Mataifa (UN).

Nchi hizo mbili huko nyuma zimeshawahi kupigana vita kutokana na mzozo wa eneo hilo, je dunia inaelekea kushuhudia tena mapambano ya nchi hizo ambazo tayari zinajihami na silaha nzito za nyukilia?

Kwanini Kashmir ni eneo tata?

An Indian activist holds a placard during a demonstration to protest against the presidential decree abolishing Article 370

Chanzo cha picha, Getty Images

Kashmir ni eneo lililopo kwenye safu za milima ya Himalaya na nchi zote mbili India na Pakistani zinadai kuwa ni eneo lao.

Katika kipindi cha ukoloni wa Mwingereza jimbo la Jammu na Kashmir lilikuwa na hadhi ya kujitawala kupitia kiongozi wa makabila, lakini likajiunga na India mwaka 1947 katika kipindi ambacho Bara Hindi lilipatiwa uhuru na kugawanywa katika mataifa mapya ya India na Pakistani.

Nchi hizo mbili huenda zikatumbukia vitani na kujikuta kila mmoja akishikilia sehemu ya eneo hilo baada ya makubaliano ya kusimamisha mapigano yalipoafikiwa.

Kumekuwa na ghasia katika upande wa jimbo hilo utakaotawaliwa na India kwa kipindi cha miaka 30 iliyopita.

Makundi ya wanaharakati wanaotaka kujitenga na India yamekuwa yakishinikiza kupewa uhuru wao.

Nini kimetokea hivi sasa?

Maelezo ya video, Mataifa ya India na Pakistan yalivyoundwa

Mwanzoni mwa mwezi wa Agosti, kulikuwa na dalili kuwa kuna jambo kubwa lingetokea katika jimbo la Kashmir.

Makumi ya maelfu ya wanajeshi wa ziada wa India yalipelekwa kwenye eneo hilo.

Shughuli kubwa ya kuhiji ya kihindu ilikatazwa na mamlaka, shule na vyuo viliamriwa kufungwa.

Watalii waliamriwa kuondoka mara moja na huduma za simu na mtandao wa intaneti kufungwa.

Viongozi wote maarufu wa kisiasa wa eneo hilo waliwekwa katika vizuizi kwenye nyumba zao.

Lakini wakati hayo yote yakiendelea, hofu kubwa ilikuwa ni kwamba ibara ya 35A ya katiba ya India ingelifutiliwa mbali.

Ibara hiyo ndiyo inayoipa Kashmir upekee na hadhi ya kujitawala.

Serikali ikashangaza kila mmoja kwa kufuta ibara nzima ya 370 ambapo 35A ni ibara ndogo, na sehemu hiyo ya katiba ndiyo imekuwa mwongozo wa sera za nchi hiyo juu ya Kashmir kwa miongo saba iliyopita.

Kashmir map
Presentational white space

Ibara ya 370 ina umuhimu gani?

Kwa kupitia ibara hiyo, Kashmir iliweza kuwa na katiba yake, bendera na uhuru wa kujitungia sheria zake. Mambo ya nje, ulinzi na mawasiliano zilibaki kuwa sekta ambazo zinaongozwa na serikali kuu ya India.

Kifungu hicho cha katiba kimekuwa kikipingwa na baadhi ya wananchi wa India hususan wahafidhina wa Kihindu.

Kashmir ndio jimbo pekee ambalo lilikuwa na Waislamu wengi lililojiunga na India wakati Bara Hindi lilipogawanywa.

Waziri Mkuu wa sasa Narendra Modi anaongoza chama chenye mrengo wa kihafidhina wa kihindu, na kuifutilia mbali ibara ya 370 ya katiba ilikuwa ni moja ya ahadi za kampeni za chama chake katika uchaguzi wa mwaka huu.

Viongozi wa chama tawala walidai kuwa jimbo hilo linabidi kuwa sawa katika kujiendesha na majimbo mengine yote ya India na baada ya ushindi wa kishindo katika uchaguzi uliofanyika mwezi Aprili-Mei chama hicho kimetekeleza ahadi yake bila kupoteza muda.

Hata hivyo wakosoaji wanasema uamuzi huo unatumiwa na serikali ili kujificha kutokana na mdororo wa kiuchumi ambao India unaupitia hivi sasa.

Kashmiri protesters clash with government forces in Srinagar, Indian-administered Kashmir in 2018.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Kumekuwa na ghasia kwenye upande wa Kashmir unaotawaliwa na India kwa miaka 30 sasa

Wenyeji wengi wa Kashmir wanaamini chama tawala cha BJP kinataka kubadili hali na sura ya jimbo hilo kwa kuruhusu wageni ambao si Waislamu kununua ardhi na kuhamia kwenye jimbo hilo.

Serikali inatetea uamuzi huo na kudai kuwa utaleta maendeleo makubwa kwenye jimbo hilo.

Members of Hindu Sena, a rightwing group, celebrate after the abolition of Article 370 in Delhi

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Wahafidhina wa Kihindu wamepokea hatua hiyo kwa mikono miwili

"Nataka kuwaambia watu wa Jammu na Kashmir kuwa ibara 370 na 35A jinsi ilivyoifanya jimbo lao," Waziri wa Mambo ya Ndani Amit Shah ameliambia Bunge. "Kutokana na ibara hizo, demokrasia imeshindwa kustawi kwenye eneo hilo, rushwa imetawala na hakuna maendeleo yaliyofikiwa."

Serekali pia inapanga kuligawa jimbo hilo katika majimbo madogo mawili. Jimbo moja litajumuisha eneo la Waislamu wengi wa Kashmir na wahindu wengi Jammu.

Jimbo la pili litakuwa Ladakh lenye Mabudha wengi na lipo karibu zaidi na jimbo la Tibet ambalo pia limekuwa likitaka kujitenga na Uchina.

Mwanasiasa mwandamizi wa upinzani kutoka chama cha Congress P Chidambaram, ameiambia serikali kuwa uamuzi huo ni wa balaa, na kuonya bungeni kuwa zinaweza kutokea vurumai kubwa.

Je ni uamuzi halali?

Kulingana na katiba, mabadiliko hayo yanaweza kufanyika pale tu patakapokuwa na makubaliano na serikali ya jimbo. Lakini kiuhalisia, hakuna serikali iliyokamilika na kuhudumu katika jimbo la Jammu na Kashmir kwa kipindi chazaidi ya mwaka mmoja sasa.

Mwezi Juni mwaka jana, India ilipoka uongozi wa jimbo hilo na serikali ya aliyekuwa waziri kiongozi wa jimbo hilo Mehbooba Mufti, ikafanywa kuwa serikali ndogo.

Hivyo, serikali kuu ili kupitisha mabadiliko ya sasa ilitakiwa kupata ridhaa ya gavana ambaye walimchagua wao wenyewe.

Serikali inasema kila ilichokifanya kimefuata misingi ya kisheria na wapo wanasheria wanaounga mkono msimamo huo.

Wapo wengine ambao wenye mawazo tofauti ikiwemo vyama kadhaa vya upinzani.

Vyama hivyo vinaweza kulipeleka jambo hilo mahakamani, japo watakuwa wanajiingiza kwenye mtego wa kupewa sifa ya kukataa umoja wa nchi ya India, hivyo kuna uwezekano mkubwa vita hivyo vikapambanwa na wanaharakati na watu binafsi.

Pakistani yapaza sauti

Waandamanaji Pakistani wakipinga hatua ya India

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Waandamanaji Pakistani wakipinga hatua ya India

Waziri Mkuu wa Pakistani Imran Khan ameapa kulifikisha suala hilo katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UN).

Bw Khan amesema uamuzi huo unavunja sheria ya kimataifa, na kudai kuwa anahofu kuwa uamuzi huo unaweza kutokomeza jamii moja (ya waisilamu).

"Ninahofu... (India) wanaweza kujaribu kuwafurusha wenyeji na kuingiza watu wapya ili wawe wengi zaid, hivyo wenyeji hawatakuwa na sauti na kubakia kuwa watumwa tu," Khan ameliambia bunge la nchi hiyo.

Kumekuwa na maandamano nchini Pakistani ambapo raia wa nchi hiyo wanapaza sauti zao dhidi ya hatua hiyo ya India.

Presentational grey line