Ziggy Wine: Mshirika mkuu wa Bobi Wine afariki baada ya kutekwa kwa siku kadhaa

Chanzo cha picha, Bobi Wine/facebook
Michael Kalinda, maarufu Ziggy Wine, msanii ambaye amekuwa akishirikiana na mbunge wa Kyadondo mashariki nchini Uganda Robert Kyagulani maarufu Bobi Wine amefariki.
Bobi Wine alithibitisha kifo cha Ziggy kilichotokea siku ya Jumapili usiku katika hospitali kuu ya kitaifa ya Mulago.
''Jana usiku ndugu yangu, rafiki na msanii mwenza Ziggy Wine alifariki katika hospitali ya Mulago'', alichapisha katika ukurasa wake wa akaunti ya facebook.
Ziggy alitekwa wiki chache zilizopita na watu wasiojulikana ambao walimpiga hadi akawa hatambuliki.

Siku ya Ijumaa Jioni bwana Kyagulani aliingia katika mtandao wa kijamii wa facebook na kutangaza: Rafiki yangu wa karibu na msanii mwenza alitekwa wiki chache zilizopita, kupigwa hadi akawa hajitambui jicho lake la kushoto likatolewa, vidole vyake viwili vikakatwa, vitu vyote alivyokuwa navyo vikachukuliwa na akutupwa katika hospitali ya Mulago ambapo alifariki.
Kulingana na familia yake, Ziggy alihudumu zaidi ya wiki moja katika chumba cha watu walio na majeraha mabaya bila matibabu yoyote.
''Alikuwa na maumivu mengi . Mara nyengine angetoka katika kitanda na kwenda msalani. Kuna wakati tulilazimika kumfunga na kitanda ili kumzuia'' , duru ziliambia the gazeti la The Daily Monitor nchini Uganda.
Je familia yake inasemaje?
Kulingana na dadake Magret Nalwanda Chocho watu waliomshambulia walidhani kwamba amekufa ndiposa wakampeleka na kumtupa katika hospitali ya Mulago.

Akizungumza na vyombo bya habari nchini Uganda bi Magret Nalwanda Chocho alisema kwamba walipatiwa barua ya kuondoka na msanii huyo katika hospitali ya Mulago na alipouliza ni kwa nini wanamtoa akiwa katika hali aliyokuwa ,aliambiwa kwamba 'hali yake iko nzuri na kwamba alihitaji chakula na dawa pekee'.
''Tulikuwa tukimlinda sana ili watu wasimkaribie kwa sababu hatukuamini hata rafikize wa karibu huku tukitaraji kwamba atatuelezea yale yaliotokea tangu kutoweka kwake'', alisema Immaculate.
Kauli ya vyombo vya usalama
Mapema, msemaji wa mji wa Kampala Patrick Onyango alisema kwamba familia ya Ziggy Wine haikuripoti kuhusu mtu aliyetoweka ama hata kushambuliwa lakini wakaahidi kufuatilia baada ya ripoti kutolewa.
Hatahivyo msemaji wa polisi Fred Enanga alisema kwamba idara hiyo imefungua faili ili kuchunguza kilichosababisha kifo chake.
''Tutahakikisha kwamba tunapata ripoti ya sababu za kifo chake na iwapo ripoti hiyo itasema kwamba Kalinda alifariki kutokana na sababu zisizo za kawaida basi tutalazimika kuchunguza ili kuhakikisha kuwa haki inapatakina''.

Enanga amesema kwamba maafisa wa polisi wametumwa katika hospitali hiyo ili kukusanya ushahidi wa kanda za CCTV ili kubaini ni gari gani lililomwasilisha msanii huyo katika hospitali ya Mulago.
''Pia tuna hamu kutokana na madai kwamba alitupwa akiwa katika hali mahututi katika hospitali ya Mulago, hivyobasi maafisa wetu wamekwenda Mulago ili kuona iwapo tunaweza kupata kanda za video za CCTV ili kuonyesha ni gari gani lililompeleka katika hospitali hiyo''.
Katika chapisho lake la mtandao wake wa facebook Bobi wine aliandika: Siku za mwisho za Ziggy Wine duniani zilikuwa za uchungu mwingi. Ziggy alikuwa mwanachama shupavu wa kundi la Firebase, kijana aliyefanya kazi kwa bidii. Kama vijana wengi wa Uganda alikuwa akitarajia taifa litakaloimarika, alisema Bobi Wine.













