Ifahamu shule inayofundisha walemavu wasioona, kusikia na kusema Tanzania

Shule ya Viziwi Iringa

Hebu fikiri maisha ya mtu anayeishi na zaidi ya aina moja ya ulemavu.

Hawezi kuzungumza, haoni na hasikii.

Maisha yao huwa magumu, kutokana na kushindwa kuona, kusikia, ama kupiga kelele ya kuomba msaada pale anapopatwa na hatari.

Changamoto hii siyo tu inawakabili walemavu hao, lakini pia wazazi, walezi ama watu wengine wanaoishi nao,

Mwalimu mkuu wa Shule ya Viziwi mkoani Iringa Tanzania Alinuswe Mwakosya akizungumzia changamoto hizo anasema unapoishi na mtu ambaye haoni na wala hasikii lazima utafute njia mbadala kumuwezesha kupata mawasiliano.

Anasema alama Mguso ndio wanayoitumia kuweza kuwasiliana na wanafunzi wao, ambao miongoni mwao wana aina tatu za ulemavu, kutokuona, kusikia na kuzungumza.

Shule ya Viziwi Iringa

'' Inahitaji umguse ndio ajue nini kinachotakiwa kufanywa, kwa hiyo ni changamoto katika kumuelewesha jambo. Mfano kuna wengine wanaletwa hapa hata choo hajui aende vipi, Wazazi wengi wanashindwa kuwadhibiti, mpaka mtoto anakuwa mkubwa bado anampa choo cha kujisaidia watoto (poti), lakini sisi tunachofanya ni kumfundisha ajue choo kiko wapi na aweze kujitambua kama anahitaji kwenda chooni...'' anasema mwalimu mkuu.

Shule hiyo ya viziwi ambayo inasimamiwa na Kanisa la Anglikana, Dayosisi ya Ruaha, imekuwa ikikabiliwa pia na uhaba wa vitendea kazi na wafanyakazi, wakiwemo walimu. Hali ambayo inafanya kazi ya kuwahudumia watoto hawa kuwa ngumu.

Maelezo ya sauti, Shule ya Viziwi Iringa

Askofu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Ruaha Dokta Joseph Mgomi anasema uwiano wa kuwatunza watoto wenye aina mbili za ulemavu, viziwi na kutosikia inatakiwa mtoto mmoja ahudumiwe na mwalimu mmoja pamoja na kuwa na mhudumu wake peke yake.

Hivyo shuleni hapo wana uhitaji mkubwa wa walimu na wahudumu kwa ajili ya watoto hao ambao wengine wana aina tatu za ulemavu.

Shule ya Viziwi Iringa

Amesema kwa wale wenye ulemavu wa kutosikia tu, watoto sita wanaweza kuhudumiwa na mhudumu mmoja.

''...Kwa kawaida walimu wanawafundisha mchana tu muda wa vipindi darasani, lakini wahudumu wanatakiwa kuwa nao muda wote, kutokana kwamba hawa watoto hawasikii na hawatoi sauti, wakati mwingine wanaweza kugombana wenyewe kwa wenyewe hivyo wanaweza kuumizana kama hakuna mtu karibu. Lakini pia yanaweza kutokea majanga mengine kama vile moto, ni hatari sana kama hata kuwepo mtu kule. Na ngumu zaidi ni kwa watoto ambao hawaoni wala hawasikii, jaribu kufikiria kama watu wako mbali...'' anasema askofu.

Mbali na changamoto hizo wanafunzi wa kike pia wamekuwa wakikabiliwa na changamoto kama vile uhaba wa taulo za kuwastiri wakati wa siku zao. Kutokana na baadhi wazazi wao kuwatelekeza shuleni hapo.