Iran yaikamata meli nyengine ya mafuta Ghuba, kwa mujibu wa vyombo vya habari

Meli ya Uingereza ya Stena Impero bado inaendelea kuzuiliwa na Iran

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Meli ya Uingereza ya Stena Impero bado inaendelea kuzuiliwa na Iran

Iran imeikamata meli nyengine ya mafuta katika Ghuba, kulingana na vyombo vya habari vya Iran .

Kamanda wa Jeshi la Iran la Revolutionary Guard alinukuliwa akisema kuwa wanamaji wa taifa hilo waliikamata meli ya kigeni ya mafuta katika Ghuba la Persia ambayo ilikuwa ikiyasafirishia baadhi ya mataifa ya Kiarabu mafuta kwa njia ya magendo .

Imesema kuwa meli hiyo ilikuwa ikibeba 700,000 za mafuta akiongezea kuwa mabaharia saba wanazuiliwa.

Kisa hicho kinajiri huku kukiwa na hali ya wasiwasi baada ya Marekani kuiongezea vikwazo Iran katika sekta ya mafuta.

Vikwazo hivyo viliwekwa tena baada ya Washington kujiondoa katika makubaliano ya kinyuklia ya Iran yalioafikiwa 2015.

Hii ni mara ya pili Iran imeishutumu meli ya kusafirisha mafuta kinyume na sheria.

Mnamo mwezi Julai , walinzi wa pwani ya Iran waliikamata meli iliokuwa ikipeperusha bendera ya Panama MT Riah.

Jeshi la Revolutionbary Guard , kwa mujibu wa mtandao wa Sepah News lilisema kuwa meli hiyo ilikamatwa wakati wanamaji wake walipokuwa wakipiga doria zenye lengo la kuwatafuta wale wanaofanya biashara haramu ya mafuta.

Pia mwezi uliopita , Iran iliikamata meli iliokuwa ikipeperusha bendera ya Uingereza kwa jina Stena Impero katika mkondo wa Hormuz ikidai kwamba meli hiyo iligongana na meli ya wavuvi wa samaki na kutoroka.

Marekani imeilaumu Iran kwa mashambulizi mawili ya kutumia vilipuzi katika Ghuba ya Oman mnamo mwezi Mei na Juni madai ambayo Tehran imekana.

Je tunajua nini kuhusu ukamataji huo wa hivi karibuni?

Chombo cha habari cha Fars kiliripoti kwamba operesheni hiyo ya kuikamata meli hiyo ilifanyika siku ya Jumatano karibu na Ghuba ya kisiwa cha farsi.

Meli hiyo ilisindikizwa hadi katika eneo la Bushehr na mafuta yake kuchukuliwa na utawala wa eneo hilo. Meli hiyo haikujulikana kwamba ilikuwa imetoweka.

Muhariri wa BBC wa maswala ya Arabuni Sebastia Usher anasema kuwa ijapokuwa mzigo wa meli hiyo ni mdogo kukamatwa kwake kutaendeleza hali ya wasiwasi katika eneo hilo.

Je ni nini kilichotokea awali?

Hali ya wasiwasi imeendelea kuwepo katika eneo la Ghuba tangu Marekani iiwekee vikwazo vya mafuta Iran .

Marekani imeilaumu Iran kwa mashambulizi mawili ya meli za mafuta katika Ghuba la Oman mnamo mwezi Mei na Juni- madai ambayo Tehran imekana.

Iran pia iliishambulia ndege isiokuwa na marubani ya Marekani katika mkondo wa Hormuz katika hali ya utatanishi.

Meli za kijeshi za Uingereza zimekuwa zikizilinda meli za mafuta za taifa hilo katika eneo hilo tangu Iran itishie kuzikamata meli zake ili kujibu hatua ya Uingereza kuikamata meli ya mafuta ya Iran Gibralta

Hatahivyo walishindwa kuizuia meli ya Stena Impero iliokuwa ikipeperusha bendera ya Uingereza.

Uingereza inasema kwamba meli hiyo iliokamatwa ilishukiwa kukiuka vikwazo vya EU dhidi ya Syria . Iran ilikana kwamba meli hiyo ilikua inaelekea Syria.