Tanzania: CCM yatwaa kiti cha Tundu Lissu Jimbo la Singida Mashariki

Tundu Lissu

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Lissu amekuwa nje ya Tanzania kwa matibabu toka Septemba 2017, amsema tarejea nyumbani atakaporuhusiwa na madaktari wake.
    • Author, Ambia Hirsi
    • Nafasi, BBC Swahili
  • Muda wa kusoma: Dakika 2

Mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Miraji Mtaturu, amepita bila ya kupingwa katika hatua za awali za matayarisho ya uchaguzi mdogo ambao ungefanyika kwenye Jimbo la Singida Mashariki, baada ya wagombea 12 wa vyama vya upinzani kutorejesha fomu.

Uchaguzi huo mdogo ulikuwa ufanyike Julai 31, mwaka huu, kufuatia aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Tundu Lissu kuvuliwa ubunge.

Afisa wa uchaguzi wa Wilaya ya Ikungi, Jonal Katanga amemtangaza Mtaturu Ijumaa jioni na baada ya kutowekewa pingamizi lolote.

Mtaturu amekabidhiwa cheti cha ubunge wa jimbo hilo lililokuwa likiongozwa na Tundu Lissu tangu mwaka 2010 hadi Juni 28, 2019.

Ruka X ujumbe
Ruhusu maudhui? (Mitandao ya kijamii)

Mkala hii imebeba madhui yaliyotoka kwenye mitandao ya kijamii. Tunaomba ruhusa yako kabla kitu chochote hakija pakiwa, sababu wanaweza wakawa wanatumia Cookies na tekinolojia nyingine. Unaweza ukasoma sera sera ya kutumia cookies katika mitandao ya kijamii kabla ya kukubali. Kutazama maudhui haya chagua accept and continue

Onyo: Imetoka kwingine na inaweza kuwa na matangazo

Mwisho wa X ujumbe

Kwa mujibu wa Gazeti la Mwananchi Mbunge huyo mteule alirejesha fomu jana kabla ya saa kumi jioni, muda ambao wagombea wote waliochukua fomu walitakiwa kuwa wamezirejesha.

Wagombea wengine waliochukua fomu ni Hamidu Hussein (ADA-Thadea), Tirubya Mwanga (UPDP), Ameni Npondia (CCK), Amina Ramadhan (DP), Ayuni John (UDP), Amina Mcheka (AAF), Maulid Mustafa (ADC), Selemani Ntandu (CUF), Feruzy Fenezyson (NRA), Abdallah Tumbo (UMD), Donald Mwanga (TLP) na Masalio Kyara (SAU).

Uchaguzi katika jimbo hilo ulikuwa umepangwa kufanyika Julai 31, 2019 kuziba nafasi iliyoachwa wazi na Lissu aliyepoteza sifa za kuwa mbunge kutokana na kutojaza fomu za mali na madeni na utoro bungeni.

Fomu ya Mtaturu ilibandikwa katika ubao wa matangazo wa ofisi ya halmashauri ya Ikungi ili kutoa fursa ya watoa pingamizi hadi leo saa kumi jioni.(Saa za Afrika Mashariki)

Lissu yupo nje Tanzania tangu Septemba 7, 2017 akitibu majeraha ya risasi alizomiminiwa akiwa katika makazi yake Area D jijini Dodoma akitoka kuhudhuria kikao cha Bunge kilichokuwa kikiendelea.

Mwanasiasa huyo mwandamizi wa upinzani nchini Tanzania, hivi karibuni aliiambia BBC kuwa anapanga kwenda Mahakama Kuu nchini Tanzania kupinga kuvuliwa ubunge.

Spika Ndugai

Chanzo cha picha, Bunge, Tanzania

Maelezo ya picha, Spika Ndugai

Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai, alitangazia bunge la nchi hiyo Ijumaa Juni 28 kuwa ameiandikia tume ya uchaguzi ya nchi hiyo kuileleza kuwa jimbo la Singida Mashariki, lililokuwa likishikiliwa na Lissu kupitia chama kikuu cha upinzani Chadema lipo wazi.

Mwanasiasa huyo pia ameiambia BBC kuwa yeye si mtoro bungeni na yungali anapokea matibabu barani Ulaya.

"Mimi si mtoro bungeni na sijawahi kuwa mtoro. Kilichonikuta kinajulikana, nilipigwa risasi 16 nikiwa natoka bungeni Septemba 7, nikaletwa nje kwa matibabu. Tangu hapo nipo nje natibiwa," amesema Lissu na kuongeza, "Kwanza walionishambulia mpaka sasa hawajulikani, hakuna aliyekamatwa. Leo inasemwa sijulikani nilipo navuliwa ubunge... kinachoendelea si ajabu, kuna watu hawana maarifa tena, walichobaki nacho ni mabavu tu."

Japo inafahamika kuwa mwanasiasa huyo alilazimika kusafirishwa nje ya Tanzania awali nchini Kenya na kisha Ubelgiji kwa matibabu baada ya shambulizi dhidi yake, kumekuwa na mjadala mkubwa juu ya kutokuwepo kwake bungeni kwa kipindi cha mwaka mmoja uliopita.

Hivi karibuni ikiwa yungali ughaibuni amezuru nchi za Marekani, Ujerumani na Uingereza, kote huko, amehojiwa na vyombo vya habari za kutoa mihadhara kwenye vyuo vikuu juu ya hali ya haki za binaadamu Tanzania.

Hali hiyo iliibua hoja miongoni mwa wakosoaji wake kuwa tayari amepona na anastahili kurudi Tanzania.