Uchumi wa China wapungua kasi baada ya miaka 27

Muda wa kusoma: Dakika 3

Kwa mara ya kwanza katika miaka 27 iliyopita, uchumi wa China umepungua kasi ya ukuaji wake katika robo ya pili ya mwaka.

Kuanzia mwezi Mei mpaka Juni mwaka huu, uchumi wa taifa hilo kubwa duniani ulikuwa kwa 6.2% ikilinganishwa na mwaka mmoja uliopita.

Matokeo hayo yanalingana na vile ilivyotarajiwa hali kuwa.

Serikali ya China inajitahidi kuchochea ukuaji wa uchumi kwa mwaka huu kwa kupunguza kodi na kuchochea matumizi.

Chia pia ipo katikati ya vita vya kibiashara baina yake na Marekani ambavyo vimeumiza hali ya biashara na ukuaji wa uchumi.

Data rasmi zilizotolewa na Ofisi ya Takwimu ya China zinaonesha kuwa kasi ya ukuaji imeshuka kutoka 6.4% ya mwanzoni mwa mwaka.

Rais wa Marekani Donald Trump ameandika kupitia ukurasa wake wa titter kuwa ushuru wa kibiashara kutoka Marekani "umeathiri pakubwa" uchumi wa China.

Mamlaka za China zinasema takwimu hizo zinaonesha hali ngumu ya kimazingira ndani na nje ya nchi.

"Uchumi umekuwa katika ustawi wa kutegemewa katika nusu ya kwanza ya 2019, lakini kuna nguvu kubwa ya kwenda chini kadri siku zinavyosonga," imeeleza Ofisi ya Takwimu ya nchi hiyo.

Uchambuzi

Andrew Walker, mwandishi wa biashara

Takwimu hizi zinaonesha kwa namna jinsi ugomvi wa kibiashara baina ya China na Marekani ulivyokuwa na athari. Ukuaji umeshuka kwa kiasi kikubwa ikilinganishwa na hali ambayo ingekuwepo kama kusingekuwa na ugomvi baina yao. Picha ya muda mrefu ni kuwa, uchumi wa China utaendelea kuwa imara japo utashuka kasi yake.

Kasi ya ukuaji wa uchumi wa China katika miongo mitatu iliyopita mpaka kufikia 2010 ilikuwa ni 10%. Lakini ilikuwa ni jambo la wazi miongoni mwa wachumi na hata baadhi ya viongozi nilioongea nao nchini China kuwa ukuaji huo usingelibaki hivyo milele.

Lengo lilikuwa ni kuhakikisha uchumi hautegemei zaidi uwekezaji na biashara ya nje badala yake kukuza vipato na matumizi ya raia. Hatua imepigwa katika eneo hilo, japo uwekezaji bado unachangia pakubwa uchumi wa Uchina.

Kuna hatari zake hata hivyo, la zaidi ni madeni makubwa ya makampuni. Mamlaka zilichochea makampuni kukopa kwa kasi baada ya uchi wa dunia kuyumba. Hiyo ilichangia pakubwa kuzuia anguko la ghafla la uchumi lakini ikaongeza hatari ya kifedha kwenye madeni.

Athari duniani kote

Ukuaji wa uchumi ukiyumba China unazalisha hofu kwengineko na mfumo mzima wa kidunia.

Edward Moya, mtaalamu wa uchumi kutoka taasisi Oanda, anasema takwimu hizo za kiuchumi "zinaonesha kuwa kuyumba kwa ukuaji wa uchumi wa China ni suala endelevu na masoko yategemee fedha zaidi za mikopo kutoka Benki Kuu ya China ili kuchochea ukuaji wa uchumi."

Mgogoro wa kiuchumi baina ya China na Marekani pia ni suala lengine la kuliangalia na athari zake zipo wazi sasa.

"Vita ya kibiashara ina atahari kubwa sana kwenye uchumi wa China, na hakuna suluhu yeyote inayotarajiwa basi tutarajie kuona uchumi ukishuka zaidi," amesema.

Japo pande zote mbili zilikubaliana kurudi kwenye meza ya mazungumzo walipokutana katika mkutano wa G20 nchini Japani, wametwangana ushuru katika bidhaa mbalimbali na kuumiza uchumi wa dunia.

Afrika ni bara ambalo linategemea pakubwa biashara na Uchina.

Ni nchi moja tu ambayo haina ushirikiano wa kibiashara na China ambayo ni eSwatini.

China ndiyo taifa lenye ushawishi mkubwa kibiashara Afrika baada ya kuipiku Marekani zaidi ya miaka 10 iliyopita.

Kwa ujumla thamani ya biashara baina ya China na Afrika kwa mwaka 2017 ilifikia kiasi cha dola bilioni 170 kutoka dola bilioni 10 mwaka 2000.

Ni dhahiri kuwa hali ya kusuasua kwa uchumi nchini China itaendelea basi Afrika nayo itaathirika pakubwa.