Mwanasoka nguli Joe Kadenge aaga dunia Kenya

Chanzo cha picha, John Nene
Mzee Joe Kadenge, anayefahamika kuwa nguli wa mchezo wa soka, ameaga dunia akiwa hospitali ya Meridian jijini Nairobi, gazeti la Daily Nation la Kenya limemnukuu mtoto wake Oscar.
Kadenge ameaga dunia akiwa na miaka 84, afya yake ilikuwa imedhoofu kwa muda. ''Baba hakuwa vizuri kiafya'', alisema Oscar.
Oscar amesema baba yake alikuwa anapata ugumu kupumua na pia alikuwa anapoteza uwezo wa kuona.
''Hali ilikuwa mbaya baada ya dada yangu kufariki nchini Marekani mwanzoni mwa mwaka huu na hakuweza kuhudhuria maziko.''
Rais Uhuru Kenyatta, vongozi wa upinzani Raila Odinga na Musalia Mudavadi ni miongoni mwa wale waliokuwa wakimtembelea mara kwa mara mzee Kadege alipokuwa mgonjwa.
Miaka miwili iliyopita Rais Kenyatta alimpa Kadenge shilingi milioni mbili na kuamuru mzee huyo kupewa kadi ya bima ya matibabu.
Wakati huo marehemu Kadenge alimshukuru rais na kuipa changamoto serikali kuwekeza kwenye michezo na kuwajali mashujaa wa michezo.

Chanzo cha picha, Ikulu Kenya
Wakati wa uhai wake akiwa mchazaji.
Kadenge alianza kucheza kandanda akichezea nafasi ya kiungo mshambuliaji na kisha mshambuliaji wa timu ya Maragoli United, kabla ya kujiunga na Abaluhya United (kwa sasa AFC Leopards) mwaka 1996.
Kadenge pia aliifundisha timu ya taifa, Harambee Stars ambayo ilifikia mafanikio makubwa.
Anakumbukwa kwa umahiri wake katika kuambaa na mpira akiwa katikati ya uwanja akihusishwa na msemo maarufu wa 'Kadenge na Mpira, Kadenge na Mpira' ulioanzishwa na mtangazaji nguli Leonard Mambo Mbotela.












