Messi apewa kadi nyekundu baada ya miaka 14 wakati Argentina ilipokutana na Chile

Chanzo cha picha, Getty Images
Lionel Messi ameonyeshwa kadi nyekundu ya pili baada ya miaka 14 wakati Argentina ilipoichapa Chile 2-1 katika michuano ya Copa America.
Mshambuliaji huyo alitoa usaidizi kwa Sergio Aguero kabla Paulo Dybala kuifungia Argentina goli la pili.
Lakini Messi alionyeshwa kadi nyekundu baada ya kusukumana uwanjani na Gary Medel akionyesha kuwa mwenye hasira, hatua ambayo ilimtoa nje pia mchezaji huyo wa Chile.
Hata hivyo, suala kubwa lililokuwa likizungumziwa ni kutolewa nje kwa Medel na Messi ambaye hajawahi kutolewa nje akiwa na Barcelona kwa miaka 14.
Mchezo ulionekana kuwa na mikikimikiki mingi kwa pande zote mbili na kusababisha kutoa nafasi kwa mipira ya adhabu.
Kulikuwa na hali ya mvutano dakika nane kabla ya kipindi cha mapumziko wakati Messi alipiga kiwiko Medel wakati wakigombea mpira.

Chanzo cha picha, PA Media
Medel alilipiza kwa kumsukuma Messi kwa uso wake, wakati wachezaji hao walipozozana kabla ya kufikiwa na mwamuzi na wote kutolewa nje.
Ilionekana kama vile Messi, katika kurejelewa tukio hilo, hakulipiza kitendo cha Medel.












