Nuh Mziwanda: 'Mapokeo ya mtu ndio changamoto katika vita dhidi ya mihadarati'

Ulanguzi na matumizi ya mihadarati Afrika mashariki
Maelezo ya picha, Ulanguzi na matumizi ya mihadarati Afrika mashariki

Leo ni siku ya Kimataifa ya kupinga matumizi na biashara ya dawa za kulevya, na Umoja wa Mataifa unasema watu milioni 35 duniani kote wanakadiriwa kutumia dawa za kulevya, tofauti na awali.

Katika ripoti yake ya kila mwaka Umoja wa mataifa unasema vifo vinavyotokana na matumizi ya kupindukia ya madawa ya kulevya yanaongezeka katika mataifa kama Amerika kaskazini huku mzozo ukishuhudiwa katika bara la Afrika kutokana na matumizi ya dawa ya Tramadol - dawa kali ya maumivu.

Kadhalika Umoja huo umetaja kuwa uzalishaji wa opium na cocaine umeongezeka kwa viwango vya juu sana, huku jitihada za kuzuia na kutibu waathirika zikipungua hususan katika magereza ya wafungwa.

Dr Kas Nyandindi kutoka Tanzania mojawapo wa mataifa ya Afrika masharki yanayoshuhudia athari za matumizi na ulanguzi wa mihadarati anaeleza kwamba hatua zimepigwa nchini humo katika kubaliana na tatizo hilo.

Anaeleza inatokana kwa kiasi kikubwa na ushiriki wa vijana katika kukabiliana na hali iliopo hasaa katika kutoa uhamasishaji katika jamii lakini pia kupitia kampeni mbali mbali za taasisi za madawa nchini.

Dkt Nyandindi anaeleza mnamo 2014 Tanzania ilishuhudia kati yawatumiaji laki tatu mpaka laki tano wa heroine sana sana kutoka eneo Dar es Salam.

Shirika la afya duniani WHO katika ripoti yake linaeleza kuwa kati ya 37.% na 75.% ya wakaazi wa Dar es Salaam wanaona ni rahisi sana kupata mihadarati kama pombe (ikiwemo ya kitamaduni), bangi na cocaine.

Ni changamoto kubwa katika bara zima la Afrika na wataalamu wa afya wanasema jitihada zimeidhinishwa ikiwemo kuyatambua maeneo yalioathirika pakubwa na kuyashughulia lakini kwamba hali bado haijaridhisha.

Kulingana na utafiti wa watumizi wa marijuana uliofanywa na shirika la New Frontier Data kutoka Uingereza, Taifa la Tanzania linaongoza kwa idadi ya watu wanaovuta bangi katika eneo la Afrika mashiriki.

Maelezo ya video, Sumu ya panya yageuzwa dawa za kulevya Tanzania

Na ni katika vita hivi ambapo baadhi ya wasanii Afrika mashariki wanajitosa kupitia sanaa na kampeni mbali mbali kushinikiza vita dhidi ya matumizi na usafirishaji mihadarati katika jamii.

Tumezungumza na wasanii wawili, Nuh Mziwanda kutoka Dar es Salaam Tanzania na Dazlah Kiduche kutoka Mombasa Kenya - miji miwili iliyoathirika pakubwa kwa ulanguzi na matumizi ya madawa ya kulevya.

Presentational grey line
Nuh Mziwanda

Chanzo cha picha, Nuh Mziwanda

Nuh Mziwanda - Dar es Salaam Tanzania

Binafsi Nuh anasema hajawahi kama kijana kutumia mihadarati lakini ameshuhudia jamaa na marafiki walio karibu na yeye wakitumbukia katika matumizi ya madawa ya kulevya.

Anasema kama msanii amejihusisha katika kutoa ushauri, ikibidi mara nyingine kuwafuata na kuwaomba vijana kuachana au kujiepusha na matumizi ya madawa hayo kupitia tamasha za muziki akitoa mfano wa lililofanyika katika eneo la Ilala.

Nuh anaeleza kwamba sio rahisi hatahivyo kutumia vipaji kuhamasisha - 'inahitaji uwe mradi wa ushirikiano' anaeleza ila amesema ni muhimu kama wasanii kujipatia changamoto ya kuchukua usukani.

Katika kupongezea jitihada zilizopigwa , ametoa mfano wa huduma inayotolewa katika vituo vya afya kama Mwananyamala ambapo waathirika hupokea matibabu.

Sanaa inakuwa sana na vijana wanajiingiza huko katika kuwavutia vijana wengine.

Zingatio anaeleza ni kuwa na uangalifu katika kuiga wengine.

Inasikitisha kuona vijana wa umri mdogo wengine kuanzia miaka 18 - 19 wakianzia taratibu tu na kuzidisha uraibu, anasema.

'Changamoto ni mapokeo ya mtu na mtu - kuna utakayemshauri akapokea ushauri na kuna wasiolipendelea hilo' anasema.

Anaongeza kuwa ni rahisi kubadili mienendo ya vijana ila kikubwa ni kupambana na hali kumalizika.

Presentational grey line
Dazlah Kiduche

Chanzo cha picha, Dazlah Kiduche

Dazlah Kiduche - Mombasa Kenya

Duzzler Kiduche msanii kutoka Mombasa Kenya anasema imekuwa changamoto kubwa kuishi katika mitaa ambapo vijana, marafiki, unaotoka nao mtaa mmoja, wanatumia na inakuwa vigumu kuwashawishi kuachana na matumizi ya madawa ya kulevya.

Anautaja mji wa Mombasa kama eneo linaloonekana kuathirika pakubwa.

Anaeleza kwamba vijana wenyewe wana nafasi kubwa ya kushinikiza jitihada kutokana na uelewa wa lugha wanayotumia.

Anasema muziki wanaotunga wasanii kwa kutumia lugha inayowavutia vijana hao ni fursa kubwa.

Jitihada za mapambano ya madawa ya kulevya - anasema licha ya hatua kupigwa katika miaka ya hivi karibuni japo kwa uchache , anasisitiza kwamba 'bado mapambano yanastahili kuongezeka kwasababu ushawishi upo mkubwa'.

Bangi ndio mihadarati inayotumika sana barani Afrika huku kukiwa na kiwango cha wastani cha kila mwaka cha asilimia 11.4 kati ya watu wazima wenye umri wa kati ya 15-64, ikikaribia kuwa mara mbili ya kiwango kinachotumika duniani cha asilimia sita, kwa mujibu wa ripoti ya New Frontier Data nchini Uingereza.

Presentational grey line

Madhara ya Bangi

  • Unaweza kusababisha kuchanganyikiwa na wasiwasi usio wa kawaida
  • Ikivutwa na tumbaku, inaweza kuongeza hatari ya ugonjwa kama vile saratani ya mapafu
  • Matumizi ya mara kwa mara yamehusishwa na hatari ya kupatwa na magonjwa ya kiakili
  • Upungufu wa kudumu wa kiwango cha mtu kufikiria na kufahamu mambo, baada ya kutumia kwa muda mrefu

Umoja wa mataifa ulitangaza leo Juni 26 kama siku ya kimataifa ya kupinga matumizi na biashara ya dawa za kulevya kama kielelezo cha azimio lake kuimarisha hatua na ushirikiano kufikia lengo la jamii ya kimataifa isiyokuwa na matumizi ya madawa ya kulevya.