Wanja Kimani: Mwanamke aliyeamua kwa hiari kuwa hataki watoto katika ndoa yake

Chanzo cha picha, @BRIT/nappy
Wanja Kimani - ni mwanamke 'asiye wa kawaida' ikiwa tutamtazama kwa kutumia jinsi jamii ya Kiafrika inavyotafsiri ndoa na uzazi.
Amekuwa kwenye ndoa kwa miaka 20. Yeye na mumewe waliamua kwamba katu, hawatapata watoto.
Katika Mahojiano na BBC Swahili, Bi Wanja alifunguka kuhusiana na msimamo wake huku akiutetea sana.
Yeye amezaliwa miongoni mwa ndugu watatu wanawake, malezi yao anasema yalikuwa ya kawaida.
Bi Wanja anasema kuwa hajashawishika kuwa ufanisi wa ndoa au ili iitwe ndoa kamili, ni lazima kuwe na hesabu ya watoto.
Kwa mtazamo wake, ndoa ni kati ya mume na mke, na wawili hao wanaweza kuamua vengine.
Lakini kwa nini akaamua kuishi bila watoto ?
Alisema kuwa haja yake kuu katika maisha hajaiona ama kuitambua kuwa ni kuzaa watoto.
Wanja anasema 'Ninapotembea huko nje unaona kina mama wengine wana watoto wengi lakini hawajali kuhusu watakacho kula, watakavyosoma na kadhalika, kwa hio najiuliza mbona kazaa na hana huruma na yule mwanawe?'

Anasema kuwa ilibidi ajitazame na kuelewa ikiwa yeye anataka kweli kuwaleta watoto duniani alafu waanze kuteseka.
Bi wanja ameeleza kuwa yeye hawachukii watoto bali haamini kuwa lengo lake kuu duniani linaambatana na kuzaa.
'Nilipojitathmini kwa undani , ni kana kwamba mimi sina zile hisia za kuwa mama, Na sikutaka kuleta watoto duniani kisha nianze kuwatelekeza "
Aliendelea kusema kuwa hata mumewe wa miaka 20 ana maoni sawa naye.
'Ni kana kwamba Mungu aliufahamu moyo wangu kwani alinipatanisha na mtu ambaye tulikuwa na maoni na msimamo sawa ".
Anasema kuwa ni kama sadfa kwani tangu walipoonana kwa mara ya kwanza, mmojawapo ya mambo yaliowaleta pamoja ni kuwa wote walikuwa hawatamani kuwa na watoto wakiwa kwenye ndoa.
Hatahivyo uamuzi huu sio mwepesi na wamekuwa wakikabiliwa na unyanyapaa ambao umeandamana na kauli za watu kuhusiana na msimamo wake.
Kwa mtazamo wake sio kwamba mtu asipozaa mtoto huwa ndio maisha hayajakamilika.
Wanja ni miongoni mwa wanawake wachache, ambao wana uwezo wa kuzaa lakini wao wameamua kuwa hesabu ya watoto haipo katika mpangilio wao wa maisha.
Mila na desturi nyingi miongoni mwa Wa-afrika zinawashinikiza wanawake wanaoolewa kuzaa, ndiposa waonekane wanawake kamili katika ndoa.
Wengi ambao wanajipata na matatizo yanayowazuia kushika uja uzito wanakuwa na mtihani mkubwa, kutokana na unyanyapaa kutoka kwa jamii na wengine hata ndoa zao kuishia kuvunjika.
Licha ya hali hiyo, Wanja anasema kuwa hajutii uamuzi huo wa kuishi maisha bila ya mtoto.
















