Doriani lapigwa mnada kwa dola 48,000 nchini Thailand

Chanzo cha picha, Chaiwat Subprasom/SOPA Images/REX/Shutterstock
Doriani la kifahari - lifahamikalo kama mfalme wa matunda - limenunuliwa kwa kima cha baht milioni 1.5 za Thailand (sawa na $48,000) katika mnada mmoja jijini Bangkok.
Inategemea utamuuliza nani, tunda la doriani laweza kuwa mfalme wa matunda au tunda lenye harufu kali kuliko yote.
Je, lina thamani kiasi gani? Tajiri mmoja mpenda vyakula ametoa jibu hivi karibuni.
Katika mnada huo kwa ajili ya kusaidia watu wenye uhitaji uliofanyika wiki iliyopita bwana huyo alitoa kitita hicho.
Kwa mujibu wa vyombo vya habari nchini humo, tunda hilo lilichumwa siku moja kabla ya mnada. Na bei hiyo ni mara mbili ya rekodi ya mwisho iliyowekwa kwenye mnada huo hapo kabla.
Bei ya kawaida ya tunda hilo lililo kwenye ubora ni kati ya dola 50 mpaka 100.
Tunda la doriani linapendwa sana katika nchi nyingi za bara Asia lakini pia wapo wengi wanaolichukia.
Harufu yake imefanya lipigwe marufuku kwenye usafiri wa umma, mahoteli na ndege kwenye baadhi ya nchi.

Chanzo cha picha, Getty Images
Novemba mwaka 2018, ndege moja nchini Indonesia ililazimika kutua ghafla baada ya abiria kulalamikia harufu kali ya tunda hilo kwenye ndege. Ilifikia wakati abiria kutaka kuwapiga wahudumu wa ndege hiyo kwa kuruhusu tunda hilo kama sehemu ya mizigo.
Mwezi Aprili 2018, zaidi ya wanafunzi na walimu 500 katika Chuo Kikuu kimoja nchini Australia ilibidi waokolewe kwa haraka na polisi kutokana na harufu kali ambayo awali ilidhaniwa kuwa ya gesi.
Hata hivyo baadae iligundulika kuwa harufu hiyo ilikuwa ni ya tunda la doriani ambalo lilikuwa limenza kuharibika kwenye moja ya makabati ya maktaba ya chuo hicho.

Chanzo cha picha, SOUTH CHINA MORNING POST/GETTY IMAG
Vikosi vya zimamoto vikaeleza kuwa harufu hiyo ilienezwa kwa haraka na mifumo ya kupoza na kusambaza hewa ya maktaba hiyo.
Mapema mwaka huu, bwana mmoja nchini Uchina alikamatwa na polisi wa usalama barabarani baada ya kushindwa kipimo cha kupima pumzi kitumikacho kuwanasa madereva wanaoendesha huku wakiwa wamekunywa pombe.
Bwana huyo alionekana katika mkanda wa video akiwakatalia maaskari hao kuwa hakuwa mlevi na badala yake alikuwa amekula madoriani kwa kiwango kikubwa.
Baada ya kufanyiwa vipimo zaidi vya damu, ikagundulika kuwa ni kweli bwana huyo hakuwa na pombe kwenye mfumo wake wa mwili na kuachiliwa huru.












