Je China kutumia madini yake ya kipekee kama turufu katika mzozo wa kibiashara na Marekani?

Chanzo cha picha, Getty Images
China imekuwa ikionesha dalili kwamba huenda ikadhibiti usafirishwaji wa madini yake ya kipekee na adimu kwenda Marekani kipindi hiki mzozo wa kibiashara kati ya mataifa hayo mawili ukizidi kufukuta.
Madini hayo kutoka China ni malighafi kuu ambayo hutumiwa na kampuni nyingi za Marekani kutengeneza vitu kama magari yanayotumia nguvu za umeme, simu na bidhaa nyengine nyingi za kielektroniki.
Mwaka jana utafiti uliofanywa na shirika la Jiolojia la Marekani uliorodhesa madini hayo kama yenye umuhimu mkubwa katika uchumi na ulinzi wa taifa la Marekani.
"China inatathmini hatua ya kuthibiti usafirishwaji wa madini hayo ya kipekee nchini Marekani," Gazeti la kitaifa la Global Times, liliandika katika mtandao wake tweeter wiki hii.

Chanzo cha picha, Getty Images
Madini hayu ni yapi?
Madini hayo adimu, ambayo hufahamika kwa lugha ya Kingereza kama rare earths ni kundi la madini 17 yanazotumiwa kwa utengenezaji na ukuzaji wa vitu kadhaa katika sekta mbalia mbali, ikiwemo nishati mbadala, bidhaa za kielektroniki, bidhaa za kutengeneza mafuta na pia hutumika kutengeneza vioo.
Japo madini hayo husemekana ''hayapatikani'' kwa urahisi, utafiti uliyofanywa na Shirika la Jiologia la Marekani umebaini kuwa yanapatikana kwa wingi katika ukoko wa dunia
Hata hivyo kuna sehemu chache sana duniani kunakopatikana migodi inayotoa madini hayo.
Uchimbaji wake ni mgumu sana na umetajwa kuwa chanzo cha uharibifu wa mazingira.
China ndio kinara wa uzalishaji wa madini hayo kwa kutoa asilimia 70.
Myanmar, Australia, Marekani na mataifa mengine pia huchimba madini hayo kwa kiasi kidogo.
Katika kuchakata makinikia ya madini hayo, China inaongoza zaidi.
Mwaka jana karibu 90% ya uchakatwaji wa makinikia yake ulifanyika nchini China.
Kampuni moja ya Australia inayoendesha shughuli zake nchini Malaysia ilichakata kiasi kilichobaki.
Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita kiwango cha uzalishaji wa madini hayo ya kipekee kilichosafirishwa nje ya China kiliongezeka mara mbili zaidi kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na nchi hiyo.
Marekani inaitegemea China kwa kiwango gani?
Marekani inaagiza karibu 80% ya kundi la madini hayo 17 ya kipekee kutoka China, takwimu za serikali ya Marekani zinabainisha.
Estonia, Ufaransa na Japan pia zinaiuzia Marekani madini hayo japo kwa uchache.
Kampuni pekee inayosafisha madini hiyo nchini Marekani hutuma malighafi yake Uchina kusafishwa - na tayari imeathiriwa na nyongeza ya kodi ya 25% iliyowekwa na China.
Marekani inaweza pia kuagiza madini hayo kutoka Malaysia, lakini sio kwa kiwango kitakachokidhi mahitaji yake.
Serikali ya Malaysia imetishia kupiga marufuku uchakatwaji wa madini hayo kutokana na sababu za kimazingira.

Chanzo cha picha, Getty Images
Je, Marekani ina uwezo wa kuanzisha kampuni yake ya kusafisha madini hayo ya kipeke ambayo ni vigumu kupatikana?
Hilo bila shaka linawezekana , lakini itachukua muda kwasababu itakabiliwa na changamoto ya kupata malighafi ikiwa China itaondolewa katika mnyororo wa uzalishaji wa bidhaa hiyo kwenda Marekani.
Hadi mwaka 1980, Marekani ilikuwa ndiyo mzalishaji mkubwa wa madini hayo.
China ishawahi kudhibiti usafirishaji wa madini hayo hapo kabla.
Mwaka 2010, walichukua hatua hiyo dhidi ya Japan, kufuatia mzozo wa kimaeneo.
China ikiidhinisha hatua ya kudhibiti uuzaji wa madini yake, kampuni nyingi za Marekani zinazotegemea madini hayo kuendesha biashara zao zitapoteza matrilioni ya dola.












