Mazungumzo ya Sudan yakwama huku jeshi likidai vizuwizi viondolewe

Chanzo cha picha, Reuters
Viongozi wa kijeshi Sudan limesitisha kwa muda wa siku tatu mazungumzo na waandamanaji juu ya kubuniwa kwa baraza huru la mpito, wamesema viongozi wa waandamanaji pamoja na jeshi.
Katika taarifa iliyotolewa kwenye televishini nchini humo, baraza la Mpito la Kijeshi (TMC) lilisema vizuwizi vilivyowekwa kwenye maeneo mbali mbali na waandamanaji mjini Khartoum sharti viondolewe.
Risasi zilifyatuliwa Jumatano wakati wanajeshi walipokuwa wakijaribu kuondoa vizuwizi mjini khartoum.
Duru zinasema kuwa hakuna tarehe mpya iliyotangazwa kwa ajili ya mazungumzo, ambayo yaliytarajiwa kukamilisha makubaliano juu ya wajumbe wa utawala utakaoliongoza taifa katika kipindi cha mpito hadi uchaguzi utakapofanyika.
Jumatano watu wapatao tisa walijeruhiwa wakati wanajeshi wa Sudan walipotumia risasi kuwatawanya waandamanaji katikakati mwa mji mkuu Khartoum, lilisema kundi la waandamanaji.
Taarifa za awali zilisema kuwa mazungumzo ya kuunda baraza litakaloongoza taifa kipindi cha mpito yameahirishwa kwa muda wa saa 72.

Chanzo cha picha, REUTERS
Sudan imekuwa ikiongozwa na baraza la kijeshi tangu kung'olewa madarakani kwa kiongozi wa muda mrefu Omar al-Bashir aliyepinduliwa mwezi uliopita, lakini limeshindwa kurejesha taifa katika hali ya utulivu.
Waandamanaji walioshinikiza kuanguka kwa utawala wa Bwana Bashir wameendelea kufanya maandamano ya kukaa nje ya makao makuu ya jeshi mjini Khartoum kudai jeshi likabidhi mamlaka kwa raia.
Ghasia za hivi karibuni zimetia dosari katika mazungumzo ambayo yalionekana kuleta matumaini ya kuundwa baraza la jeshi na kiraia kuongozanchi hiyo kwa miaka mitatu hadi utakapofanyika uchaguzi.

Chanzo cha picha, EPA
Upinzani unasemaje?
Akizungumza kabla ya tangazo la jeshi, Rashid al-Sayid,msemaji wa baraza la muungao wa upinzani- Alliance for Freedom and Change, aliliambia shirika la habari la AFP kwamba : "Baraza la jeshi lilituambia kwamba waandamanaji lazima waondoe vizuwizi na kurejea kwenye kwenye mgomo wa kukaa ."
Kiongozi mwingine wa ulinzani , Ahmed Rabie, alithibitisha kuwa mazungumzo yalikwama , akisema kuwa jeshi lilitaka barabara katika mji wa Khartoum na maeneo mengine zifunguliwe kabla ya kurejea kwenye meza ya mazungumzo.

Chanzo cha picha, AFP
Makubaliano ambayo tayari yamefikiwa?
Katika mkutano wa pamoja na waandishi wa habari siku ya Jumanne usiku ,msemaji wa TMC Luteni Jenerali Yasser al-Atta alisema kuwa mkataba umefikiwa wa uundwaji wa kipindi cha mpito cha miaka mitatu kuelekea utawala wa kiraia.
Alisema kuwa makubaliano ya mwisho juu ya mgawanyo wa madaraka yatasainiwa na Muungano wa upinzani katika kipindi cha saa 24. Hiyo ikiwa ni pamoja na kuundwa kwa baraza huru ambalo litaongoza nchi hadi utakapofanyika uchaguzi.
Jenerali Atta alisema kuwa Muungano wa upinzani utakuwa na theruthi mbili ya viti vya bunge la mpito litakalokuwa na wabunge 300, huku viti vilivyosalia vikichukuliwa na makundi mengine.
Awali , msemaji wa vuguvugu la maandamano Taha Osman alisema kuwa pande zote zilikubailiana juu ya muundo wa mamlaka zinazotarajiwa - baraza huru, barza la mawaziri na bunge.













