Tanzania: Hofu yatanda baada ya makaburi ya albino kufukuliwa na watu wasiojulikana

albino

Chanzo cha picha, Getty Images

Watu wenye ualbino nchini Tanzania wamemtaka rais wa nchi hiyo John Magufuli kuingilia kati wimbi la kufukuliwa kwa makaburi ya watu wenye ualbino.

Chama cha albino cha nchi hiyo kimesema watu wenye albino wameanza kuwa na hofu kwani hawajui nia na msukumo wa kufukuliwa kwa miili ya wenzao.

Wiki iliyopita mwili wa mmoja wa albino aliyekufa mwaka 2015 ulifukuliwa na baadhi ya mabaki kuchukuliwa na watu wasiojulikana.

Katibu Mkuu wa chama cha watu wenye albino Tanzania Mussa Kibimba anasema malalamko yao yanakuja mara baada ya matukio ya mfululizo ya kufukuliwa kwa makaburi kule Mbeya .

Mpaka sasa makaburi mawili tayari yamefukuliwa huko Mbeya na haijajulikana dhumuni la kufukuliwa kwa miili yao na hata kujulikana masalio ya miili hiyo inaenda wapi?

Kaburi la Aman Anywelwisye Kalyembe ambaye alikuwa ni mtu mwenye ualbino aliyekufa mwaka 2015 wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya, kaburi lake limefukuliwa tarehe 24 mwezi Aprili na watu wasiojulikana.

Kibimba anaeleza kuwa hofu kubwa imekuja kwao sababu miaka mitano iliyopita waliishi kwa wasiwasi sana hivyo jambo kama hilo likitokea lazima liwashitue.

"Ukatili na uovu wa mauaji dhidi ya albino ulikuwa mkubwa nchini mpaka hii leo wenzetu ni walemavu wa viungo na wengine waliuwawa kutokana na unyanyasaji huo.

Bado sisi ni wahanga na tuna misukosuko ya mawazo kwa sababu ya usalama wetu "Katibu mkuu wa chama cha albino Tanzania.

Matukio haya ya kufukua makaburi yameleta hofu miongoni mwa albino na familia zao huku wengine wakidhani kuwa matukio hayo yanafanyika kwa sababu muda wa uchaguzi mkuu nchini humo umekaribia.

Aidha watetezi wa haki za binadamu wanasema ushambulizi dhidi ya watu wenye ualbino umepungua sana lakini sasa uvamizi umeelekea kwenye makaburi yao kufukuliwa.

Matukio ya kufukuliwa makaburi yalianza kuripotiwa tangu mwaka 2016.

albino

Chanzo cha picha, AFP

Tanzania ni miongoni mwa nchi za bara la Afrika lenye watu wengi wengi wenye ualbino nao hutambuliwa kutokana na rangi yao ya ngozi,macho na nywele zao .

Mauaji ya albino yalishamiri kutokana na matakwa ya waganga wa kienyeji ambao huwaambia wateja wao kwamba viungo vya Albino huleta bahati ya kupendwa,maisha marefu na mafanikio katika biashara.

Wakati jambo hilo makosa kufikiria kwamba mtu akiwa na viungo vya mtu mwenye u- Albino vitaweza kumsaidia kumletea mafanikio katika biashara, ama atavua samaki wengi na hata kupata madini mengi machimboni.