'Shujaa' atengeneza barabara kwa mikono yake kuwasaidia wanakijiji Kenya

Nicholas Muchami

Chanzo cha picha, Philip Kinyungu

Maelezo ya picha, Nicholas Muchami amekua akifanya kazi ya kutengeneza barabara bila malipo

Mwanaume mmoja nchini Kenya ameiambia BBC kuwa ameamua kutengeneza barabara kwa mikono yake ili kuondokana na adha inayowakabili wanakijiji wenzie.

Akitumia Jembe, Shoka na Koleo, Nicholas Muchami mpaka sasa amekwishatengeneza barabara ya umbali wa kilomita 1.5 ndani ya siku sita na amebakiza kipande kidogo amalize barabara yote.

Amefikia hatu hiyo baada jaribio la kuwashawishi viongozi wa kijiji kujenga barabara kugonga mwamba.

Amekua akimwagiwa sifa tele kwa jitihada zake katika kijiji cha Kaganda.

Maelezo ya video, Mchongaji sanamu maarufu anayetumia mkono mmoja Kenya

Wakazi wa kijiji hicho katika Kaunti ya Muranga, iliyo umbali wa kilometa 80 kutoka mji mkuu Nairobi, wamekua wakitumia barabara ya umbali wa kilometa 4 kufika katika maeneo ya kupata mahitaji yao.

Mwandishi wa BBC, Peter Mwai anasema wanakijiji walikua wanaudhika kwa kuwa njia ya mkato kuelekea kwenye maduka kwa njia ya miguu ilikua imezibwa hali iliyomfanya bwana Muchami kuchukua hatua.

Barabara ya Nicholas Muchami

Chanzo cha picha, Philip Kinyungu

Maelezo ya picha, Barabara ni pana kiasi cha kuwezesha gari kupita.

''Nina nguvu nyingi .Niliamua kujitolea,'' aliiambia BBC.

Anasema alifanya kazi tangu saa moja kamili asubuhi mpaka saa kumi na moja jioni Jumatatu mpaka Jumamosi akitaka kuikamilisha barabara hiyo kabla ya majira ya mvua.

''Nilipokua nikifanya kazi hii, watu walikua wakiniuliza, 'unalipwa'? alisema.

Nicholas Muchami

Chanzo cha picha, Philip Kinyungu

Maelezo ya picha, Bwana Muchami amekua akifanya kazi wa saa nane kwa siku

Ingawa nusu kilometa ya barabara bado inahitajika kumaliziwa, wanakijiji wakiwemo wanafunzi wanaoelekea shule za msingi na sekondari za karibu, wamekua wakitumia sehemu ya barabara iliyokamilika.

''Sasa imewafanya watu wafurahi, nami nimefurahi pia.Kazi yangu imewasaidia watu wa kila aina,'' alisema mwanaume huyu mwenye miaka 45.

Ana mpango wa kuendelea kutengeneza kipande cha barabara kilichobaki, ingawa wanakijiji wengine walikataa kumsaidia kwa kuwa hakuna aliye tayari kufanya kazi bila kulipwa, alisema.

Hadithi yake kwa mara ya kwanza iliwekwa kwenye ukurasa wa Facebook wa Kinyungu Micheke, aliyemsifu Muchami kwa hatua aliyochukua baada ya majibu hasi aliyoyapata kutoka kwa viongozi wa kijiji kukataa kumsaidia.