Wamiliki wa malori Tanzania walalamikia sheria ya udhibiti wa uzito wa magari ya EAC

Baadhi ya Wafanyabiashara wa nchi za SADC wagomea kutumia bandari ya Dar es Salaam
Maelezo ya picha, Sheria mpya ya udhibiti uzito ya Jumuia ya Afrika Mashariki imelalamikiwa kuikosesha mapato waendesha malori Tanzania
Muda wa kusoma: Dakika 3

Wamiliki wa malori nchini Tanzania wamelalamika kuhusu sheria ya udhibiti wa uzito wa magari ya Jumuia ya Afrika Mashariki wakisema kuwa sheria hii inawagharimu kwenye soko

Sheria ya udhibiti wa uzito wa magari ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na Kanuni zake za mwaka 2017 ilianza kutumika rasmi mwaka huu, huku wadau wakitakiwa kutii sheria hiyo ili kuepuka adhabu kali zinazoweza kutolewa.

Sheria inasemaje?

Sheria mpya inaeleza kuwa ukomo wa mtaimbo(Axle) wenye matairi mapana utakuwa tani 8.5 badala ya tani 10 za awali.

Kuwepo kwa mfumo wa kuweka kumbukumbu za makosa ya msafirishaji na anayezidisha uzito ambao hatimaye unaweza kusababisha gari kufungiwa kufanya usafirishaji kwa muda au moja kwa moja.

Adhabu ya malipo ya faini kwa makosa ya usafirishaji hadi dola za Marekani 15,000 au kifungo kisichozidi miaka 3 au vyote kwa pamoja.

Adhabu hizo zinahusu pia watumishi wa mizani wanaoshiriki njama na wasafirishaji ili kukwepa kulipa tozo ya kuzidisha uzito .

Gharama za utunzaji gari iliyokuwa na makosa katika maeneo ya mizani baada ya siku tatu ni dola za Marekani 50 kwa siku badala ya dola za Marekani 20 kwa siku kwenye sheria hii mpya.

Makamu mwenyekiti wa chama cha wamiliki wa malori nchini Tanzania, Elias Lukumay amezungumza na BBC, amesema hali ni ngumu mno kwa wafanyabiashara kutokana na sheria hii

Bandari ya Dar es Salaam

Chanzo cha picha, Tanzania today website

Maelezo ya picha, Nchi wanachama wa SADC kwa kiasi kikubwa hutegemea Bandari ya Dar es Salaam

'' Bandari ya Dar es Salaam kwa asilimia 70 inategemea nchi za SADC, lakini kwa sasa sheria itatuumiza kwenye soko.''

Maelezo ya video, Jeshi la Tanzania limeanza rasmi operesheni ya kuratibu ununuzi wa korosho

Kuhusu sababu za kuwa sheria hii kulenga kulinda miundombinu yake ya barabara Lukumay anaona kwamba Serikali za Afrika Mashariki zinapaswa kuchukua hatua ya kuboresha miundombinu ya barabara ambazo nyingi ziliengwa miongo mingi iliyopita.

''Barabara zetu zilijengwa takriban miaka 30 iliyopita ,na barabara hizi wakati zinajengwa zilijengwa kwa makadirio ya kupita magari 10000 kwa wiki , lakini sasa hupita magari takriban 60000 kwa wiki, hivyo matumizi ya barabara yameongezeka. Na kwa miaka yote Bandari ya Dar imekuwa ikitegemea barabara katika usafirishaji wa mizigo kutoka bandarini.''

''Wadau waelewe athari za sheria, wenzetu wa Zambia na wa Congo wameanza kuleta mgomo kutumia Bandari ya Dar es Salaam kwa sababu mtu hawezi kutumia gharama zilezile za usafirishaji kwa mzigo mdogo.Magari ya Tanzania yanayokwenda Congo hunyimwa mzigo wakati wa kurudi.''

Kiongozi huyu wa waendesha malori anatoa ombi kuwa Tanzania itazame upya sheria hii waahirishe matumizi yake ili kwanza ufanyike mchakato wa kushawishi nchi za SADC ambazo ni watumiaji wakubwa wa barabara za Tanzania katika kusafirisha mizigo kutoka bandari ya Dar es Salaam watumie sheria hii pia.

Ruka X ujumbe
Ruhusu maudhui? (Mitandao ya kijamii)

Mkala hii imebeba madhui yaliyotoka kwenye mitandao ya kijamii. Tunaomba ruhusa yako kabla kitu chochote hakija pakiwa, sababu wanaweza wakawa wanatumia Cookies na tekinolojia nyingine. Unaweza ukasoma sera sera ya kutumia cookies katika mitandao ya kijamii kabla ya kukubali. Kutazama maudhui haya chagua accept and continue

Onyo: Imetoka kwingine na inaweza kuwa na matangazo

Mwisho wa X ujumbe

Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo Zitto Kabwe anaona kuna athari kadha wa kadha iwapo sheria hii ya udhibiti uzito wa magari itaendelea kutumika, anasema Tanzania itapoteza kiasi kikubwa cha fedha kutoka kwa nchi za SADC zinazotegemea Bandari ya Dar es Salaam.

''Kama malori kutoka Zambia kwa mfano ikiwa hayatafika Tanzania kuchukua mafuta, Tanzania itapata hasara iwapo itatekeleza sheria hii na hasara hii ikiwa ni ukosefu wa ajira kwa watanzania wanaoendesha malori, mabenki yatapata hasara kwasababu wawekezaji wamenunua magari ambayo hayaendi sambamba na sheria hii mpya''

''Tanzania imepoteza heshima yake kwenye jumuia za kimataifa, Tanzania ingetumia diplomasia yake kushawishi nchi za SADC kuwa na sheria hiyo hiyo ya nchi za Afrika Mashariki na kwa maana hiyo Dar es Salaam ingeendelea kuwa bandari chaguo kwa nchi za Zambia,Malawi na Congo.''Alimalizia Zitto.