Uchaguzi wa Nigeria 2019: Atiku Abubakar amkabili Muhammadu Buhari

Chanzo cha picha, Reuters/AFP
Kura za uchaguzi uliokuwa na ushindani mkali zimeanza kuhesabiwa nchini Nigeria , huku muda wa kupigia kura ukiongezwa katika baadhi ya maeneo kufuatia kucheleweshwa Jumamosi Alfajiri.
Mpinzani mkuu wa rais Muhammadu Buhari 76 ni aliyekuwa makamu wa rais wa zamani Atiku Abubakar, 72.
Yeyote atakayeibuka mshindi atalazimika kuzungumzia swala la ukosefu wa umeme , tishio la usalama na hali mbaya ya kiuchumi.
Uchaguzi huo ulitarajiwa kufanyika wiki iliopita lakini ukacheleweshwa dakika ya mwisho kutokana na matatizo ya kimipango.
Rais Buhari alipiga kura yake nyumbani kwao huko Daura kaskazini mwa jimbo la Katsina.
Alipoulizwa iwapo angempongeza mpinzani wake iwapo angeshinda alisema 'nitajipongeza mwenyewe'.
Mashambulio yalioripotiwa
Takriban saa mbili kabla ya uchaguzi huo kuanza siku ya Jumamosi, wakaazi wa mji wa Maiduguri , mji mkuu wa jimbo la Borno katika eneo la mashariki kaskazini mwa mji waliripoti kusikia milipuko kadhaa na milio ya risasi.
Maafisa wa polisi katika jimbo hilo katika taarifa walisema kuwa hakuna tisho lolote .
Milio hiyo ya risasi haikuwa ikiwalenga raia lakini ilifanyika kutokana na hali ya usalama , ilisema taarifa.
Jimbo la Borno ndio eneo linalotoka kundi la wapiganaji wa Boko Haram ambalo lilisema kuwa lilipanga kuvuruga uchaguzi huo.
Katika jimbo la kaskazini mashariki la Yobe, watu wanaotuhumiwa kuwa wapiganaji walishambulia mji wa Geidam wakiwalazimu watu kutoroka , chombo cha habari cha Reuters kimesema.
Kwa nini uchaguzi huo ulicheleweshwa?
Kura hiyo iliahirishwa katika mkutano na vyombo vya habari uliowashangaza wengi mapema siku ya Jumamosi tarehe 16 , saa tano kabla ya vituo vya kura kufunguliwa.

Chanzo cha picha, AFP
Tume huru ya uchaguzi nchini Nigeria imetoa sababu kadhaa za kucheleweshwa kwa shughuli hiyo ikiwemo jaribio la kukandamiza kura hiyo na maswala ya kimipango kama vile hali mbaya ya hewa na matatizo ya kuwasilisha makaratasi ya kupigia kura vituoni.
Inec ilisema kuwa mipango yote ilikuwa imakamilika kwa kura hiyo kufanyika.
Sheria za uchaguzi huo
Mgombea mwenye kura nyingi atatangazwa mshindi katika raundi ya kwanza iwapo mtu huyo atajipatia asilimia 25 ya kura, thuluthi mbili ya majimbo 36 ya Nigeria.
Kuna wagombea 73 waliosajiliwa katika uchaguzi huo wa urais , lakini kampeni zilitawaliwa na viongozi hao wawili wakuu

Chanzo cha picha, AFP
Chama tawala cha All Progressives Congress (APC) kimeapa kulisogeza taifa hilo mbele kikidai kuwa katika awamu ya kwanza bwana Buhari amefanya mengi ya msingi ambayo bado hayajaonekana.
Bwana Aboubakar na chama chake cha People's Democratic Party wameahidi kulirudisha taifa la Nigeria katika kazi kikisema kuwa rais Buhari amepoteza muda wote wa miaka minne aliyopewa.
Wagombea wote wawili wanatoka katika eneo la kaskazini lenye Waislamu wengi, Huku wote wakiwa katika miaka yao ya 70, nusu ya wapiga kura milioni 84 katika taifa hilo la Nigeria wako chini ya umri 35
Je ni maswala gani yanayopiganiwa?
Nigeria ambalo ndio taifa kubwa kwa uzalishaji wa mafuta barani Afrika limekabiliwa na ufisadi na ukosefu wa kutumia mafuta hayo kuwekeza kuameathiri maendeleo nchini humo.
Taifa hilo lilikumbwa na kuanguka kwa uchumi wake 2016 na kuimarika kwake polepole kunamaanisha kamba hakuna kazi za kutosha kukabiliana na idadi kubwa ya vijana wanaotarajiwa kuajiriwa.
Kwa sasa karibia robo ya watu wanaotarajiwa kuajiriwa hawana kazi.














