'Nimekua nikijiuliza ni nani baba ya watoto wangu, sikuwaza jambo lingine'

Richard Mason
Maelezo ya picha, Richard Mason

"Nilihisi kama mtu aliyemgongwa na nyundo."

Alisema mfanyibiashara mashuhuri wa Uingereza Richard Mason, mwenye umri wa miaka 54.

Mason anasema kilichomshutua zaidi ni kwamba daktari alimfahamisha kuwa alikuwa na ugonjwa unaofahamika kama cystic fibrosis uliomfanya kupoteza nguvu ya kuzalisha tangu alipokua mdogo.

Hali iliyomaanisha kuwa yeye sio baba ya watoto wake watatu aliyodhani amezaa na mke wake wa zamani, Kate.

"Nilifahamishwa kuwa wanaume wote wanaougua cystic fibrosis hawana uwezo wa kuzalisha,"milionea huyo aliiambia kituo cha BBC Radio 5 Live.

Uchunguzi wa DNA katika maabara

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Uchunguzi wa DNA katika maabara

"Nilidhani pengine nimepewa majibu ambayo si sahihi,lakini daktari alinihakikishia kuwa ana uhakika kuhusu uchunguzi wake na kwamba nahitaji kuzungumza na mtalaka wangu kuhusu baba wa watoto wetu."

Mason alienda kufanyiwa uchunguzi wa kimatibabu baada ya mke wake wa sasa ,Emma, kushindwa kupata mimba.

Utapeli wa uzazi

Alijadiliana kuhusu suala hilo na Kate, aliyekua wametalakiana nae mwaka 2007 baada ya miaka 20 ya ndoa, alimwambua mapacha wake Ed na Joel, 19, na Willem (23) ni wanawe.

Hata hiyo uchunguzi wa DNA umekanusha madai hayo.

"Kwa muda mrefu ugunduzi huo umenipatia usumbufu wa kimawazo,"Mason alielezea.

Jaji mahakamani

Chanzo cha picha, Getty Images

"Nimekua nikijiuliza ni nani baba ya watoto wangu, sikuwaza lingine."

Richard alimshitaki mtalaka wake kwa utapeli mwezi Novemba mwaka jana na amekubali kumlipa dola 320,000 kwa kumharibia sifa kutokana na dola zaidi ya milioni tano alizolipwa walipoachana.

Hata hivyo jaji alimkubalia Kate kutomtambulisha baba wa watoto wake.

''Kate( mtalaka wa Mason)amekataa kumtaja baba watotor - Lakini kwa nini ameamua kufanya hivyo kwa kweli hatuelewi hilo kabisa'' aliliambia gazeti la Daily Telegraph wakili Roger Terrell.

Richard Mason na mke wake wa sasa

Chanzo cha picha, Facebook

Maelezo ya picha, Richard Mason na mke wake wa sasa

"Kuna wakati vijana hawa watataka kumjua baba yao mzazi - na wakati huo ukifika nitawafahamisha. Sijui kama baba yao ni mmoja wa marafiki wangu wa karibu," Mason anaamini.

"Huenda ni mtu wa karibu sana na mimi, mawazo hayo hunijia kila nikiwaangalia vijana wangu wakicheza mpira wa miguu au magongo. Kwa kweli sijui," aliiambia BBC.

"Ukijipata katika hali kama hii ambayo inaathiri maisha yako kwa kiwango kibwa hivi,bila shaka ungelipenda kumjua mhusika mkuu," aliongeza.

Mfanyibiashara huyo sasa ameahidi zawadi ya dola 6,400 kwa mtu yeyote atakaemsaidia kubaini baba mzazi wa watoto wake.

Gazeti la Daily Mail la Uingereza, limeripoti kuwa Mason anaamini watoto wake huenda wamezaliwa na mwanamume ambaye amekuwa na uhusiano wa kimapenzi na mke wake wa zamani miaka ya 1990- alifanya kazi na katika benki ya Barclays, tawi la London ambako Kate alikua akifanya kazi.

Juhudi ya BBC kupata tamko la Katekuhusiana na suala hili hazikufanikiwa.

Hakuna mawasiliano

Kisa hiki kimemuacha na masikitiko makubwa Mason, baada ya watoto wawili kukatiza mawasiliano nae.

"Naona kile wanachofanya katika mtandao wa kijamii wa Facebook na hilo linanivunja moyo sana. Mkubwa wao alifuzu chuo kikuu siku chache zilizopita na hakuna mtu aliyenialika," aliliambia gazeti la Daily Mail.

Siku hizi ni Ed, mmoja wa mapacha hao, anaewasiliana na Mason.

Lakini wiki iliyopita Joel, pacha wa Ed alivunja kimya chake kwa Daily Mail na kukosoa vikali tabia ya Mason.

''Yeye ni mtu mwenye ubinafsi na sio aina ya mtu ungelipenda kuwa pamoja naye. Nilianza kugundua hilo nilipokua na umri wa miaka 15'' alisema.

Kando na hilo kijana huyo amesema hana haja ya kumjua babake mzazi.

"Richard ni baba yangu sina haja ya kumjua baba mwingine. Sidhani hata kama yuko hai."