'Yohana wa Mungu' anayelaumiwa kwa kuwanyanyasa wanawake ajisalimisha kwa polisi Brazil

Chanzo cha picha, AFP/Getty Images
Tabibu wa kiroho nchini Brazil ambaye analaumiwa kwa kuwanyanyasa kingono zaidi ya wanawake 300 amejisalimisha kwa polisi, kwa mujibu wa vyombo vya habari.
Joao Teixeira de Faria, ambaye pia anafahamika kama 'Yohana wa Mungu' alitangazwa kuwa mtoro baada ya tarehe aliyopewa ya kujisalimisha kwa mamlaka kukamilika.
Madai dhidi yake yalianza mapema Disemba wakati wanawake kadhaa walidai kuwa tabibu hiyo wa kiroho alikuwa amewanyanyasa kwenye kliniki yake.
Bw Faira anakana madai hayo.
Tabibu huyo ana makao yake mji ulio kati kati mwa nchi wa Abadiania magharibi mwa mji mkuu Brasilia, lakini ana wafuasi kote duniani.
Alijisalimisha kwa njia gani?
Gazeti la O Globo linasema kuwa dhehebu hilo lilitoa dola milioni 8.9 kutoka benki kadha siku ya Jumatano na kuashiria kuwa huenda alikuwa na njama ya kuikimbia Brazil au kuficha pesa hizo ikiwa labda atahitajika kulipa fidia.

Chanzo cha picha, AFP
Mamlaka zilijibu kwa kutangaza waranti wa kukamatwa siku ya Ijumaa.
Siku ya Jumapili, video ya simu iliyopeperushwa na kituo cha televisheni cha Globo ilimuonyesha Bw Faria akitoka kwenye gari na kujisalimisha kwa polisi huko Abadiania.
Alisafirishwa kwenda makao makuu ya polisi huko Goiania, mji mkuu wa jimbo Goias.
Wakili wake Alberto Toron, alisema atakata rufaa Jumatatu. Alisema alikuwa na matumaini kuwa Bw Fariqa anaweza kuwekwa kwenye kifungo cha nyumbani badala ya jela.
Madai dhidi yake yalianza vipi?
Wiki iliyopita mpiga picha raia wa Uholanzi Zahira Leeneke Maus, aliiambia televisheni ya Globo kuwa Bw Faria alimshauri kufanya vitendo vya ngono na kisha kumbaka.
Wanawake tisa raia wa Brazil ambao hawakutajwa majina, pia waliiambia televisheni hiyo kuwa tabibu huyo aliwanyanyasa kwa misingi kuwa alikuwa akiwapa nguvu za kuwasafisha.

Chanzo cha picha, Reuters
Baadaye gazeti la O Globo lilisema kuwa lilikuwa limezungumza na wanawake wawili zaidi ambao walikuwa na madai kama hayo.
Wajumbe wa tabibu huyo mwenye miaka 76 wanasema anakataa madai ya kuhusika kwenye mambo yaliyo kinyume na sheria wakati akitoa matibabu.
Bw Faria, ambaye mwenye si daktari, awali alipigwa faini na hata kufungwa kwa kuhudumu bila leseni.
Mtangazaji wa runinga nchini Marekani Oprah Winfrey alisafiri kwenda nchini Brazil mwaka 2013 na kushuhudia akitoa matibabu kwenye kliniki yake.












