Chokoleti tani moja yamwagika barabarani Ujerumani

Maafisa katika mji mmoja magharibi mwa Ujerumani walilazimika kuifunga barabara moja baada ya tani moja ya chokoleti kumwagika barabarani.

Trela moja lililokuwa linasafirisha chokoleti hiyo majimaji kutoka kiwandani lilipata ajali na chokoleti kumwagika barabarani katika mji wa Westönnen baadaye Jumatatu.

Chokoleti hiyo iliganda upesi na kuwa gumu kutokana na baridi kali.

Inakadiriwa kwamba chokoleti hiyo ilifunika barabara eneo la ukubwa wa mita 10 mraba.

Iliwalazimu maafisa 25 wa zima moto kutumia sepetu, maji moto na mienge ya kutoa hewa yenye joto sana kusafisha barabara hiyo.

Wafanyakaziwa kiwanda cha chokoleti cha DreiMeister pia walisaidia katika 'operesheni' hiyo.

"Licha ya kisa hiki cha kusikitisha, hatutarajii kwamba chokoleti zitaadimika msimu huu wa Krismasi," idara ya zima moto ilisema.

DreMeister wamewaambia waandishi wa habari kwamba kiwanda hicho kingerejelea shughuli zake za kawaida za uzalishaji baadaye Jumatano.

Unaweza kusoma pia: