Jamal Khashoggi: Mwendesha Mashtaka Saudia ataka waliomuua mwanahabari wapatiwe adhabu ya kifo

Khashoggi

Chanzo cha picha, EPA

Ofisi ya Mwendesha Mashtaka Mkuu nchini Saudi Arabia imemaliza uchunguzi wake juu ya nani aliyeamuru kuuawa kwa mwanahabari Jamal Khashoggi na kufikia kikomo kuwa haikuwa Mwanamfalme Mohammed bin Salman.

Uchunguzi huo umebaini kuwa mauaji hayo yaliamuriwa na afisa mwandawizi wa idara ya usalama wa taifa ya Saudia ambaye alipewa kazi ya kumshawishi Khashoggi kurejea Saudia. Mwanahabari huyo ambaye alikuwa kinara wa kumkosoa Bin Salman alikimbia Saudia mwaka 2017 na kuhamia Marekani.

Kwa mujibu wa msemaji wa ofisi hiyo, Khashoggi alidungwa sindano ya sumu baada ya purukushani kuibuka ndani ya ofisi ndogo za ubalozi wa nchi hiyo jijini Istanbul, Oktoba 2, 2018.

Watu 11 tayari wameshafunguliwa mashtaka kutokana na mkasa huo na waendesha mashtaka wanataka watano kati yao kupatiwa adhabu ya kifo. Uchunguzi unaendelea kwa watu wengine 10 ambao wanshukiwa kushiriki mauaji hayo.

Katika mkutano na waandishi wa habari, Naibu Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Saudia Shalaan bin Rajih Shalaan amesema mwili wa Khashoggi ulikatwa katwa ndani ya ubalozi baada ya kuuawa.

Vipande hivyo vya mwili vilikabidhiwa kwa mshirika wao ambaye ni raia wa Uturuki nje ya ubalozi. Tayari picha ya kuchora ya mshirika huyo imetolewa na uchunguzi unaendelea kujua vipande hivyo vya mwili vilipelekwa wapi.

Bwana Shalaan hata hivyo hakuwataja wale ambao wamefunguliwa mashtaka juu ya tukio hilo.

A man wearing a mask of Saudi Crown Prince Mohammed bin Salman at a protest outside the Saudi consulate in Istanbul, Turkey (25 October 2018)

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Waandamanaji wakionesha hisia kali kuwa Mwanamfalme Mohammed bin Salman anahusika na mauaji

"Uchunguzi wetu umebaini kuwa aliyeamuru mauaji ni kiongozi wa timu ya ushawishi aliyetumwa Istanbul na Naibu Mkurugenzi wa Usalama Generali Ahmed al-Assiri kumtaka Khashoggi kurudi nyumbani," amesema Shalaan.

"Mwanamfalme bin Salman hakuwa na taarifa yeyote ya kilichokuwa kinaendelea," alisisitiza.

Mwanamfalme Mohammed, ambaye ni mtoto wa Mfalme Salman ndiye anayetawala nchi ya Saudia kutokana na baba yake kuwa mgonjwa amejitetea kuwa hakushiriki kwa namna yeyote ile. Na pia amesema mauaji hayo ni "kosa kubwa la jinai ambalo halina utetezi".

Wakosoaji wake hata hivyo wanasema kuwa uwezekano ni mdogo sana kuwa hakuwa na taarifa juu ya operesheni hiyo.

Khashoggi

Chanzo cha picha, EPA

Maelezo ya picha, Picha za watu wanaoaminika kushiriki operesheni ya kumuua Khashoggi

Watu 21 waliokamatwa kutokana na tukio hilo wamekuwa wakionekana katika shughuli mbali mbali za kiusalama za Saudia. General Assiri na kigogo mwengine Saud al-Qahtani wamefutwa kazi kutokana na tukio hilo.

Shalaan amesema Qahtani amezuiwa kutoka nje ya Saudia na anaendelea kuchunguzwa. Hata hivyo hakusema chochote kuhusu Generali Assiri.

Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan amesema "amri ya kumuua Khashoggi imetoka kwenye mamlaka za juu kabisa za serikali ya Saudia" lakini haamini kuwa ilitolewa na Mfalme Salman.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki Mevlut Cavusoglu hata hivyo amesema baadhi ya kauli za Shalaan haziridhishi.

"Wanasema mtu huyu aliuawa sababu alipambana, lakini mauaji hayo yalipangwa kabla," aliwaambia waandishi.

Khashoggi

Chanzo cha picha, AFP/GETTY

"Tena,wanasema mwili wake ulikatwa katwa...lakini hili si jambo la kukurupuka. Vifaa vya kutekeleza hilo na watu wa kulifanya waliingizwa nchini na baadaye kutekeleza."

Maafisa wa Uturuki awali walisema kuwa mmoja wa maafisa usalama 15 wa Saudia walioingia Uturuki kumuua Khashoggi alikuwemo mtaalamu wa kuchunguza sababu ya vifo ambaye aliingia nchini humo na msumeno.

"Wale ambao walitoa amri na kuchochea watajwe na mchakato huu usizibwe," amesema Cavusoglu na kuongeza kuwa Uturuki "itatoa mwangaza wa mauaji haya katika hatua zote."