Uchaguzi Marekani 2018: Ilhan Omar na wanawake walioibuka na ushindi wa aina yake

Ilhan Omar

Chanzo cha picha, Reuters

Baada ya heka heka za uchaguzi usiku kucha Marekani, chama cha rais Donald Trump cha Republican kimedhibiti bunge la Seneti na cha Democrat sasa kinadhibiti bunge la wawakilishi.

Na kwa mara ya kwanza, wanawake wawili waislamu, katika jimbo la Michigan Rashida Tlaib na wa jimbo la Minnesota Ilhan Omar wamechaguliwa katika bunge la Marekani.

Bi Omar, mwanamke mwenye umri wa miaka 36, mdogo kuwahi kuchaguliwa bungeni, alihamia Marekani akiwa na umri mdogo.

Amemshinda mwanachama wa Republican Jennifer Zielinski na kukishinda kiti kuliwakilisha jimbo la Minnesota bungeni.

Uchaguzi Marekani

Chanzo cha picha, Getty Images

Ilhan na Rashida Tlaib wa jimbo la Michigan wamekuwa wanawake wawili wa kwanza wa kiislamu kuchaguliwa katika bunge la Marekani.

Katika mahojiano na BBC mwaka 2016 Ilhan ameeleza ni kwanini ni muhimu sana kuwa mwanamke tena muislamu, ni mambo muhimu katika historia yake.

Ameleezea kwanza ugumu wa ushindani dhidi ya kiongozi mwenye umri uliomzidi wake, na pia ugumu wa kuwa mgombea nchini Marekani akiwa ni mgeni kutoka jamii ya Wasomali.

Anasema nafasi yake ilikuwa finyu kupokewa katika jamii ambayo iliona ni afadhali kuwepo mgombea mwanamume ikilinganishwa na mgombea wa kike.

Hatahivyo, anasema alipata moyo sana kutokana na vijana wengi kumuunga mkono.

Huenda hapo ndipo safari yake ya uongozi ilipoanzia.

Ilhan Omar ni mwanasiasa nchini Marekani aliyezaliwa nchini Somalia kutoka Minnesota

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Ilhan Omar ni mwanasiasa nchini Marekani aliyezaliwa nchini Somalia kutoka Minnesota

Safari ya Ilhan Omar kisiasa

  • Ilhan Omar alizaliwa Oktoba 4, 1981 ni mwanasiasa nchini Marekani aliyezaliwa nchini Somalia kutoka Minnesota.
  • Alizaliwa Mogadishu na alilelewa Baydhabo, Somalia.
  • Baadaya vita kuzuka nchini Somalia mnamo 1991, familia yake ilitoroka na kukimbilia katika kambi ya wakimbizi nchini Kenya.
  • Alifuzu katika chuo kikuu cha North Dakota State katika sayansi ya siasa na masuala ya kimataifa mnamo 2011
  • Alichaguliwa kupitia chama cha Democtratic mnamo 2016, kuwa mwakilishi katika bunge la wawakilishi katika jimbo la Minnesota, na kuweka historia kuwa mbunge wa kwanza wa raia wa Marekani mzawa Somalia kuchaguliwa uongozini Marekani.
  • Yeye ni mkurugenzi wa sera na miradi ya mtandao wa wanawake.
  • Na sasa amechaguliwa katika bunge la wawakilishi Marekani.

Ilhan ameeleza ina umuhimu mkubwa na anatumai inatoa matumaini, kuwa mwanamke wa jamii ya nje ya Kisomali, anayevaa hijab ameapishwa akiwa ameshikilia msahafu au Qurani kubwa.

Ujumbe ni kwamba chochote linawezekana.

Huku tukizungumzia kuhusu matokeo ya aina yake ya kwanza, ni muhimu kutambua pia Jared Polis wa Colorado, amekuwa gavana wa kwanza aliye kwenye uhusiano wa jinsia moja nchini Marekani.

Katika jimbo la New York Alexandria Ocasio-Cortez; ni Mmarekani wa asili wa kwanza kuchaguliwa bungeni.