Maswali mengi kuhusu kwa nini simba jike akamuua mwenzake baba wa wana simba wake?

Chanzo cha picha, Reuters
Simba jike kwenye makao ya kuwatunza wanyama nchini Marekani amemuua simba wa kiume baba ya wana simba wake katika kisa ambacho wataalamu wanasema ni cha kushangaza.
Simba hao walikuwa wameishi pamoja huko Indianapolis kwa miaka nane.
Kulingana na makao hayo ya kuwatunza ni kwamba, hakujakuwa na kisa chochote cha mzozo kati ya simba hao kabla ya shambulizi la wiki iliyopita
BBC iliwauliza watafiti wa simba kuhusu kile wanafikiria kiliweza kuchangia shambulizi hili.
Kipi kilitokea?
Zuri, 12, alimshambulia Nyack, 10, na wafanyakazi hawakufaulu kuwatenganisha. Nyack alikufa kwa kukosa hewa huku Zuri akijeruhiwa.
Makao hao yanasema yanafanya uchunguzi wa kina.

Chanzo cha picha, Reuters
Prof Craig Packer, mkurugenzi wa kitengo cha utafiti wa Simba chuo cha Minnesota, aliiambia BBC kuwa shambulizi kama hilo halikutarajiwa.
"Tumeona mifano ya simba wa kiume wakiua simba wa kike na makundi ya simba wa kike wakiwafukuza simba wa kiume, lakini simba wa kike kumuua simba wa kiume? "hilo sijaliskia sijalisikia."
Ni vipi tabia hii si ya kawaida kwa Simba?
Paul Funston, mkurugenzi wa shirika la Panthera, ambalo linahusika na kuwatunza wanyama pori kama simba, alikiri kuwa kisa hicho ni cha kushangaza.
Msituni kundi la simba wa kike hushambulia simba wa kiume kuwalinda wana simba wao na visa kama hivyo vimerekodiwa kwenye mbuga za wanyama pori. Hata hiyo Bw Funston alisema hajaona kisa kama hicho kilichosababisha kifo.

Chanzo cha picha, EPA
Simba wa kiume kawaida huwafukuza wana simba wa kiume wakati wanakua kuhakikisha kuwa wamebaki peke yao na simba wa kike. Wakati mwingine simba wa kiume huwaua wana simba wakati haswa wanataka kuchukua himaya mpya ili wawezi kuwadhibiti simba wa kike.
Simba wa kiume pia wanafahamika kuwa wakali kwa simba wa kike na wanaweza kuwaua simba wa kike wanaokataa kujamiana nao.
Bw Funston anasema kuwa Zuri ambaye anatajwa kuwa mama mwenye kuwalinda watoto alikuja kumuogopa Nyack hali iliyosababisha wapigane.
"Hata kama wanyama ni watulivu au wanaonekana kuwa watulivu, haimaanishi kuwa hawapitii misukosuko," Bw Funston alisema.

Chanzo cha picha, Courtesy Bruce Patterson, Field Museum
Bruce Patterson, mtafiti huko Field Museum in Chicago, anasema anafahamu visa wa simba wa kike ambao wamewashambulia na kuwajeruhi simba wa kiume wanaowakawsirisha. Kinyume na kisa cha makao hayo hakuna hata mmoja alishika koo la simba wa kiume.
Bw Funston ambaye amefanya uchunguzi kuhusu Simba kwa maika 25 anakubali kuwa kisa hiki si cha kawaida.












