Daraja la Hong Kong-Zhuhai: Daraja refu zaidi duniani kwa picha
Daraja refu zaidi duniani ambalo lina umbali wa 55km (maili 34), linalofahamika kama daraja la Hong Kong-Zhuhai-Macau limefunguliwa rasmi.
Daraja hilo linapatikana katika mlango wa Mto Pearl na linasifiwa kama ufanisi mkubwa wa kihandisi.

Chanzo cha picha, Getty Images
Daraja hilo lina pia njia ya chini kwa chini na linaunganisha visiwa vya Hong Kong na China bara kupitia Macau.

Chanzo cha picha, Reuters
Kutoka mwanzo wake hadi mwisho wake, ukishirikisha pia barabara mbili zinazoliunganisha, daraja hilo urefu wake ni mara 20 zaidi ya daraja maarufu la Golden Gate linalopatikana San Francisco.

Chanzo cha picha, Reuters
Daraja hilo limejengwa kuhimili mitetemeko ya ardhi na vimbunga ambavyo mara kwa mara hukumba eneo hilo.
Limejengwa pia kuhimili kugongwa na meli iwapo ajali kama hiyo itatokea.

Chanzo cha picha, AFP
Ili kuziwezesha meli kupitia mlango huo wa mto, daraja hilo linafikia wakati na kuingia chini ya maji, na kuwa barabara ya chini kwa chini ya urefu wa 6.7km, kupitia visiwa viwili bandia, kwa maana kwamba visiwa hivyo ni vya kujengwa na si asilia.

Chanzo cha picha, Reuters
Mradi huo wa ujenzi unapitia katika eneo ambalo hupitia ndege zikipaa na zikienda kutua katika uwanja wa kimataifa wa Hong Kong.
Hii iliwalazimu wahandisi kuhakikisha kwamba daraja hilo haliendi juu sana.

Chanzo cha picha, Reuters
Ujenzi wa mradi huo ulianza mwaka 2009 lakini ulicheleweshwa mara kwa mara na pia kukawa na wasiwasi kuhusu usalama wake.
Aidha, gharama yake ya ujenzi imekuwa ikipanda mara kwa mara na kwa jumla sasa inakadiriwa limegharimu zaidi ya $20bn (£15.3bn).

Chanzo cha picha, AFP
Mwanzoni ilitarajiwa daraja hilo lingefunguliwa rasmi mwaka 2016 lakini hata tarehe kamili ya uzinduzi wake mwezi huu haikuwa imethibitishwa, hadi ilipobainishwa jana kwamba lingezinduliwa leo.

Chanzo cha picha, Reuters
Sio tu kwamba ujenzi wa daraja hilo umepita bajeti pia na muda uliokadiriwa kutumika kulijenga bali pia limegharimu maisha ya watu.
Maafisa wa Hong Kong na China wanasema kwamba wajenzi tisa walifariki wakati wa ujenzi wa daraja hilo.

Chanzo cha picha, AFP
Daraja hili linaunganisha maeneo matatu ya China - mawili ni ya utawala maalum ya Makau na Hong Kong na eneo la tatu ni China bara.
Hii ina maana kwmaba daraja hili linapitia maeneo yenye mifumo tofauti ya kisheria na kisiasa.

Chanzo cha picha, Reuters
Mabasi na magari ya kibiashara yatasafirisha abiria na mizigo kupitia daraja hilo.
Teksi hata hivyo haziruhusiwi na ni magari machache sana ya kibinafsi ambayo yataruhusiwa kupita.

Chanzo cha picha, EPA
Mtu anapokuwa anasafiri kati ya Hong Kong na China bara huhitajika kuwa na visa. Vituo viwili vya uhamiaji vimejengwa kuwahudumia watu watakaokuwa wanatumia daraja hilo kusafiria.

Chanzo cha picha, Reuters
Nini sababu ya kulijenga daraja hili? Kuokoa muda. Safari kupitia mlango huo wa mto huchukua zaidi ya saa nne. Sasa kwa kutumia daraja hilo, safari hiyo itachukua dakika 30 pekee.

Chanzo cha picha, Reuters
Lakini baadhi ya wakazi Hong Kong wamekosoa nia ya kujengwa kwa daraja hilo, wakisema hakuna anayelihitaji sana.
Wanasema zaidi ni jaribio la kuiunganisha zaidi Hong Kong na China bara kikamilifu.
Hong Kong ni eneo linalojitawala ambalo lilikuwa koloni ya Uingereza hadi lilipokabidhiwa tena kwa China mwaka 1997.
Unaweza kusoma pia:
Picha zote zina hakimiliki












