Mohamed Dewji: Bilionea Mtanzania Mo Dewji alivyotekwa alfajiri hotelini Dar es Salaam

Muda wa kusoma: Dakika 2

Vyombo vya usalama nchini Tanzania vimesema kuwa vinaendelea na uchunguzi na msako wa kumtafuta mmoja wa matajiri wa umri mdogo zaidi barani Afrika Mohamed Dewji, 43, ambaye alitekwa nyara mapema leo asubuhi na watu wasiojulikana.

Mfanyabiashara huyo alitekwa akiwa hana walinzi wowote na hata gari alilokuwa analitumia alikuwa anaendesha mwenyewe.

Watu wawili wasiofahamika ambao wanasemekana kuwa sio raia wa Tanzania (Wazungu), walikuwa wameziba nyuso zao wakati walipofika kumteka katika hotelini.

Walioshuhudia wanasema kuwa waliona risasi ikipigwa juu na akikamatwa kupelekwa katika gari la watekaji nyara hao.

Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama na mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda amesema juhudi za kumpata akiwa hai na salama zinafanyika na kuwapata wahalifu waliomteka.Ingawa kwa sasa watu watatu tayari wameshikiliwa na polisi.

Mo Dewji ni nani?

Kwa mujibu wa jarida maarufu la masuala ya fedha la Forbes, ana utajiri wa dola bilioni 1.5.

Mo mwenye umri wa miaka 43 ndiyo tajiri namba moja Afrika Mashariki, na pia miongoni ma matajiri wa umri mdogo zaidi Afrika.

"Alinunua viwanda vya nguo na mafuta vilivyokuwa vinamilikiwa na Serikali kwa bei ndogo na kuvifanya viwe na faida zaidi kwa kutumia mtindo wa kisasa wa menejimenti," inaongeza ripoti hiyo.

Mohammed Dewji ni afisa mkuu mtendaji wa kampuni ya METL iliyoanzishwa na baba yake miaka ya 1970.

METL ina viwanda vya kutengeneza nguo na bidhaa nyingine za matumizi ya binadamu vikiwamo vyakula, sabuni na vinywaji. Pia ina mapato yanayozidi Dola 1.4 milioni za Marekani (Sh2.5 trilioni) kwa mwaka.

Katika kampuni hiyo, ambayo imekuwa na ushindani dhidi ya kampuni kubwa nyingine kama Said Salim Bakhresa, Dewji anamiliki asilimia 75 ya hisa zote.

Kwa mujibu wa tovuti yake, METL inaendesha shughuli za uagizaji na usafirishaji bidhaa kutoka na kwenda nje, uzalishaji unaohusisha nguo, vinywaji na vyakula, usagaji nafaka, nishati na petroli na utengenezaji baiskeli.

Pia inahusika na huduma za simu, fedha, kilimo na pia ina kitengo cha kontena kwenye Bandari ya Dar es Salaam.

METL ina shughuli zake katika nchi sita barani Afrika na ina malengo ya kujipanua zaidi katika maeneo zaidi.

Dewji ni mtanzania pekee aliyesaini mkataba mwaka 2016 wa kutoa kwa wahitaji nusu ya mali yake.

Mo Dewji Foundation ndio asasi ambayo aliianzisha ili kutekeleza nia yake hiyo na kazi yake kubwa ni kusaidia watanzania wasiojiweza kwa upande wa afya,elimu na maendeleo jamii.

Mbali na biashara na shughuli za jamii Mo Dewji amewahi kuwai mwanasiasa na mwaka 2005 mpaka 2015,Mohamed Dewji alikuwa mbunge wa Singida Mjini.

Dewji pia ni mpenzi wa michezo na amewekeza katika klabu ya mpira ya Simba ya Tanzania.