Profesa PLO Lumumba azuiwa kuingia Zambia kwa sababu za 'kiusalama', upinzani wasema ni aibu kwa taifa

PLO Lumumba

Chanzo cha picha, eacc

Maelezo ya picha, PLO Lumumba

Profesa wa sheria na mtoa mihadhara maarufu kutoka Kenya Prof PLO Lumumba alizuiwa kuingia nchini Zambia kutokana na sababu za 'kiusalama' kwa mujibu wa mamlaka za nchi hiyo.

Kiongozi wa upinzani nchini Zambia Hakainde Hichilema amesema hatua hiyo imeliletea aibu taifa hilo.

Prof Lumumba, ambaye jina lake kamili ni Patrick Loch Otieno Lumumba, alikuwa atoe hotuba kuhusu ushawishi wa China barani Afrika leo Jumapili katika chuo kikuu cha Eden.

Lakini baada ya kuwasili uwanja wa kimataifa wa Keneth Kaunda mjini Lusaka siku ya Jumamosi, alizuiwa kuingia ambapo alilazimika kurudi nchini Kenya.

"Serikali kupitia idara ya uhamiaji imemzuia kuingia nchini Prof Patrick Lumumba, raia wa Kenya kutokana na sababu za kiusalama," Waziri wa habari na utangazaji Dora Siliya alisema.

Kiongozi wa chama cha upinzani cha United Party for National Development, Hakainde Hichilema amesema hatua hiyo ya kumzuia msomi huyo imeliaibisha taifa hilo.

Bw Hichilema alisema kudhalilishwa kwa Prof Lumumba ni thibitisho ya msimamo wa upinzani nchini humo kwamba serikali ya Zambia inaongozwa na 'viongozi wa kiimla'.

Alisema kudhalilishwa kwa mtu kama huyo maarufu duniani kunaliharibia sifa taifa hilo.

Kwa mujibu wa Bw Hichilema, aliyewania urais dhidi ya Rais Edgar Lungu mwaka 2016, walio hatari kwa Zambia ni wageni ambao wamekuwa wakinyakua ardhi na mali ya umma.

China ndiyo mwekezaji mkubwa nchini Zambia na iko pia kwenye nchi kadhaa za Afrika, ikitoa misaada bila masharti na kandarasi nyingi hupewa Wachina.

Mjini Lusaka na kote nchini, China iko mbioni kujenga viwanja vya ndege, barabara, viwanda na vituo vya polisi huku miradi mingi ikiwa inafadhiliwa na mikopo kutoka China.

Deni la Zambia linakadiriwa kuwa dola bilioni 10.6 lakini kuna shaka kuwa serikali inaficha madeni.