Korea Kaskazini: Hatutaharibu silaha zetu ikiwa vikwazo vitaendelea kuwepo

Ri Yong Ho at the UN

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Ri Yong-ho aliuambia mkutano wa Umoja wa Mataifa kuwa vikwazo hivo vinapunguza imani yake kwa Marekani.

Waziri wa mashauri ya nchi za kigeni wa Korea Kaskazini ameonya kuwa hakuna vile nchi yake itaharibu zana za nyuklia wakati Marekani bado inaendelea kuiwekea vikwazo.

Ri Yong-ho aliuambia mkutano wa Umoja wa Mataifa kuwa vikwazo hivo vinapunguza imani yake kwa Marekani.

Hivi karibuni Korea Kaskazini imerejelea wito wake wa kuitaka Marekani na Umoja wa Mataifa kuondoa vikwazo na imeungwa mkono kutoka China na Urusi.

Lakini uongozi wa Trump unasema kuwa vikwazo hivi vitadumu hadi pale Korea Kaskazini itaharibu zana zake za nyuklia.

Rais Donald Trump na kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong-un walifanya mkutano wa kihistoria mwezi Juni ambapo Bw Kim aliahidi kuharibu zana za nyuklia.

Ri alisema nini?

Alisema Marekani ilikuwa inasisitiza suala la kuharibiwa silaha kwanza, sera ambayo iliongeza idadi ya vikwazo.

"Bila ya imani kwa Marekani hatuwezi kuwa na uhakika kwa usalama wetu wa kitaifa na katika hali kama hiyo hakuna vile tutaharibu silaha zetu kwanza."

"Imani kuwa vikwazo vinaweza kuchangia sisi kusalimu amri ni ndoto," aliongeza.

Kipi kimefanyika tangu mkutano wa Singapore?

Makubaliano yaliyoafikiwa huko yalisema kuwa Korea Kaskazini ingeharibu zana zake za nyuklia lakini hayakuwa na mwongozo au muda au njia kuthibitisha mchakato huo.

Mwezi Agosti Rais Trump aliilaumu China ambaye ni mshirika wa Korea Kaskazini kwa suala hilo kutokana na tofauti zake za kibiashara na Marekani.

Hata hivyo mapema mwezi huu kiongozi wa Korea Kusini Moon Jae -in alifanya ziara ya siku tatu nchini Korea Kaskazini - ikiwa ndio ya kwanza kufanywa na rais wa Korea Kusini mjini Pyongyang kwa miongo kadhaa.

Bw Moon alisema aliweza kuthibitisha kujitolea kwa Kim Jong-un katika kuharibu zana za nyuklia na pia alikuwa na nia ya kukutana tena na Rais Trump hivi karibuni.

Kim pia aliahidi kuharibu eneo kuu la kufanyia majaribio ya makombora.