Rais Magufuli amfuta kazi Naibu waziri wa mambo ya nje

Magufuli

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Rais wa Tanzania John Pombe Magufuli

Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amemteua Dkt. Damas Daniel Ndumbaro kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Dkt. Ndumbaro ambaye ni Mbunge wa Songea Mjini Mkoani Ruvuma amechukua nafasi ya Dkt. Susan Alphonce Kolimba ambaye uteuzi wake umetenguliwa ingawa sababu ya utenguzi huo haikubainishwa.

Wakati huo huo, Rais Magufuli amemteua Dkt. Faraji Kasidi Mnyepe kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Dkt. Mnyepe anachukua nafasi ya Prof. Adolf Mkenda ambaye ameteuliwa kuwa katibu mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii.

Prof. Mkenda amechukua nafasi ya Jenerali Mstaafu Gaudence Milanzi.

Uteuzi wa viongozi hao umefanyika leo tarehe 26 september, 2018 na tarehe ya kuapishwa itatangazwa baadaye.

Rais Magufuli amekuwa akiteua na kutengua mara kadhaa viongozi ambao anaona hawaendani na kasi anayoitaka katika kumletea maendelo ya uchumi wa viwanda.

Mwigulu Nchemba

Chanzo cha picha, Mwigulu/facebook

Miongoni mwa mawaziri walioathirika na shoka la rais Magufuli ni aliyekuwa waziri wa mambo ya ndani ya nchi Mwigulu Lameck Nchemba ambaye uteuzi wake ulitenguliwa.

Mwigulu Nchemba alikuwa amejipatia umaarufu wake kwa juhudi zake za kuzuia maandamano dhidi ya Rais Magufuli.

Licha ya hapo awali alikuwa amehamishwa kutoka wizara ya kilimo, mifugo na uvuvi, hadi wadhfa wake wa mwisho.

Nchemba alisimamishwa kazi baada ya kuhudumu kwa miaka miwili katika baraza la Rais Magufuli.

Waziri wa zamani wa habari Nape Nnauye

Mpema mwaka uliopita rais Magufuli alimvua majukumu yake aliyekuwa waziri wa habari Nnape Nauye siku moja baada yakupokea ripoti ya kamati ya uchunguzi kuhusu uvamizi uliotekelezwa na mtu anayedaiwa kuwa mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda katika studio za kituo cha habari cha kibinafsi cha Clouds.

Kamati hiyo, kwenye ripoti yake, ilionekana kumkosoa Bw Makonda na kusema alitumia vibaya mamlaka yake.

Kamati hiyo ilipendekeza, miongoni mwa mengine, kwamba Bw Nnauye awasilishe malalamiko ya waandishi wa habari dhidi ya mkuu huyo wa mkoa kwa Rais wa Tanzania pamoja na kuanzishwa kwa uchunguzi dhidi ya polisi waliongia na silaha za moto kwenye chombo hicho cha utangazaji.