Ajali ya kivuko cha MV Nyerere na kumbukizi ya safari yangu Ukara

Ilikuwa ni siku ya Alhamisi nikiwa nimekaa nafuatilia taarifa kupitia vyanzo mbalimbali vya habari,ghafla nakutana na taarifa za kuzama kwa kivuko cha MV Nyerere mahala ambapo mwaka jana Januari 2017 nilikuwa katika eneo hilo.
Nilianza kuvuta kumbukumbu za hali ya usafiri niliokuta wakati huo, huku kivuko hiki pekee kikiwa ndiyo tegemeo la usafiri kwa wakazi wa kisiwa cha Ukara.
Ilikuwa ni lazima mtu kulazimika kusubiria kwa siku nzima ili uweze kurejea upande mwingine hata mie nilifuata ratiba hiyo ambayo ilikuwa ni kutokana na kutokuwa na namna nyingine ya usafiri isipokuwa MV Nyerere.

Chanzo cha picha, STEVE MSENGI
Hivyo kusikia na kuona picha kwamba kivuko hiki ambacho nilikipanda sasa kimezama, du! moyo wangu ulikumbwa na simanzi mchanganyiko na uoga kwani hata safari yangu hiyo watu walikuwa si haba kwani tulijazana huku kivuko kina uwezo wa kubeba watu 100 tu.
Safari yote hiyo ilikuwa ni kwamba mvua inyeshe jua liwake nifike katika lile jiwe linalodaiwa kucheza na ambalo limekuwa kivutia ndani na nje ya Tanzania kama sehemu ya utalii, huku kukiwa na mijadala mingi juu ya kucheza kwa jiwe hilo wengine wakihusisha na Imani za kishirikina.
Safari hii ya mwaka jana ilikuwa ni jaribio langu la pili kuhakikisha nafika Ukara, ambapo awali nilishindwa kufika kutokana na sababu za changamoto za usafiri lakini nia ikawa pale pale kwamba nifike na kujionea simulizi za maajabu kisha niweze kuijuza dunia mambo hayo.
Hivyo wakati huu jitihada za kuopoa miili zikiwa zinaendelea huku wafiwa wakiwa katika hali ya kuendelea kupokea pole kutoka kwa wasamaria wema, nimeona niandike mguso wa ndani ya moyo wangu kwa hili lililotokea, ambapo sababu zinazotajwa ikiwemo ya kubeba watu zaidi kwangu niliishuhudia ndani ya kivuko hicho hicho na ilinitisha kwamba Mungu ni mwema.
Je, kama ingelikuwa siku hiyo ndiyo yanatokea madhila haya ningelikuwa wapi leo hii?
Kisiwa cha Ukara ambacho kinajitambulisha kwa simulizi nyingi za kuaminika ambazo si za paukwa pakawa bali zinazohusishwa na imani za kishirikina, kina mambo mengi niliyohadithiwa kama jani la mti kubadilika kuwa Mamba, mara wengine wakidai wanakijiji huko wana mazingaombwe mengi, ni habari ambazo ziliniogopesha lakini nikapiga moyo konde.

Nichukue fursa hii kumshukuru mama Gertrude Mongella ambaye alinitia moyo sana pale nilipomuuliza taarifa za kina kuhusiana na kisiwa cha Ukara.
Kama mama na kiongozi wa muda mrefu aliniondoa hofu kabisa safari ikasonga mbele, na alinisaidia sana kuweza kuniunganisha na watu muhimu kwa lile jambo nililoliendea.

Marehemu kusafiri na abiria walio hai
Lipo jambo ambalo pia siwezi kulisahau, wakati nikiwa narejea kutoka Ukara kuja Mwanza, niliona mtu mmoja aliyekuwa amelala amejifunika huku watu wakiwa wamemuacha alale hapo ,
nikawauliza kwanini huyu analala badala ya kukaa ili kuwe na nafasi ya wengine pia?
oooh nikasikitishwa na majibu kwamba si kama alikuwa amelala usingizi wa kawada,bali alilala mauti yaani alikuwa amekufa,hili siwezi kulisahau.

Chanzo cha picha, Reuters
Walisema kuwa mtu huyo alikuwa anapelekwa hospitalini Ukara ili akatibiwe na akafariki njiani.
Walisisitiza kwamba wangependa siku moja wawe na Boti la ambulance kwa ajili ya kusafirisha wagonjwa wao kwa sababu kituo chao cha afya hakikidhi mahitaji yao.
Leo hii vyote hivi vinanifanya kurejewa na picha ya safari yangu hiyo na watu wa huko waliokuwa wenyeji wangu.

Chanzo cha picha, STEPHEN MSENGI
'Kila nyumba kuna msiba yaani huku,hali ni mbaya'ni maneno ya baadhi ya wenyeji wangu ambao nimekuwa nikizungumza kuwapa pole huko Ukara, wanasema safari kwa siku afadhali zingelikuwa tatu, kujazana huko kusingekuwepo maana safari moja inachukua dakika 45 tu au saa moja.
Lakini kutokana na hili huenda na ni imani yangu kwamba wananchi hao wanaotegemea vyombo vya usafiri wakapatiwa njia mbadala ya kuwarahishia usafiri wao.

Nasema pole sana wana Ukara,Mungu awape nguvu kupita katika kipindi hiki kigumu mnachopitia na ambacho kama taifa kwa ujumla tunapitia.
Bwana alitoa na Bwana ametwaa jina la Bwana libarikiwe Amen.
Mambo gani unastahili kuzingatia unaposafiri kwa feri?
- Panga kuondoka mapema ili upate kuwasili kwa wakati ungali bado mchana
- Zuia kusafiri wakati bahari au ziwa ni chafu au wakati hali ya hewa ni mbaya
- Kama chombo cha usafiri unahisi kimebeba watu wengi kupita kiasi, shuka mara moja
- Mara unapopanda abiria , fahamu kuhusu sehemu zilizo karibu nawe. Hakikisha kuwa maeneo ya kutokea au kutorokea yako salama na pia hakikisha kuwa yako wazi.
- Hakikisha jaketi za uokozi ziko kwenye chombo, ziko wapi hasa na unaweza kuzikifikia wakati wa dharura?
- Vyombo vya kutangaza viko sawa kuweza kutangaza wakati kuna dharura?
- Wahudumu wa chombo wanaweza kuwasiliana na abiria kwa haraka?
- Kama unaamini kuwa sehemu fulani ya chombo haipo sawa, shuka mara moja na fanya mipango tofauti ya kusafiri.














