Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
India Sakkim: Uwanja huo umejengwa katika eneo lenye milima linalotajwa na wahandisi kuwa na mandhari ya kupendeza zaidi duniani.
Uwanja wa ndege wa 100 nchini India uliofunguliwa rasmi na waziri mkuu Narendra Modi katika jimbo la kaskazini mashariki la Sikkim,unasemekana kuwa mzurizaidi duniani.
Sikkim, ni jimbo dogo la kifalme linalopatikana katika eneo la milima ya Himalayas, ambayo ni ya tatu kwa urefu.
Jimbo hilo limeunganishwa na maeneo ya Tibet, Bhutan na Nepal kupitia milima minane.
Uwanja wa kwanza wa ndege katika jimbo hilo uko Pakyong, karibu kilomita 30 sawa na (maili 18) kutoka makao makuu yake ya Gangtok.
Eneo hilo lenye milima limetajwa na wahandisi kuwa na mandhari ya kupendeza zaidi duniani.
Uwanja huo wa ndege umejengwa kwenye eneo la mlima juu ya kijiji cha Pakyong, uko kilomita 60 karibu na mpaka wa India na Uchina.
Uwanja huo wa ndege umejengwa katikati ya mabonde ya kina kirefu pande zote mbili pia unasemekana kuwa na barabara ya kilomita 1.75
Uwanja huo pia una sehemu mbili kubwa ya kuegesha magari pamoja na eneo la abiria 100 kuhudumiwa kwa wakati mmoja.
Kutokana na hali mbaya ya hewa, maradi wa ujenzi ulichukua miaka tisa kukamilika. Msemaji wa kampuni ya Punj Lloyd, anasema
''Tulikabiliwa na changamoto kubwa wakati wa ujenzi lakini kila hatua tuliyopiga ilitupatia matumaini makubwa''
Wahandisi wanasema changamoto kubwa ilikua kusafirisha vifaa vizito vya ujenzi katika eneo la milima lililo na barabara nyembamba.
Mvua kubwa iliyonyesha kati ya miezi ya Aprili na Septemba - katika eneo la Sikkim ilitatiza shughuli ya ujenzi.
Miongoni mwa changamoto zingine walizokumbana nazo wahandisi ni miteremko ya mawe inayozunguka uwanja huo.
Uwanja wote wa ndege, ikiwa ni pamoja na barabara, umejengwa kwenye ardhi ambayo yenyewe iliundwa kwa kujenga ukuta wenye kima cha futi 263ft unaopitia mabonde ya kina.
Punj Lloyd anasema ni moja ya kuta kubwa ''ulio imara'' zaidi duniani.
Ndege za kibiashara zitaanza shughuli zake kutoka mji wa Pakyong Oktoba 4.
Uwanja huo unatarajiwa kukuza na kuimarisha shughuli za utalii katika jimbo la Sikkim, ambalo linasifika kwa kuwa na mandhari ya kuvutia zaidi duniani.
Picha kwa hisani ya Rajiv Srivastava