Rafiki: Uamuzi wa mahakama kuu Kenya kuondosha kwa muda marufuku dhidi ya filamu una maani gani?

Maudhui ya filamu hiyo yanahusisha mapenzi ya jinsia moja

Chanzo cha picha, RAFIKI

Maelezo ya picha, Maudhui ya filamu hiyo yanahusu mapenzi ya jinsia moja
Muda wa kusoma: Dakika 2

Mahakama kuu Kenya imesimamisha kwa muda marufuku ya kupeperushwa kwa filamu ya wapenzi wa jinsia moja Rafiki ilioundwa nchini humo.

Filamu hiyo kuhusu uhusiano wa kimapenzi wa wanawake wawili, tayari imeonyeshwa katika tamasha la filamu la Cannes na sasa inaweza kuwasilishwa katika kuwania tuzo ya Oscar.

Bodi ya kukagua filamu Kenya iliiipiga marufuku filamu ya Rafiki mnamo Aprili kwa misingi ya kwamba inahimiza uhusiano wa kimapenzi wa jinsia moja.

Mahakama kuu leo Ijumaa imebatilisha marufuku hiyo angalau kwa muda, ikiamua kwamba sasa itaweza kupeperushwa kwa watu wazima nchini kwa muda wa siku saba.

Muelekezi wa filamu hiyo - Wanuri Kahiu katika mtandao wa twitter ameelzea furaha yake kufuatia uamuzi huo leo Kenya.

Hatahivyo mkurugenzi mkuu mtendaji wa bodi ya ukaguzi wa filamu Kenya Ezekial Mutua katika ujumbe aliotuma kwenye mtandao wa kijamii Twitter - ameonya kwamba bodi hiyo inatazama kuona ni ukumbi upi wa umma wa kuonyesha filamu utakaoionyesha filamu hiyo pasi na idhini ya bodi hiyo.

Amendelea kueleza kwamba litakuwa janga na aibu kuruhusu filamu za mapenzi ya jinsia moja kuwa kielelezo cha utamaduni wa Kenya.

Hatua hii ina maana gani?

Rafiki, ndio filamu ya kwanza kutoka nchini kenya kuwahi kuonyeshwa katika tamasha la filamu la Cannes.

Tamasha la Cannes, ni miongoni mwa matamasha ya filamu makubwa duniani ikiwa pamoja na tamasha la Oscars. Wanafilamu,watayarishaji na waongozaji wa filamu wanakutana sio tu kushindanisha filamu lakini pia ni nafasi kubwa ya kuuza filamu zao kwa makampuni makubwa.

KFCB iliipiga marufuku filamu hiyo kuonyeshwa hadharani au kutangazwa kwenye televisheni na kusambazwa, ikisema maudhui ya filamu hiyo inayoonesha mapenzi ya jinsia moja kati ya wanawake wawili, inakiuka sheria za Kenya.

Sharti kubwa la filamu hiyo sasa kuweza kujumuishwa katika tuzo ya mwaka ujao 2019 ya Academy chini ya kitengo cha filamu bora ya lugha ya kigeni, ni lazima filamu hiyo ionyeshwe nchini kenya kabla ya mwisho wa mwezi huu Septemba.

Na ikifanikiwa, itakuwa tena ni mara ya kwanza kwa filamu kutoka nchini Kenya kuteuliwa katika kitengo hicho.

Uamuzi wa mahakama umepokewaje?

Kuna walio furahia uamuzi huo wa mahakama kuruhusu kuonyeshwa nchini kwa filamu ya Rafiki wakieleza kuwa ni There is nothing else remotely liberating about this moment.

Baadhi wakieleza matumaini yao kwa kesi hii kuwa mfano kwa nyengine zinazoathirika na marufuku za bodi ya filamu Kenya.

Na kuna waliotazama uamzui huo kama njia ya serikali kuwapumbaza wakenya na mambo mengine yalio muhimu zaidi kama vile mjadala kuhusu mswada wa ushuru.

Mwezi Juni mwaka uliopita, bodi hiyo ilipiga marufuku baadhi ya vipindi vya televisheni katika ving'amuzi vya DSTV na GOTV vilivyosemekana kuunga mkono mapenzi ya jinsia moja.

Vitendo vya mapenzi ya jinsia moja ni kinyume ya sheria kama nchi nyingi barani Afrika.

Tendo la ngono kati ya watu wa jinsia moja inahukumu ya miaka 14 gerezani nchini Kenya.