Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Angela Merkel atua Nigeria katika ziara ya mwisho kwa nchi za Afrika Magharibi
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel yupo nchini Nigeria katika ziara ya mwisho kwa nchi za Afrika Magharibi.
Merkel alionana na wakuu wa nchi za Senegal na Ghana mapema wiki hii.
Ziara hii inalenga kukuza uhusiano wa kiuchumi baina ya Ujerumani na Afrika Magharibi sambamba na kuangalia namna ya kupunguza suala la wahamiaji haramu wanaoingia barani Ulaya.
Safari ya Angela Merkel katika mji mkuu Abuja nchini Nigeria itaangazia maeneo makuu manne ambayo ni ulinzi, uhusiano wa kiuchumi, uhamiaji na uchaguzi mkuu ujao wa Nigeria.
Merkel atakutana na mkuu wa ECOWAS na baadae Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari.
Viongozi hao wawili watajadili njia za za kuboresha uchumi baina ya mataifa hayo mawili yenye nguvu kiuchumi barani mwao.
Merkel amesafiri na wafanyabiashara wakubwa kutoka Ujerumani.
Rais Buhari na Merkel watagusia pia suala la usafirishaji haramu wa watu kuingia Ulaya, huku safari yake kwenda Magharibi mwa Afrika ikichagizwa zaidi na maandamano ya kupinga wahamiaji yaliyofanyika Mashariki mwa Ujerumani siku kadhaa zilizopita.